• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
WANGARI: Kupanda miti ya kiasili kutasaidia kuhifadhi vyanzo vya maji

WANGARI: Kupanda miti ya kiasili kutasaidia kuhifadhi vyanzo vya maji

Na MARY WANGARI

AKIZUNGUMZA majuzi katika sherehe za kuadhimisha Sikukuu ya Maeneo ya Maji Ulimwenguni, Waziri wa Mazingira, Bw Keriako Tobiko aliamrisha Huduma ya Misitu Nchini (KFS) kuondoa miti ya kisasa na badala yake kupanda miti zaidi ya kiasili.

Waziri huyo alikuwa akirejelea misitu kama vile yenye mikalatusi ambayo imesababisha kukauka kwa eneo mojawapo lenye chemchemi katika Kaunti ya Nakuru.

Kwa hakika kauli ya waziri hiyo ni ya busara na inapaswa kuungwa mkono na wadau wote husika hasa kwa kuzingatia jinsi baadhi ya miti hiyo inavyochangia kiangazi nchini kwa kufyonza kiasi kikubwa kupindukia cha maji kutoka ardhini.

Kwa mfano, mikalatusi ni miti inayotumia kiasi kikubwa zaidi cha maji huku ikiwa na uwezo wa kufyonza hadi lita 20 za maji kutoka ardhini wakati wa kiangazi na hadi lita tisini wakati ambapo hali ya anga ni yenye unyevunyevu.

Hii inaamaanisha kwamba msitu wa miti 1,000 ya mikalatusi unaweza kusababisha hata mto kukauka, hali ambayo inaashiria wazi hatari inayosababishwa na baadhi ya miti.

Isitoshe, mbali na kusababisha uhaba wa maji nchini kwa kuathiri viwango vya maji ardhini, baadhi ya miti ya kisasa kama vile mikalatusi hutoa aina fulani ya kemikali kwenye udongo, hivyo kuharibu mimea mingine.

KFS ni sharti ijitahidi kupanda miti asilia yenye ukakamavu na uwezo wa kukabili mawimbi na dhoruba kali kandokando mwa mito na maziwa ili kuzuia mmomonyoko wa udongo unaoshuhudiwa hasa wakati wa mafuriko kutokana na mvua kubwa.

Miti ya kiasili kama vile michikichi inachangia mno katika kuhifadhi mazingira kwa sababu mbali na kwamba haifyonzi kiasi kikubwa cha maji kutoka ardhini, miti hiyo pia husaidia kuimarisha kingo za mito na kudhibiti mtiririko wa maji.

Hatua ya kuondoa miti inayoathiri mazingira na kupanda miti zaidi ya kiasili katika nafasi hizo, inaambatana na kifungu cha sheria kuhusu Usimamizi na Mipangilio ya Mazingira 1999 katika Katiba.

Ili kuhifadhi chemchemi za maji, ni muhimu pia kuondoa majengo ya muda mfupi na ya kudumu yanayojengwa karibu na chemchemi za maji, ikiwemo kubuniwa kwa sera madhubuti zinazowezesha kuadhibiwa vikali kwa viwanda vinavyotupa uchafu kwenye mito.

Juhudi za kuhifadhi mazingira kwa kulinda chemchemi za maji nchini zinahitaji ushirikiano wa pamoja baina ya wananchi na serikali katika viwango vya kaunti na serikali ya kitaifa.

Hatimaye, kulinda chemchemi za maji nchini kwa kuhifadhi mito vilevile kutachangia pakubwa katika kufanikisha Ajenda Kuu Nne za maendeleo za Rais Uhuru Kenyatta pamoja na kuhakikisha kwamba hakuna uhaba wa chakula nchini.

You can share this post!

Valentino yasisimua wengi kwa njia tofauti

MUTUA: Bashir atapigwa mnada duniani apende asipende

adminleo