Makala

WASONGA: Tuwe macho virusi vipya visipenyeze hapa Kenya tena

July 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

MAJUZI ripoti zilichipuza katika vyombo vya habari kwamba virusi vipya vimegunduliwa nchini China na vina uwezo wa kusambaa kutoka kwa nguruwe hadi kwa binadamu.

Hizi ni habari za kutamausha kwa sababu zimejiri wakati ambapo ulimwengu ungali unaendelea kupambana na mkurupuko wa virusi vya corona, ambavyo vimeathiri chumi za mataifa mengi.

Iliripotiwa kuwa wanasayansi walipata ushahidi wa virusi hivyo katika watu walioambukizwa kwenye vichinjio vya nguruwe nchini China.

Wataalamu wanasema virusi hivyo kwa jina, “G4 EA H1N1” vina uwezo wa kushambulia na kusambaa kwenye mfumo mzima wa binadamu wa kupumua.

Hii ina maana kuwa homa hii ya nguruwe ina sifa zinazoshabihiana na homa ya sasa ya corona ambayo imeambukiwa zaidi ya watu milioni 11 na kuangamiza wengine zaidi ya 500,000 kote ulimwenguni.

Hofu ni kwamba wanasayansi waliogundua homa hii mpya wanasema chanjo zote za homa zilizopo haziwezi kudhibiti virusi hivi vipya. Kimsingi, hii ina maana kuwa homa hii mpya haina tiba, na hivyo ina uwezo wa kugeuka janga sawa na hili la corona.

Hii ina maana kuwa mataifa ya ulimwengu haswa ya Afrika yanapasa kujiandaa mapema kukabiliana mlipuko wa virusi hivi vipya.

Serikali ya Kenya inapasa kuwekeza rasilimali nyingi katika sekta ya afya kutokana na funzo ambalo ilipata kutokana na janga corona linaloendelea kutikitisa ulimwengu.

Rasilimali nyingi ziwekezwe katika Taasisi ya Utafiti wa Kimatibabu Nchini (KEMRI) ili iwe na uwezo wa kuendesha utafiti zaidi haswa katika nyanja ya magonjwa ya kuambukiza na ambayo husambaa kwa kasi.

Wataalamu wa taasisi hii wanafaa kufanya kazi zao kwa ushirikiano na wenzao katika mataifa ya nje ambayo yamepiga hatua kubwa katika nyanja ya utafiti.

Kwa kuwa asilimia 80 ya huduma za afya zinasimamiwa na serikali za kaunti, sehemu kubwa ya Sh117 bilioni ambazo zilitengewa Wizara ya Afya zinapasa kutumika kufadhili mipango ya kupiga jeki vituo vya afya katika maeneo ya mashinani.

Huu ndio wakati ambapo serikali inapasa kununua vifaa vya kisasa vya matibabu, kuajiri wahudumu zaidi wa afya na kuwapatia mafunzo maalum.

Isitoshe, Kenya inahitaji kuwa na idadi kubwa ya wataalamu katika nyanja ya magonjwa ya kuambukiza ili iweze kukabiliana na milipuko ya homa hatari kama hii ya corona.

Janga hili la sasa lafaa kuwa funzo kwa viongozi wetu wa serikali kwamba wanafaa kujiandaa mapema kukabiliana na changamoto kama hizi za kiafya ambazo zimeibuka kuwa na athari kubwa kuwa shughuli za kiuchumi.

Japo serikali imefanya kazi nzuri ya kuwahamisisha wananchi kuhusu namna ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona, kuchipuka kwa virusi vipya kuna maana kuwa bado serikali ina kibarua kikubwa.