Makala

WASIA: Kuaminiana kwa washikadau ni msingi muhimu wa kufikia ufanisi masomoni

April 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na HENRY MOKUA

ISMAIL ni miongoni mwa watu wanaoamiwa kuhakikisha nidhamu; si kwa wanawe tu bali pia wanaomzunguka. Mbinu za kuadhibu, kunasihi na kuadilisha anazo.

Zaidi, husikiwa mara moja kila anapotoa kauli hivi kwamba hajawahi kutarajia mwanawe kubishana naye kuhusu jambo la kumnufaisha mwana huyo moja kwa moja.

Majuzi lakini amenisimulia kisa ambapo mwanawe katika ngazi ya chekechea amekataa kabisa kumsikia licha ya viboko vya kumnyoosha vinavyoelekeza Vitabu Vitakatifu.

Mwanawe huyo alidai kwamba yu mgonjwa ijapo hakuonesha dalili za ugonjwa. Baada ya kichapo alichokisikitikia mwenyewe, mtoto alishikilia pale pale; haendi shuleni.

Katika harakati za Ismail kusaka majibu kuhusu kisa na maana ya hali ile, ndipo mtoto alipoonesha dalili za malaria. Kumbe wakati akikaidi agizo la baba yake la kwenda shuleni alikuwa ameanza kuhisi maumivu.

Baba mtu alijutia sana hasira zake mtoto alipogunduliwa kuwa na malaria.

Hivi wewe ni mwepesi kiasi gani katika kuamini kauli za mwanao? Je wewe mwana, wamwamini mzazi wako kiasi gani? Mwalimu na mwanafunzi je mwaaminiana?

Kuaminiana kunakowaziwa kuwa msingi wa ndoa tu huwa na umuhimu mkubwa katika takriban mahusiano yote.

Kunapokosekana, huwapo uwezekano wa kutoa hukumu isiyostahiki au kumvunja moyo anayetarajia kueleweka na kuaminiwa.

Ni wanafunzi wengi ninaokutana nao wakaniarifu kwamba wazazi wao hawakuwatendea mambo ya kimsingi
waliyotarajia.

Ninapodadisi lakini hugundua kwamba wanafunzi hao wamekosa tu kuwaamini wazazi wao ambao wamejitahidi kuwakimu.

Wapo wanafunzi wengine ambao hata wanapokosa mahitaji hayo ya kimsingi huridhishwa na jitihada za wazazi wao; kisa na maana, wanawaamini.

Likizo inapoanza, mawasiliano ni mengi yanayotarajiwa kufanyika. Kwanza ni ripoti watakazotoa walimu kuhusu matokeo ya wanafunzi wao. Ili kupiga hatua mbele, kuaminiana kutakuwa jambo muhimu.

Ukimwona mwanao kakuletea ripoti yenye matokeo bora usivyotarajia, usiwe mwepesi wa kuishuku na kumweleza ulivyotarajia afeli kwa namna unavyomfahamu kwa kawaida.

Utamvunja moyo asitake kujibidiisha tena – hata waweza kuwa kiini cha kufeli kwake hatimaye. Badala ya kumtajia mambo hasi uliyoyatarajia kwake, mpongeze kwanza kisha ukadadisi kuhusu hali ya mambo shuleni.

Huenda mwanao amebadili nia na kuzidisha bidii masomoni.

Kumshuku hali ametoa kijasho kupata matokeo bora kutamsababisha kuamini kwamba humtakii mema licha ya kumhangaikia sana.

Kumbuka mwanao hayupo peke shuleni; wapo wanafunzi wenye maono hali kadhalika walimu waliojitolea na kila uchao wanajishughulisha kuhakikisha ufanisi wa kila mmoja.

Huenda mwanao ni zao la juhudi hizi.

Kauli ya mwalimu si ya kuchukuliwa hivi hivi.

Anapotaja kwenye ripoti ya mwanao kwamba anahitaji kutilia mkazo masomo fulani, usiwe mwepesi wa kulaani walimu wa masomo hayo.

Anaposhtakia kwamba mwanao afaa kujiepusha na marafiki wapotovu, usijipe kulipuuzilia mbali wazo la mwalimu ukidai wamfahamu mwanao vyema – kwamba ni mwadilifu wa kupigiwa mfano.

Amini kauli ya mwalimu kwanza, kisha shauriana naye kuhusu hatua mwafaka ya kuchukua kuhakikisha kila mmoja wenu amefaidi.

Mzazi wako amekuwa mtoto kwanza, akawa kijana kisha mzazi. Mwalimu wako amekuwa mwanafunzi kwanza kisha akawa mwalimu, kwa hivyo hata ukawa mwerevu, huwapiku upande wa maarifa.

Wanapokuambia ujitenge na marafiki wako wa sasa na kupata wengine watakaokuhimiza kuwa mwadilifu na kufanikiwa masomoni, wazia kwa makini kauli zao.

Wanapokutajia kwamba mahusiano ya kiholela na vijana wa jinsia nyingine yatakudidimiza hatimaye, usipuuze kwa msingi kwamba wajua kupanga mikakati – yatie maanani yakuokoe.

Nawe mwalimu kuwa radhi kuambilika. Mzazi akishikilia kwamba mwanawe hana tatizo la kumdidimiza anapokuwa nyumbani, saidiana naye kudadisi tatizo ambalo huenda limemkumba shuleni na kumdidimiza.

Nihitimishe hivi: amini kila lenye mashiko, msingi wa kuaminiwa. Chunguza kwa hekima kila unalolishuku ili ubaini ukweli walo.

Muhimu zaidi, jiepushe kadri uwezavyo na kutomwamini anayestahiki kuaminiwa na kwa hatua yako hiyo kumvunja kwani hujui utamdhuru kiasi gani kwa kumshuku visivyo na iwapo atawahi kukuamini yeye.