Makala

WANDERI: Ruto atueleze ukweli kuhusu maovu ya awali

March 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

NI dhahiri kwamba Naibu Rais William Ruto ni kiongozi aliyetengwa serikalini kwa sasa ingawa bado yumo ofisini.

Malalamishi na kauli zake nzito kuhusu njama za kumyamazisha zinamsawiri kama kiongozi anayefahamu mengi kuhusu siri ambazo huwepo serikalini.

Upeo wa malalamishi yake ulikuwa mnamo Jumamosi, baada ya kusema kwamba atawataja maafisa wa serikali ambao wanatumia afisi zao kuwahangaisha watu wanaoonekana kumuunga mkono yeye ama wakitangamana naye.

Kwa kiongozi kama Dkt Ruto, hizi ni kauli nzito na ni matamshi ambayo hayapaswi kuchukuliwa kwa urahisi hata kidogo.

Hata hivyo, ana kibarua kwani kama kiongozi ambaye amekuwepo serikalini tangu 2013, tungemsihi asiwataje tu maafisa hao, bali afichue baadhi ya siri ambazo zimefichika hadi sasa.

Baadhi ya siri hizo ni vifo tata vya watu maarufu, ambavyo vimebaki kuwa siri kwa wengi, hasa baada ya uchaguzi tata wa 2017.

Kwa mfano, ni nani alimuua aliyekuwa Msimamizi Mkuu wa Kitengo cha Habari, Mawasiliano na Teknolojia (ICT) katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Chris Msando?

Nani aliyewaagiza polisi kutumia bunduki kuwaua waandamanaji ambao hawakuwa wamejihami baada ya uchaguzi huo?

Je, serikali ilihusika? Yalikuwa maagizo na amri kutoka kwa wakuu wa polisi?

Kilicho dhahiri ni kwamba, hii itakuwa nafasi nzuri kwa Dkt Ruto kufichua siri hizi zote ili kuondoa giza ambalo limekuwepo kwa muda mrefu.

Tunatumaini kuwa hili litawafanya watu wengine ambao walihudumu katika serikali za marais Mzee Jomo Kenyatta na Daniel Moi kujitokeza pia kueleza baadhi ya siri ambazo zimefichika hadi sasa

Siri hizo ni mauaji tata ya watu binafsi na uandaaji wa ghasia za kikabila zilizoikumba nchi katika miaka ya 1992, 1997, 2002 na 2007/ 2008. Nyingi za ghasia hizo zilitokea katika eneo la Bonde la Ufa.

Na ingawa kumekuwa na juhudi za kutafuta ukweli wa ghasia hizo kupitia michakato wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), matukio hayo bado yamebaki kuwa siri na fumbo kubwa hadi sasa.

Katika utawala wa Mzee Kenyatta, vifo vya watu kama Pio Gama Pinto, Tom Mboya, JM Kariuki kati ya wengine vimebaki kuwa siri.

Chini ya enzi ya Mzee Moi, vifo vya watu kama Dkt Robert Ouko, Titus Adungosi, Askofu Alexander Muge, Kaasisi John Kaiser vimebaki kuwa siri pia.

Mzee Kenyatta alifariki mnamo 1978 bila kutoa kauli yoyote ikiwa alikuwa na ufahamu wa wale waliopanga vifo hivyo. Bw Moi naye alifariki mwezi uliopita na siri nyingi zilizouandama utawala wake.

Kimsingi, hii ni nafasi ya Dkt Ruto na washirika wa Mzee Kenyatta na Bw Moi, ambao bado wako hai, kueleza ukweli kuhusu matukio yaliyoziandama tawala hizo.

[email protected]