WASIA: Namna ya kukabili kiherehere cha mtihani ili kuvuna alama nzuri
Na HENRY MOKUA
UMEWAHI kujiandaa kujieleza vilivyo katika kikao fulani kisha ukabaki ukijilaumu, ukijigombeza hasa kinapofikia hatima?
Pengine kwa kutopewa muda wa kutosha au kuzidiwa na woga, unakumbuka uliyonuia kuyataja kikaoni baada ya kikao chenyewe kufikia tamati?
Je, kwa mwanafunzi anayejiandaa kujieleza kikamilifu katika mtihani lakini akashindwa mara kwa mara? Ni majuto, utamaushi kiasi gani anaokuwa nao kushindwa kujieleza na kufeli mara kwa mara?
Hili ndilo swali nitakalojaribu kujibu leo; kwanza kwa kubaini vyanzo vya hali yenyewe, kisha kupendekeza suluhisho.
Si mara chache wanafunzi hunikabili na swali hili: nina nia ya kupita, nami hujitahidi, ila mitihani hunibwaga kila uchao, nifanyeje?
Kwanza chunguza na utathmini maandalizi yako. Je, unao utaratibu maalumu unaoufuata wakati wa kudurusu na kujiandaa kufanya mitihani?
Huwa unaandaa ratiba ya muda ya kudurusu kulingana na ratiba ya mtihani?
Ni jambo la busara kujifunza namna ya kudurusia kila somo. Mathalani, masomo tekelezi, kama yale ya sayansi, pia Hisabati, yaweza kudurusiwa mapema tu, kabla ya mitihani kuandaliwa.
Kwa namna gani? Masomo haya hujumuisha fomyula na hesabu kwa kiasi cha haja; waweza kutumia fomyula zenyewe katika mazoezi mpaka zikakolea akilini mwako.
Hii ni sawa na kusema, udurusu wa masomo haya haukomi, ni tukio la siku hadi siku na kadri unavyofanya mazoezi, ndivyo unavyozidi kujiamini hivi kwamba ukikabiliwa na maswali katika mtihani, unayaona kawaida sana.
Sisemi usiyapitie mitihani inapowadia, ila yashughulikie tena na tena kabla ya udurusu wa mwisho, saa kadhaa kabla ya mitihani yayo wala usiyasahau masomo mengine unayoyafanya, jiandae vilivyo kwayo pia.
Pili, kuwa na matazamio au shabaha zinazofikilika. Wakati mwingine tunajiwekea shabaha zinazokiuka uwezo wetu ajabu. Yaani wewe ukiwa na uwezo wa kupata alama C kwa wakati fulani, unajiwekea shabaha ya B+, au uwezo wa kupata alama 200, ukajiwekea shabaha ya alama 350.
Katika hali hii, utajikatiza tamaa bure.
Nisemavyo mara kwa mara, jadiliana na mwalimu wako au mwingine yeyote anayeweza kukuelekeza unapojiwekea shabaha.
Ijapo ni muhimu kujiamini, ni hatari kujiamini kupita kiasi.
Fuata maagizo kwa makini, yasome upya kama ambaye hujawahi kuyasoma awali. Nimeona wanafunzi si haba wenye uwezo wakifeli kwa kutofuata maagizo ya mtihani. Kutokana na pupa na kushangaa mtihani ulivyo rahisi, hushindwa kugundua mitego ya kimakusudi ya utahini na kuishia kufeli.
Kichungi
Mtihani ni kichungi na kusudi ni kuchuja wasioweza kufuata maagizo au kubaini mitego iliyomo.
Wakati mwingine maswali yamefungamanishwa, kwa mfano katika insha ukahitajika kuambatisha wasifukazi wako kwenye barua ya kutuma maombi ya kazi, wewe ukaandika ama barua au wasifukazi na kupuuza hiyo sehemu nyingine kwa sababu una haraka ili uwababaishe wenzio kwamba wewe ni makini zaidi…utapita kweli? Soma maagizo kwa makini, ikibidi yarudie.
Tulia kabla na wakati wa mtihani, iruhusu kumbukumbu yako kufanya kazi vilivyo.
Wanafunzi ni wengi pia ambao kwa kuona swali moja au mawili wasiyoyamudu, huanza kutetemeka ndani kwa ndani, wakati mwingine hata wakatambulika.
Utagundua kwamba kumbukumbu yako ya muda ndiyo imesahau lakini taratibu inaanza kupenyezewa vidokezi na kumbukumbu ya kudumu. Kwa hivyo, anza na maswali mepesi – marehemu mama yangu angenikumbusha hili kabla ya kila mtihani na sikuwahi kulijutia – nawe una nafasi ya kulibaini. Wakati ukiendelea na maswali mepesi, yale mengine hukumbukika taratibu.
Mwisho kabisa na nafikiri muhimu zaidi, shauriana na mmoja wa walimu wako kuhusu hali hii. Mweleze fika unavyojiandaa na unavyoandika mitihani yenyewe kisha matokeo yakakukatiza tamaa. Huenda akagundua udhaifu fulani mahususi kwako na kwisha zishughulikia, hutasita kukiri kwamba kushikamana ndiyo njia pekee ya kila ushikwapo pamoja na dua kwa Mwenyezi Mungu.