• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
WASIA: Kumthamini mwalimu ndiyo msingi wa kumthamini mwanafunzi wake

WASIA: Kumthamini mwalimu ndiyo msingi wa kumthamini mwanafunzi wake

Na HENRY MOKUA

BAADA ya matokeo ya mtihani wa kitaifa wa Cheti cha Kuhitimu Kisomo cha Msingi (KCPE) kutangazwa wiki jana, mijadala mingi iliendelea kuyahusu, si katika mazungumzo ya ana kwa ana, si kwenye redio, si kwenye vituo vya televisheni, mitandao ya kijamii.

Katika mijadala yote hii, nilivutiwa na mmoja katika kundi sogozi (WhatsApp Group) fulani.

Ndugu mmoja alikumbuka hali inayomsubiri shuleni mwake baada ya shule kufunguliwa mapema mwaka kesho. Alishtakia jinsi anavyotarajia wanafunzi waliovuta mkia kusajiliwa shuleni mwake huku wenziwe wakipokea wale waliotia fora.

Huu ukawa tu msingi wa kueleza fundo chungu lililomkaa moyoni…lipi lakini – kwamba shule za kitaifa hupokea wanafunzi wenye alama 350 na zaidi kwa 500 na walimu wazo kuzidi kusifiwa huku wale waliopokea wanafunzi wenye alama 200 au chini yazo kwa 500 wakikashifiwa kwa kuzembea wanafunzi wao wanaposelelea kwenye mkia.

Ukidhani alikomea hapo unakosea – aliwahi kutoa mfano wa hali ilivyo katika utabibu – kwamba wagonjwa mahututi ndio hupelekwa kwenye hospitali zilizostawi kama vile Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta huku walio afadhali wakipelekwa kwenye vituo vya afya karibu na kwao…akapendekeza kwamba wanafunzi wenye alama zaidi ya wastani wasajiliwe katika shule za kaunti na walio na alama za chini ya wastani wasajiliwe katika shule za kitaifa zenye vifaa vya kuwafaa zaidi. Nakuachia ujiamulie iwapo wazo lake lina mashiko au la.

Kwa upande wangu, naona wakati umewadia kwetu kubadili mitazamo katika misingi ya kibinafsi, taasisi na kitaifa. Yatupasa kwanza kukubali kushawishika kwamba uwezo wa watoto wetu unatofautiana na hayo nakisia ndiyo mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Sijaona kizazi chochote hata vinavyoangaziwa katika vitabu vitakatifu kilichokuwa na watu wenye uwezo sawa.

Vitabu hivyo husimulia kwamba wengine walikuwa viongozi waliosimamia laki kadha za watu, wengine wakasimamia maelfu na wengine mamia.

Vitabu hivyo havisiti pia kutaja kwamba palikuwepo na watumishi wa viongozi wa ngazi mbalimbali. Hivi ndivyo kusemaje msimulizi? Wanafunzi, kama binadamu wengine wowote wana uwezo unaotofautiana na tutakosea kuwatathmini kwa msingi wa alama zao katika mitihani tu.

Changamoto kuu ya humu mwetu ambayo labda humfanya mwalimu kuchelea kumfundisha mwanafunzi aliye chini ya wastani ni kwamba mwalimu hathaminiwi.

Akithaminiwa, ni kwa saa kadhaa na shingo upande.

Kuangaliwa kama mkembe bila kupewa uhuru wa kujiamulia mambo, kutohusishwa katika mashauriano yanayohusu taaluma yake, kutishiwa kiholela na kutolipwa sawasawa na juhudi zake ni miongoni mwa mambo yanayomfisha moyo mwalimu wa enzi hii.

Humfanya kukata tamaa na kutomthamini mwanafunzi anayehitaji muda na makini zaidi kuelekezwa.

Katika nchi zinazomthamini mwalimu kwa yakini, mwalimu haoni ugumu wa kumwelekeza mwanafunzi kwa dhati, akiwa mwepesi au mzito.

Kwa hivyo? Wakati umewadia kwa serikali kumthamini mwalimu zaidi ili awe na hamasa ya kufanya kila lote kumfaa mwanafunzi wake wa kiwango chochote.

Kwa vyovyote vile, mwanafunzi asije akawa mwathiriwa wa jambo lisilomhusu.

Iwapo ana uwezo mdogo kiakademia, si kwa sababu ya uzembe bali kimaumbile, na umwelewe ewe mwalimu na kumpa mwongozo unaostahiki.

Wakati serikali ikijizoazoa kutimiza matakwa ya mwalimu vilivyo, yupo Mungu mbinguni asiyepitwa na kila juhudi ya mwanadamu itokanayo na nia njema.

Ukimpata mwanafunzi hafifu, mwelekeze kwa dhati ya moyo – aridhike kwamba umefanya kila uliloweza kumfaa – huu ndio msingi wa baraka kwa mwalimu.

Nawe mwanafunzi usije ukajiachia kwa kufikiri alama uliyoizoa ni ya chini mno – jiliwaze kwa mambo unayoweza kuyafanya vema. Ikiwa Yusufu tunayesoma kisa chake katika vitabu vitakatifu alianzia utwana akakwea taratibu hadi akawa Waziri Mkuu, nawe usiwe mwepesi wa kukata tamaa. Itumie kila fursa uipatayo vilivyo na hakika, juhudi zako zitazaa matunda.

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Wangu Kanuri

KINA CHA FIKIRA: Iweje wageni wanakifurahia Kiswahili huku...

adminleo