Makala

WASIA: Jinsi ya kuukabili woga wa kushauriana na mwalimu wa somo

July 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na HENRY MOKUA

MWANA wako amewahi kukuuliza swali likakuzungusha akili usijue la kujibu?

Mdogo wako je?

Unajua watoto wakati mwingine huwa na imani ya kupindukia kuhusu uwezo wa wazazi wao.

Hutaraji, la, hujua kwamba wazazi wao wanajua kila kitu. Naam! Kila kitu!

Huja siku lakini mwanao akakuuliza swali, si la kukujaribu bali la kutaka kujua kweli, ukakosa usemi. Nilikuwa katika hali karibu sawa na hiyo wikendi iliyopita.

Baada ya kusema na kundi fulani la wanafunzi na kuwahimiza watie shime masomoni, awamu ya maswali iliwadia. Nikafanya kosa ambalo kila mwalimu bora hulifanya baada ya kipindi, lipi lakini? ‘Kufikia hapa upo radhi kuuliza swali lolote kuhusiana na mada hii…’ nikadakiza na kutarajia yale maswali ya kawaida, nayo hayakukosa. Kisha nikachukua kjikaratasi kingine na kukisoma: Je, nikiwa na tamaa ya kupita mtihani lakini nikalemewa na somo fulani halafu nikakosa ujasiri kabisa wa kushauriana na mwalimu wa somo hilo, nifanyeje? Nilimjibu nilivyomjibu lakini likanipa mshawasha wa kuliwazia zaidi.

Ingekuwa zamani kidogo, ningelijibu swali hilo kwa wepesi sana, labda kwa kauli moja mbili hivi: ushikwapo shikamana, naye mwenye haja huenda choo, na yangeishia hapo. Sivyo ilivyo sasa.

Nimekuja kugundua kwamba woga ni tukio la kihalisia zaidi kuliko tunavyofikiri.

Kutegemea mazingira alimozaliwa mwana, alimokulia, watu aliotangamana nao tangu utotoni, mazingira ya shuleni anamosomea na mambo mengineyo, anaweza kukosa kujiamini kabisa kiasi cha kuwaachia wengine wamwendeshee maisha yake.

Kuna wakati mtoto ni sawa na fahali aliyevunjika mguu na apaswa kurejeshwa zizini – nyumbani.

Ikikosa kufanyika hivyo, aweza kuwa raslimali ya woga, ukamtumia utakavyo. Kwako mwanafunzi uliye katika hali hii ya kuogopa kushauriana na mwalimu wa somo fulani akuandae vilivyo, ulifahamu fika na kukabiliana na mitihani vilivyo, jaribu mikakati ifuatayo.

Wazia unapotaka kuenda, mustakabali wako yaani. Ungependa kuishi maisha ya aina gani? Ikiwa kuna mtu katika ujirani wako unayemhusudu kwa namna alivyofanikiwa jiulize, hivi napaswa kufanya nini ili maisha yangu ya halafu yawe ya kuridhisha, ikiwezekana, yawe kama ya jirani yangu huyu? Ukisha, wazia gharama ya kukufikisha hapo: Je napaswa kupata alama gani ili kujiunga na taaluma hii? Nahitaji kuzoa alama gani katika kila somo, jumla, ili nijiunge na kozi hii? Msukumo utakaoupata waweza kukupa ujasiri akali kuanza kushauriana na mwalimu ili kwa pamoja mwondoe vizingiti vya kukuzuia usitimize ndoto zako. Matamu ya kufanikiwa na kusomea kozi ya ndoto zako hayatakuruhusu kuzidi kujidekeza.

Zingatia mibadala; je kuna mbinu nyingine naweza kuitumia ikanifanikisha kando na mashauriano? Ukiipata – ingawa mwenyewe sina hakika ipo, ijaribu!

Ukigundua kushauriana kutakufaa zaidi, jaribu kufanya mazoezi toka sehemu unayoielewa, japo ndogo kisha uulize maswali kuihusu. Kwa hivi, hutaonekana mbumbumbu unavyohofia; utaweza kumdhihirishia wa kushauriana naye kwamba yapo machache unayoyafahamu.

Halafu, anza kushauriana na mwanafunzi mwenzio, rafikiyo ambaye ni mjuzi wa somo utakalo kushauriana kwalo. Kabla ya shughuli, mweleze nia yako kinagaubaga, udhaifu wako wa kuogopa kushauriana na mwalimu na umshawishi awe akiandamana nawe kuenda kwa mwalimu mpaka uzoee.

Hatua nyingine ni ya kujiunga na kundi la mijadala kuhusu somo ulipendalo. Kwa nini mwalimu?

Kwa kuwafaa wenzio katika somo unalojiamini kwalo unakuza ukakamavu wako; waweza kujiambia: ama kweli, nakifahamu na kukipenda Kiingereza ingawa Kiswahili kinanitatiza!

Kwa hivyo? Unao msingi wa kujieleza kwamba angalau somo fulani nalielewa kwa kiasi cha haja, nikililielewa hili pia, nitabakiza hatua chache tu kuufikia ufanisi.

Mwisho, mweleze mwalimu wa somo ulipendalo aseme na mwenziwe wa somo linalokutatiza. Waweza pia kumwomba mzazi aseme na mwalimu wa somo aanzishe harakati ya mashauriano nawe.

Kwa vyovyote vile, tafuta mbinu uanzishe mashauriano na mwalimu na udumu kufanya vile…hata miungu haitaweza kukuzuia kutwaa ufanisi ambao utalazimika kujisalimisha kwako. Kila la heri.