WANDERI: Wakenya watasalia watumwa daima dahari
Na WANDERI KAMAU
UCHAGUZI mdogo wa eneobunge la Kibra ambao ulifanyika Alhamisi iliyopita umedhihirisha kwamba Wakenya daima watabaki watumwa wa viongozi wa kisiasa.
Hili linatokana na hali kwamba baadhi ya wanasiasa walioungana kumpigia debe mwaniaji wa ODM Bernard Okoth (Imran), walikuwa mahasimu wakubwa kisiasa.
Mfano mzuri ni hatua ya Gavana Anne Waiguru wa Kirinyaga kuungana na kinara wa ODM Raila Odinga kumpigia debe Bw Okoth.
Kwa vyovyote vile, hawa ni viongozi waliowashangaza wengi kwani wamekuwa mahasimu wakubwa kisiasa kabla ya “handisheki” kati ya Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta.
Ikumbukwe kuwa Bw Odinga ndiye alifichua wizi wa fedha katika katika Shirika la Huduma ya Kitaifa kwa Vijana mnamo 2015 wakati Bi Waiguru alihudumu kama Waziri wa Ugatuzi.
Bw Odinga aliishangaza nchi nzima, alipofichua kwamba karibu Sh800 milioni hazikujulikana zilivyotumika katika shirika hilo, licha ya Bi Waiguru kupinga madai ya Bw Odinga.
Shinikizo zilipomzidia, Bi Waiguru alijiuzulu kama waziri, akimlaumu Bw Odinga kwa masaibu yake.
Uadui wao ulikuwa mkubwa kiasi kwamba Bi Waiguru alimshtaki Bw Odinga mahakamani kwa madai ya kumharibia sifa.
Katika nyakati hizo zoye, Wakenya wengi walimwona na kumchukulia Bw Odinga kama mkombozi wao kutokana na ufichuzi aliofanya.
Kundi jingine la Wakenya lilimwona Bi Waiguru kama hasimu mkubwa wa nchi, ambaye aliyepaswa kushtakiwa na kufungwa gerezani kwa tuhuma za uporaji.
Cha kushangaza ni kwamba, Bi Waiguru aligeuza masaibu yaliyomkabili, akijitetea dhidi ya ‘maonevu’ na ‘usaliti’ wa Upinzani kutokana na ‘mafanikio makubwa’ aliyokuwa amepata katika wizara yake.
Na alipotangaza kwamba angewania ugavana katika Kaunti ya Kirinyaga, wenyeji walimchukulia kuwa “mwana mpotevu” aliyeingiliwa kutokana na uchapakazi wake.
Walimchagua kwa kiwango kikubwa cha kura ili “kumwaibisha adui wao”, yaani Bw Odinga. Kwa kweli, walifaulu “kumwaibisha” Bw Odinga kwa kumchagua Bi Waiguru kama kiongozi wao.
Zaidi ya hayo, Bi Waiguru alichaguliwa na magavana wenzake kuwa naibu mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG).
Hivyo, kuungana tena kwa Bw Odinga na Bi Waiguru katika kampeni ya Bw Okoth kunazua taswira ya wazi kwamba wanasiasa ni viumbe wadanganyifu ambao hufaulu kuendeleza malengo yao kwa kuwazuga na kuwapumbaza wananchi.
Walipoungana, Bi Waiguru aliirai jamii ya Agikuyu inayoishi katika eneo hilo kumpigia kura Bw Okoth kama ishara ya kuunga mkono mwafaka wa Rais Kenyatta na Bw Odinga.
Hata hivyo, hawakumuuliza zilikoenda Sh800 milioni zilizodaiwa kupotea katika NYS chini ya usimamizi wake, wala vile watafaidika kwa kumchagua Bw Okoth.
Hili pia linamsawiri Bw Odinga kama mtu mnafiki, ambaye huwa anajivika kofia la “uanamapinduzi” ilhali ni kama ndumakuwili anayelenga kujifaidi.
Funzo kuu hapa ni kuwa Wakenya wenyewe ndio watakaojikomboa kutoka utumwa wa kisiasa, ila si wanasiasa. Wao ni kama daraja kuu la kuwawezesha wanasiasa hao kujifaidi wenyewe.