Wanjigi sasa atwaa usukani wa Safina, aahidi ukombozi wa kiuchumi
Mfanyabiashara aliyegeuka mwanasiasa, Jimi Wanjigi, amechukua rasmi uongozi wa chama cha Safina, akiahidi kukifufua na kukifanya kuwa jukwaa la ukombozi wa kiuchumi na kisiasa nchini.
Wanjigi alichukua usukani kutoka kwa mwanzilishi wa chama hicho, wakili Paul Muite, katika Mkutano Mkuu wa Kitaifa (NDC) uliofanyika jijini Nairobi. Akizungumza akiwa ameandamana na wakili Willis Otieno, ambaye sasa ni naibu kiongozi wa chama, Wanjigi alitangaza ajenda ya mageuzi aitayo FIST Agenda, inayolenga kupigania ustawi wa familia, uchumi wa mwananchi, na mustakabali wa taifa.
“Nchi iko kwenye mgogoro mkubwa. Watoto wetu wamefungwa katika madeni, familia haziwezi kumudu maisha, na haki za wananchi zinakiukwa,” alisema. “Kenya iko tena utumwani – ila safari hii, mkoloni ni wa ndani.”
Wanjigi alisema chama cha Safina kitaongoza mapambano dhidi ya ufisadi, ukosefu wa ajira, na mzigo mkubwa wa ushuru. Pia aliahidi elimu na afya bila malipo, kupunguza ukubwa wa serikali, na kuwezesha wafanyabiashara wadogo kupata mikopo kwa urahisi.
Safina, kilichoanzishwa Mei 13, 1995 na Muite na wanaharakati wenzake waliokuwa wakipinga utawala wa Moi, kilikuwa sauti ya mageuzi, kikipigania haki, usawa, na demokrasia ya kweli. Kwa miaka mingi, chama kilikumbwa na dhuluma za kisiasa, kusumbuliwa na kucheleweshwa kusajiliwa, lakini kilihusishwa na mafanikio ya mageuzi yaliyozaa Katiba ya 2010.
Katika hotuba yake ya kuaga, Muite alisema: “Tulianzisha Safina kwa imani kwamba kila Mkenya ana haki ya maisha bora, elimu, huduma za afya, na uhuru. Ni wajibu wa kizazi hiki kipya kuendeleza mapambano haya.”
Chama pia kilitangaza orodha mpya ya viongozi wakiwemo Patrick Birya (mwenyekiti), Nelson Osiemo (mkurugenzi wa uchaguzi), Joakim Simiyu (naibu katibu mkuu), na Diana Belta (mwenyekiti wa Baraza la Usawa). Uongozi huo mpya unaashiria juhudi za chama kupanua msingi wake na kuvutia vijana.
Wanjigi, ambaye awali alifadhili miungano ya kisiasa nyuma ya pazia, alijitokeza hadharani 2021 alipojaribu kumenyana na Raila Odinga katika kuwania tiketi ya urais kupitia ODM. Ingawa hakufaulu, alijenga taswira mpya kisiasa.
Wachambuzi wanasema hatua yake ya kuongoza Safina inaonyesha mwelekeo mpya wa wanasiasa chipukizi kutumia vyama vidogo kama majukwaa mbadala. Hata hivyo, changamoto kwake ni kugeuza Safina kuwa chama chenye ushawishi kitaifa, kwani kwa sasa hakina wabunge, maseneta, wala magavana.
Wanjigi amekuwa akilenga kizazi cha Gen Z ambacho kiliongoza maandamano ya kupinga ushuru mwaka 2024 na 2025, akiwaita “Mau Mau wapya wa kiuchumi.”
“Serikali hii imeua vijana wetu kama vile wakoloni walivyoua wapigania uhuru,” alisema. “Lakini sasa macho yetu yamefunguka.”