WASIA: Yakome mahusiano ya kiholela hata yawe na mikataba mizuri
Na HENRY MOKUA
MWISHONI mwa kikao kimoja nilichokuwa nacho na vijana likizoni, awamu ya maswali na majibu, binti mmoja – mwanafunzi – alishtakia kwamba yeye ni yatima na waangalizi wake hawawezi kumkimu kikamilifu.
Nilikuwa karibu kuanza kujibu alipotaja changamoto hasa.
Kumbe maelezo yale ya awali yalikuwa kitangulizi tu.
Vipi tena? Alipojiunga na kidato cha kwanza, matokeo yake yalikuwa afadhali, sasa yamedidimia mpaka yanampa wasiwasi mwenyewe, nao waangalizi wake ambao ni shangazi zake walaani kufeli huko kwake mara kwa mara.
Si hayo tu lakini. Binti ana marafiki wawili wa kiume ambao anawashawishi wamsaidie kukimu mahitaji yake yasiyokidhiwa na shangazi zake lakini kwa masikilizano kwamba wasimdhuru kwa kushiriki naye ngono hadi akamilishapo kisomo chake.
Unaanza wapi unapokabiliwa na kisa kama hiki?
Kwangu hakikuwa kisa kama hiki bali hiki hasa.
Hali iliniwia ngumu zaidi nilipogundua kwamba msichana yule hakunipa muda hata wa kujibu.
Kila nilipotaka kutoa kauli, alikumbuka jambo, akanikatiza na kulitia katika kisa chake ili lisije likasahaulika katika kujibiwa kwake.
Niligundua kwamba alihitaji kusikilizwa zaidi, na kweli, baada ya kujieleza kwa muda, aliyaachia machozi yaliyobeba fundo lile chungu yamtiririke hadi apone.
Nimekuja kubaini kwamba wapo wengi walio katika hali sawa na binti huyu wa kisa na mkasa.
Wakati mwingine unaposikiliza visa hivi, unaguswa kiasi kwamba maneno yale yale unayopaswa kutumia kujibu yanakupotea. Hata hivyo, binadamu ameumbwa na uwezo wa kutatua nyingi ya changamoto zinazomkabili.
Ikiwa wewe ni miongoni mwa wanafunzi wa kike au wa kiume wanaopitia changamoto sawa na hii, ni muhimu ufahamu kwamba ndiwe wastahili kuchukua hatua ya awali zaidi kujikomboa. Kwa kuchukua hatua ya kuweka wazi changamoto yake, mwanafunzi niliyemsimulia alionesha nia ya kujikwamua na kuanza maisha mapya.
Mahusiano
Hatua ya busara na ya awali kwako kuchukua ni kuwazia faida unayoweza kupata kutokana na mahusiano yako sawa na ya binti yule. Je, marafiki zako hao wakiyakimu mahitaji yako ya vitu unavyohitaji kutumia shuleni pamoja na masurufu, waweza kuyafikia malengo yako ya kiakademia?
Je, unapozingatia faida na hasara za mahusiano yako, waweza kukiri kwa ujasiri kwamba faida zitazidi hasara utakayoipata? Katika mahusiano ya namna hii, ukweli wa kimsingi ni kwamba pesa za masurufu na za matunzo utakazopata zitazua hasara zaidi kwako kuliko faida. Mbona hasara na nitakuwa sawa na wenzangu nisiweze kudhalilishwa?
Labda hata nitaweza kujiamini zaidi kwa kuwa sawa nao! Ewe uliye katika mahusiano ya namna hii, fahamu kwamba hayo unayoyaona faida, ndiko kupoteza hasa. Kila utakapokumbuka hisani au fadhila ya rafiki zako hao, fikra zako zitapaa ukaanza kufikiri kuwahusu na kuona walivyo afadhali kuliko watu wa ukoo wako au wanaostahiki kukukimu.
Katika harakati hii, utapoteza kimhemko, kisaikolojia, kiakili, kiroho na hata kijamii.
Nafsi yako itakuwa na vita nawe kila utakapojaribu kuishawishi ikubali kwamba hatua unazozichukua ni sahihi nayo ikishikilia ni hatari.
Mvutano huu utazifanya fikra zako kuvurugika kwa kuwa kila mara wakubwa zako watakuwa wanakukumbusha kwamba hujatimiza umri wa kuwa na uhusiano ya kimapenzi, nayo dhamiri yako italishikilia wazo hili.
Kuipotosha kutakuwa vigumu mno, wala usidhani ninazungumzia walio na mahusiano zaidi ya mmoja; huo mmoja una madhara sawa na zaidi ya mmoja.
Kuamua nani utakayemwambia changamoto yako; mkubwa wako atakayeweza kukusikiliza bila kukuhukumu kisha akuongoze taratibu kuondokana na hali yenyewe ndiyo hatua unayopaswa kuchukua.
Mweleze waziwazi ngazi uliyofikia uhusiano wenu wa kimapenzi ili akusaidie kuondokana nao.
Jambo moja litakalokufafanukia kando na hayo mengi niliyokwisha kuyataja ni kwamba, mikataba ya ‘nitakusaidia tu bila kushiriki ngono nawe’ si ya kudumu.
Wengi waliyoifanya watakuambia kwamba ilivunjika hata kabla ya kuanza kutekelezwa. Tokeo lake? Msongo, maradhi, mimba za mapema, hata kifo unapojaribu kuavya.
Ukifanya uamuzi wa kuelekeza mawazo yako yote masomoni mwako, utaanza kuimarika na hatua kwa hatua utafikilia matokeo yatakayovutia makini ya walimu. Wakigundua umeimarika, tayari utakuwa umeishawishi mioyo yao kupanga na usimamizi wa shule kukusaidia kuliko kutegemea misaada ghushi ambayo una bahati iwapo hujaanza kuilipia kwani hakika ni kwamba sharti uilipie hatimaye!