WASIA: Mashauriano ni muhimu kuwaadilisha vijana wanaobaleghe
Na HENRY MOKUA
WIKENDI iliyopita mzazi fulani alinisimulia kisa cha kuchekesha na kusikitisha kwa wakati mmoja – kuchekesha kwa namna mzazi mwenziwe alivyohadaiwa na watoto wake mwenyewe; na kusikitisha kwa sababu ya kuhofia hatima ya watoto wake hao waliomhadaa.
Baada ya baba ya watoto wa kisa na mkasa kuamua kuwaadhibu binti zake wawili kila mmoja wao anapokosea, ndugu hawa walifanya masikilizano kati yao kutokosea kabisa; kwa vipi lakini?
Kwa kufikia mwafaka yeyote kati yao asimfahamishe baba yao kwamba mwenziwe amekosea.
Kwa kipindi fulani, baba yao alijua kwamba binti zake wamekoma kukosea kwani hakuripotiwa kuhusu utovu wowote wa nidhamu wa mmoja wao.
Mama yao asingekuwa makini na kugundua njama yao hiyo, baba angesalia kuamini kwamba adhabu yake imewabadilisha.
Sawa na baba huyu, wengi wa wazazi tumehadaiwa na watoto wetu; labda kwa sababu ya mbinu mbovu za kuadhibu tunazozitumia, hasa kwa vijana ambao ndio kwanza wanabaleghe au kuvunja ungo.
Inakuwaje mzazi umwadhibu mwanao kwa kosa lisilo lake ilhali unajua hakika siye aliyelifanya?
Je, ni kutofafanukiwa kwamba enzi zimebadilika na hivyo mbinu au mitindo ya kuadilisha sharti ibadilike?
Ukweli ni kwamba sharti tuendelee kuwaadilisha na kuwaadhibu watoto wetu, lakini tutalifanyaje hili bila kujali matokeo yalo?
Katika kuadhibu, tunakuwa na nia ya kurudi au kurekebisha, pindi tukisahau kwamba hii ndiyo nia yetu, kuna uwezekano mkubwa wa kupoteza.
Mtoto anapofikia umri wa kubaleghe au kuvunja ungo, huwa ameingia katika ngazi nyingine ya maisha – si mtoto tena ingawa pia si mtu mzima.
Kwa msingi huu, anakuwa na kuchanganyikiwa kwingi ambako wewe wazazi wapaswa kuuelewa. Kwa kweli, anakuwa mtu wa kipekee ambaye huhitaji mbinu za kipekee za kuadilishwa na kuadhibiwa.
Maelekezi
Ijapo kuna mengi asiyoyaelewa, yeye hudhani tayari anayaelewa.
Mbinu mwafaka ya kumwaelekeza katika hali hii ni kumshirikisha katika kubuni baadhi ya kanuni za kuiongoza familia ili ifikie azma yayo.
Anapaswa kueleweshwa kwamba kwa kuamka mapema kusoma, anajitengezea mustakabali bora na kukosa kufanya hivyo ni kujipotezea nafasi muhimu maishani mwake.
Mkumbushe kwamba kwa kutoamka mapema na kujitahidi, ana hakika ya kudidimiza matokeo yake na hivyo kusababisha hasara kwako wewe mzazi au mwangalizi wake.
Kutokana na hitaji kubwa la uhuru wa kujiamulia mambo analokuwa nalo akibaleghe au kuvunja ungo, litakuwa jambo la busara kwako kupunguza masharti uliyoyabuni mwenyewe na kumshirikisha katika maamuzi kupitia kwa mashauriano.
Mama aliyenisimulia kisa nilichokwisha kukitaja alinieleza pia kwamba baba yao huwaelekeza kutojishughulisha na kingine chochote isipokuwa vitabu vyao.
Kwa hivyo, binti zake huwa mezani kusoma kila anapowataka kufanya vile baba yao.
Cha kusikitisha ni kwamba pindi tu anapoondoka, vitabu huwekwa pembeni hadi anapokisiwa kurejea au anapothibitika karejea kweli.
Katika mchezo huu wa paka na panya ambao mama watu hajaweza kuusitisha, kuna hakika ya kufeli kwa mabinti hawa.
Inambidi baba watu abadili nia, akubali kwamba bintize si watoto tena ijapo si watu wazima pia.
Ili kuwafaa mtoto wako katika umri huu, sharti uhiari kujishusha hadi alipo msemezane kwa upendo – ni kwa hivi ndipo atakutajia matazamio yake na changamoto zake.
Uhusiano wa karibu utakapojengeka mkabuni sheria za nyumbani pamoja kwa misingi inayoeleweka na kuthibitika, ndipo utaweza kuidhibiti hali.
Vinginevyo, utakuwa unaishi tu katika ulimwengu wa fantasia na matokeo yake wayajua.