WASIA: Angazia masuala mapya ya kiakademia sasa ili kiherehere cha mtihani kikuambae
Na HENRY MOKUA
SIJUI lini mwisho umesafiri kwenda usipokujua.
Kwa kutotaka kubahatisha upotee, ikakubidi kutafuta maelekezo kutoka kwa mtu uliyeamini kwamba angekuelekeza vilivyo ili ufike bila tashwishi.
Natumai wakumbuka ilivyokulazimu kuulizauliza iwapo hapo aliposimamisha gari dereva kila alipolisimamisha ili abiria washuke ndipo ulipopaswa kushuka pia.
Wakati mwingine hata ulijiona au kuonekana mjinga kwa kuuliza maswali mepesi mno ambayo sasa ukiyaangalia waona kweli hayachukuani na hadhi yako. Kisa na maana? Kutojua!
Na je, umewahi kuelekezwa kupika chakula usichojua kukipika?
Yamkini vilevile uliuliza kabla na baada ya kila hatua ukumbushwe hatua inayofuatia usije ukakosea.
Kwa jumla, mambo mageni huibua wasiwasi fulani hata kuwashinda wengine kabisa kuyakabili.
Katika masuala ya kiakademia, hali hii huwa na uzito hata zaidi.
Upo wakati ambapo kwa sababu hii au ile unakuta kwamba hujakamilisha au kukamilishiwa matakwa ya silabasi ipasavyo, tena kwa wakati.
Sababu yaweza kuwa kuugua kwako wakati faslu fulani ikifunzwa, mwalimu wako kuugua kwa kipindi fulani au kuhamishwa na mwingine kukawia kutumwa mahali pake; almuradi unakawia kushughulikia sehemu fulani ya silabasi kwa sababu moja ama nyingine.
Unapogundua kwamba una mapengo fulani katika maandalizi yako kwa mtihani, hasa kutokamilisha silabasi, ujue kwamba wakati mwafaka zaidi wa kushughulikia hali hiyo ndio huu.
Awamu ya pili ya muhula wa pili ni kipindi muhimu katika maisha hasa yako mtahiniwa.
Huu ndio wakati unapopaswa kujikadiria mwenyewe ukaona yale ambayo ameyashughulikia na yaliyosalia.
Unapogundua mawili matatu ambayo hayajashughulikiwa bado, unaweka mikakati ya kuyakabili. Mbona bado kuna muhula wa tatu?
Hili ndilo swali ambalo wanafunzi wengi hujiuliza kisha wakajidekeza.
Namna njia ngeni au upishi wa chakula kigeni unavyohangaisha ndivyo kujifunza mambo mapya ya kiakademia kunavyotatiza hasa ambapo pana shinikizo za kila nui. Kwa hivyo?
Chukua hatua ya kuorodhesha faslu zote ulizofunzwa na kujifunza hadi sasa.
Hii itakupa picha kamili ya kazi uliyosaza na unayopaswa kuipangia kabla ya muhula huu kukamilika. Ukishajua, sema na, la, mshawishi mwalimu wako akuelekeze katika faslu husika nje ya darasa.
Huenda atakuwa anaendelea kuifunza darasani; ikifanyika hivyo, mwombe mwanzie nyuma kule anakopanga kumalizia kisha mrejee kinyumenyume wakati akiendelea na kazi ya darasani.
Kujiamini
Huenda asitumie muda mwingi kama autumiao darasani lakini waweza kuwa na hakika kwamba atakuondolea wasiwasi kuhusu faslu hiyo (hizo).
Kwa kufanya mazoezi, utaibukia kujiamini katika maswala haya yaliyokuwa yamesalia sawa na uliyoyashughulikia awali.
Majuzi nimekutana na mwanafunzi ambaye alinitajia kwamba yeye hanuii kujibu swali la Diwani ya Hadithi Fupi ‘Tumbo Lisiloshiba na Hadithi Nyingine’ katika mtihani wake wa kitaifa mwaka 2019.
Miongoni mwa sababu za uamuzi wake ni kwamba kwanza hakipendi na pili, hajajiandaa kwacho; lakini najua hata wewe waweza kuamua kwamba sababu hapa ni moja; kutojiandaa.
Unatarajia kwamba nilimshauri atumie muda uliosalia muhula huu kujiandaa kwani unatosha, na hujakosea kwani hivyo ndivyo nilifanya.
Najua atakuja kunishukuru siku moja; lakini hata asipokuja sitakuwa nimetenda wema na kuenda zangu? Hivyo ndivyo nafikiri.
Ijapo wakati mwingine waweza kujiondolea lawama kwamba haikuwa hiari yako kutokamilisha silabasi, hutakuwa na fursa ya kumweleza kila mwajiri wako mtarajiwa habari hiyo. Kwa hivyo pana busara katika kupanga kuangazia masuala yaliyosalia japo kwa juu juu ili ujihakikishie ujasiri kuyahusu.
Kuyapuuza kisha ukakumbana nayo katika siku ya kwanza ya mtihani kutakutamausha.
Isitoshe, jitihada zako wakati huo kwamba ujifunze masuala hayo mapya japo kidogo zitakupotezea muda.
Tenga muda baina ya sasa na likizo ya Agosti uyashughulikie yote yaliyosazwa hadi sasa, iwapo hutayamaliza, jaribu kiasi cha kuridhisha na utayafurahia matokeo ya hatua yako hii.