• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 5:29 PM
WASIA: Zingatia kigezo cha uadilifu unapoteua rafiki, vinginevyo utadamirishwa

WASIA: Zingatia kigezo cha uadilifu unapoteua rafiki, vinginevyo utadamirishwa

Na HENRY MOKUA

RIZIKI alikuwa mwanafunzi stadi sana tangu ajiunge na shule ya msingi.

Walimu wake wangemsifia bila kusita kwa makini yake na mikakati aliyobuni kudhibiti mawimbi ya ujana ili asalie kileleni katika masomo yake.

Ilikuwa kawaida kuwasikia walimu wake wakimpigia mfano mara kwa mara na kuwataka wanafunzi wenziwe wamwige.

Alipojiunga na kidato cha kwanza bado alisalia kileleni. Katika kidato cha pili lakini, mambo yalianza kubadilika.

Matokeo yake yalianza kudidimia; likawa suala la kumtanabahisha kila aliyekuwa karibu naye; si walimu, si wazazi na waangalizi wake, si wenzake waliokuwa na nia njema!

Yeye angedakiza tu: masomo machache yanayonitatiza nitayaacha hivi karibuni niendelee na yale niyapendayo!

Je mwanao au mwanafunzi wako anapokushawishi ukubali kwamba ataimarika pindi akiyaacha masomo yanayomtatiza, na miongoni mwayo ni Kiingereza, Kiswahili na Hisabati – masomo ya lazima – unafanyaje?

Ikiwa hujapata jibu la moja kwa moja kwa swali hili, changamoto yako si tofauti na ya walimu, wazazi na waangalizi wengi. Kisa na maana, mwanafunzi anafeli masomo ya lazima na anadai akiyaacha yanayomtatiza matokeo yake yataimarika, huoni anakuchanganya?

Kila mambo yanapofikia hapa, hatua ya busara kuchukua ni kuchunguza kiini hasa cha mwanao kuanza kuwa mbunifu kupita kiasi.

Chunguza anakula nini, anakunywa nini, anatembea na nani, wapi, na mambo mengine yanayochukuana na haya.

Katika haya yote lakini tambua kwamba uwezekano mkubwa wa mwana kuathirika hivi, ni marafiki wa karibu alio nao. Kama ilivyo katika masuala ya wongovu, pana hatari kubwa muumini anapojipa kumwokoa mpotevu kutokana na ushirika wa karibu.

Aghalabu, mwadilifu ndiye huasi uadilifu wake na kujiunga na mwenziwe mpotovu.

Ukweli mchungu hapa ni kwamba masafa toka kwenye uadilifu hadi upotovu ni mafupi ukilinganisha na yale ya upotovu hadi uadilifu na kila mwenye nia njema atakutajia hili kimachomacho! Kwa hivyo?

Ikiwa unajitakia mema ewe kijana, mwanafunzi, teua rafiki zako kwa makini.

Imethibitika kwamba mvuto wa marika (watu wenye umri sawa na wako) huwa na athari kubwa katika maamuzi mengi ayafanyayo kijana.

Bahati njema ni kwamba, marika hawa wapo wa sampuli mbili – waadilifu na watovu wa maadili.

Ni heri iliyoje ukijiunga na rafiki au marafiki waadilifu! Je ni rahisi kama kutamka tu? La! Ingekuwa rahisi hivyo, ni wachache mno wangepoteza dira…unakusudia nini?

Kuvutia rafiki mwema, sharti kwanza uwe rafiki mwema, na kuwa rafiki mwema ni gharama!

Habari njema ni kwamba wengi wamepitia njia hiyo awali kwa ufanifu, usiwe na wasiwasi.

Nifanyeje basi? Jinyime starehe, anasa kwa kipindi kifupi, ufurahie katika siku zako za halafu.

Unapokuwa kijana, unakuwa na hitaji kubwa la kujiamulia mambo hata kwa kumpuuza mzazi; ili uwe rafiki mwema, mtii mzazi na mwangalizi wako.

Ana tajriba pana ya maisha, na kama ilivyo katika biashara yoyote njema, mtu akiwekeza, hutarajia faida – je wewe wafikiri mzazi wako anaweza kuwekeza kwako halafu akupotoshe kwa nia ya kupata hasara, haiwezekani!

Izime mihemko ya ujanani kwa utawa, ucha Mungu.

Katika umri wako wa kubaleghe au kuvunja ungo, nia yako ni kuzungukwa na marafiki wa jinsia nyingine – hivi ndivyo unajihisi umekamilika!

Jifunze kujinyima mahusiano ya namna hii kadri iwezekanavyo; kwani kuna ubaya?

Katika siku za awali, mnajiambia: hapa ni kusoma tu! Mkikosa uangalizi wa mtu mzima mwenye maadili yake, uwezekano wa kugeuza huko kusoma tu kukawa na ziada ni mkubwa mno!

Katika mahusiano kwa jinsia nyingine yatakayobidi, hakikisha unakuwa na kiasi usije ukajiponza mwenyewe.

Somea palipo na wazee wenu au mahali wazi pasipoweza kuwa na ushawishi wa kugeukia ngono badala ya kusoma.

Tatizo la Riziki liliwahi kugunduliwa – kumbe alikuwa amejiunga na marafiki wapotovu akayapuuza masomo yake.

Aliponasihiwa, alibadili nia akajitahidi na kufuzu masomoni mwake!

Je wewe unafanya uamuzi gani leo? Utamkoma rafiki yako mpotovu na kujiunga na yule mwadilifu ama upo tayari kwa lolote!

Lau ungebadili nia leo ujiwekee ufanisi katika mustakabali wako! Ukikosa, usije ukanilaumu kwani nimeshatekeleza wajibu! Kila la heri!

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: John Muli

KINA CHA FIKIRA: Wakenya wamezoea kuhalalisha makosa ya...

adminleo