Washindi wa Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell watajwa
Na CHRIS ADUNGO
Kwa ufupi:
- Dotto Rangimoto kutoka Tanzania aliibuka mshindi wa kwanza na kutia mfukoni Ksh500,000 katika Kitengo cha Ushairi
- Kazi hizo zilikuwa miongoni mwa miswada 30 iliyosomwa na waamuzi watatu ambao ni Profesa Ken Walibora, Daulat Abdalla Said na Ali Attas
- Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Kiafrika hutolewa kila mwaka kwa miswada bora
- Miswada inayoshinda huchapishwa na East African Educational Publishers (EAEP) na Mkuki na Nyota Publishers
WASHINDI wa Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Afrika walitangazwa rasmi na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Abdilatif Abdalla mnamo Januari 15, 2018.
Madhumuni makuu ya tuzo hiyo iliyoanzishwa mnamo 2014 na Dkt Lizzy Attree (Mkurugenzi wa Tuzo ya Caine) na Dkt Mukoma wa Ngugi (Chuo Kikuu cha Cornell, Marekani) ni kuthamini uandishi kwa lugha za Kiafrika, kuhimiza sanaa ya tafsiri baina ya lugha za Kiafrika zenyewe kwa zenyewe na pia kutafsiri maandishi ya lugha nyingine kwa lugha za Kiafrika.
Dotto Rangimoto kutoka Morogoro, Tanzania aliibuka mshindi wa kwanza na kujipa uhakika wa kutia mfukoni Dola 5,000 (kima cha Ksh500,000) katika Kitengo cha Ushairi kutokana na kazi yake, Mwanangu Rudi Nyumbani.
Rangimoto almaarufu ‘Jini Kinyonga’ aliwapiku Mbaruk Ally (Tanzania) na Richard Atuti Nyabuya (Kenya) waliowasilisha miswada ya diwani Hali Halisi na Umalenga wa Nyanda za Juu mtawalia.
Ally Hilal Ali kutoka Tanzania pia alitia kapuni Dola 5,000 baada ya kuibuka mshindi wa Kitengo cha Riwaya kutokana na kazi yake Mmeza Fupa.
Wengine waliokamilisha orodha fupi ya waandishi waliokuwa wakiwania tuzo hiyo ni Hassan Omar Mambosasa (Tanzania) na Profesa Mwenda Mbatiah (Kenya) waliowasilisha miswada Nsungi na Kibweta cha Almasi mtawalia kwa minajili ya Kitengo cha Riwaya. Prof Mbatiah kwa sasa ni Mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Nairobi.
Miswada
Kazi hizo zilikuwa miongoni mwa miswada 30 iliyosomwa na waamuzi watatu ambao ni Profesa Ken Walibora (Mwenyekiti wa Majaji) ambaye ni mwanataaluma na mwandishi; Daulat Abdalla Said ambaye pia ni mwanataaluma na mwandishi anayesomesha Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar; na Ali Attas ambaye ni mwandishi na mwalimu wa Kiswahili na Kiingereza katika Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje, Japan.
Zawadi za tuzo hiyo mwaka huu zitatolewa mnamo Februari 13, 2018 jijini Nairobi, Kenya.
Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Kiafrika, yenye thamani ya jumla ya Dola za Marekani 15,000, hutolewa kila mwaka kwa miswada bora, au kwa vitabu vilivyochapishwa miaka miwili kabla ya mwaka wa kutolewa zawadi, katika fani za riwaya, ushairi, wasifu na riwaya za picha.
Kuchapishwa
Miswada inayoshinda huchapishwa na mashirika ya uchapishaji vitabu ya East African Educational Publishers (EAEP) na Mkuki na Nyota Publishers.
Na mswada bora wa ushairi hufasiriwa kwa Kiingereza na kuchapishwa kitabu na shirika la Africa Poetry Book Fund.
Tuzo hii inadhaminiwa na kampuni ya Mabati Rolling Mills (MRM), Kenya, na kampuni ya ALAF Limited, Tanzania (ambazo ni miongoni mwa kampuni za Safal Mauritius Limited); pia na Ofisi ya Makamu wa Mkuu wa Masuala ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Cornell, na Idara ya Taaluma za Afrika ya Chuo Kikuu cha Cornell, Marekani.
Kampuni ya Safal Investments Mauritius Limited na matawi yake (ambayo ni pamoja na Mabati Rolling Mills Limited, Kenya, na ALAF Limited, Tanzania) inajulikana kwa jina la jumla la The Safal Group.
Hii ni kampuni kubwa kabisa inayotengeneza mabati katika nchi 12 za Afrika (www.safalgroup.com). Wakizingatia historia ndefu ya uandishi katika lugha ya Kiswahili, majaji walieleza:
Mwanangu rudi nyumbani:
Mashairi yaliyomo katika diwani hii yametumiliwa lugha iliyojaa taswira na majazanda yanayowakilisha vyema hisia zinazoelezwa katika dhamira mbalimbali.
Mshairi amefaulu sana kuzitumia mbinu na miundo kadha wa kadha ili kuyajadili masuala yanayohusu hali na mazingira tafauti tafauti katika maisha ya binadamu.
Anayazungumza maswala mazito mazito, lakini kwa namna ambayo hayamuelemei msomaji wake.
Bali, badala yake, huwa yanamhimiza aendelee kuyasoma. Hata yale masuala makongwe, kwa mfano uhusiano baina ya wazazi na wana wao, yanajadiliwa kwa namna ya kuvutia na kuyafanya kama kwamba ndiyo mwanzo yanaanza kujadiliwa sasa.
Mshairi huyu ni mtunzi stadi. Na diwani hii ni mchango mkubwa katika ushairi wa Kiswahili wa zama zetu hizi.
Mmeza fupa:
Si mno mtu kukutana na riwaya ya Kiswahili ambayo mwandishi wake amejidhihirisha kuwa ni mbuji wa lugha fasaha na ya kisanii, inayotiririka kitabia kwa hiari yake, na bila ya kuonesha dalili zozote kwamba imelazimishwa.
Wahusika wake wote wamebuniwa kwa ustadi, na kupewa kazi mwafaka za kuziwakilisha tanzu na matabaka mbalimbali ya jamii – pamoja na mikinzano na mazingira yao ya kihistoria, ya kisiasa, ya kisaikolojia, ya kitamaduni, ya kimjini au ya kijijini.
Licha ya kwamba matukio ya riwaya hii yanatokea katika kisiwa cha kubuni, masuala yanayojadiliwa humu ni miongoni mwa yale masuala sugu yanayoendelea kulisumbua bara la Afrika kisiasa, kijamii na kiuchumi.
Riwaya hii inatudhihirishia mandhari mapya ya utanzu huu wa Fasihi ya Kiswahili.
Baruapepe:
[email protected]