• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
WANDERI: Yawezekana tunaishi nyakati za mwisho?

WANDERI: Yawezekana tunaishi nyakati za mwisho?

Na WANDERI KAMAU

KUNA uwezekano tunaishi katika nyakati za mwisho wa dunia? Ndilo swali kuu ambalo linaibuka wakati huu ambapo dunia inakumbwa na msururu wa migogoro isiyoeleweka.

Kulingana na vitabu vitakatifu, baadhi ya dalili ambazo zitaashiria ujio wa nyakati hizo ni vita baina ya nchi, maradhi yasiyo tiba, chuki kati ya ndugu, majanga kama njaa, mitetemeko ya ardhi kati ya mengine.

Kando na janga la virusi vya corona, ambalo limeitikisa dunia nzima, majanga mengine ambayo yameendelea kuzua maswali mengi kuhusu chimbuko lake ni nzige hatari ambao wamevamia maeneo mbalimbali nchini, maradhi mabaya kama saratani na uvamizi wa konokono ambao uliripotiwa katika Kaunti ya Kirinyaga majuzi.

Kama nzige, konokono hao wameripotiwa kuvamia mashamba ya mpunga na kusababisha uharibifu mkubwa wa mazao.

Tangu mwaka uliopita, ugonjwa wa saratani umeua mamia ya watu bila kujali hulka wala tabaka yao.

Baadhi ya viongozi waliotuacha ni aliyekuwa Mbunge wa Kibra, Bw Ken Okoth, aliyekuwa gavana wa Bomet Dkt Joyce Laboso, aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya Safaricom, Bw Bob Collymore kati ya Wakenya wengine.Sawa na saratani, Corona haibagui.

Inawaua wanaume kwa wanawake, vijana kwa wazee, matajiri kwa maskini na weupe kwa weusi. Kinaya ni kwamba, walioathirika zaidi ni mataifa ya bara Ulaya, ambapo mengi husifiwa kuwa na uwezo mkubwa zaidi ya kiuchumi.

Baada ya ‘kuondoka’ China, virusi hivyo vilielekea katika nchi kama Italia, Uhispania, Uingereza, Amerika huku Kenya pia ikiwa mwathiriwa mkuu.

Baadhi ya watu maarufu ambao tayari wamethibitishwa kuambukizwa ni Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson, Mwanamfalme Charles (Uingereza), mwanamuziki Arlus Mabele, kutoka DR Congo ambaye alifariki kati ya wengine.

Ingawa chimbuko hilo limehusishwa na kila nadharia, kilicho wazi ni kwamba, funzo kuu lililopo ni kuwa kuna nyakati ambazo hufika ambapo Mungu hudhihirisha kuwa ndiye anayeishikilia dunia na vilivyomo ndani yake.

Kimsingi, janga hili lingekuwa limepata tiba au dawa za kupunguza makali yake kufikia sasa. Hata hivyo, limesalia fumbo kuu kwa nchi zote duniani.

Kuna baadhi ya wananadharia wanaosema virusi hivyo ni “vita baridi” vya Uchina dhidi ya Amerika kwenye ushindani wa kudhibiti mwelekeo wa kisiasa na kiuchumi duniani.

Swali ni: Kuna furaha ipi kwa taifa lolote lile kutumia maafa ya maelfu ya watu kudhihirisha “ubabe” wake wa kiteknolojia, kijeshi, kiuchumi ama kisiasa?

Kulingana na historia, majanga yote makubwa ambayo yameikumba dunia yalipata suluhisho la kupitia ushirikiano kati ya nchi mbalimbali zilizoathiriwa nao.

Kwa mfano, Vita Vikuu vya Pili vya Dunia (1939-1945) viliisha baada ya mataifa yaliyozozana kutia saini mikataba kadhaa ya amani.

Vivyo hivyo, lazima nchi kama Uchina na Amerika zishirikiane ili kulikabili janga hili. La sivyo, lawama na ushindani usiofaa ni sawa na kulipisha kuenea zaidi.

[email protected]

You can share this post!

ODONGO: Tusisahau nzige, mafuriko tunapokabiliana na virusi

Sonko hatimaye alisha Meja Jenerali pilipili ya siasa za...

adminleo