WASONGA: Ufisadi usipenyezwe katika uajiri wa maafisa wa sensa
Na CHARLES WASONGA
ZAIDI ya vijana 900,000 huingia katika soko la ajira kila mwaka baada ya kukamilisha masomo na mafunzo katika viwango mbalimbali, kulingana na takwimu za serikali.
Japo serikali ilisema uchumi ulikua kwa asilimia 6.3 mnamo mwaka wa 2018 kinaya ni kwamba nafasi za ajira bado ni finyu zaidi, hasusan, katika sekta ya umma.
Hii ina maana kuwa vijana wengi wanahangaika mitaani na vijijini baadhi ya kuhitimu kwa shahada mbalimbali kutoka vyuo vya mafunzo, hali ambayo ni hatari kwa usalama wa nchi.
Hii ni kwa sababu baadhi ya vijana kama hao ndio wamekuwa wakijiunga na magenge hatari ya wahalifu ambayo huhangaisha watu maeneo mbalimbali nchini. Isitoshe, baadhi yao wamehiari kujiunga na makundi ya kigaidi baada ya kupoteza matumaini ya kupata ajira.
Ndiposa napendekeza kwamba serikali inapoanza mchakato wa kuwaajiri zaidi ya watu 164, 000 watakaoendesha zoezi la kuwahesabu watu (sensa) vijana kati ya umri wa miaka 18 na 35 wapewe kipaumbele. Sensa ya mwaka huu itafanyika kuanzia Agosti 24.
Katika miaka ya nyuma Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS) limekuwa likotoa nafasi hizo kwa walimu na watu wengine wenye ajira ya kudumu huku vijana waliokamilisha masomo katika viwango vya kidato cha nne, vyuo vya kadri na vyuo vikuu wakinyimwa nafasi hizo.
Vijana kama hao wapewe nafasi hizi hasa zile za makarani wa kuhesabu watu (enumerators) na wachanganuzi wa data kutumia teknolojia kwa sababu uwezo wanao, mradi wapewe mafunzo mafupi.
Kwa hivyo, serikali inafaa kuhakikisha shughuli ya kuajiri vibarua hao inaendesha kwa njia inayozingatia haki bila mapendeleo.
Na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) iwe chonjo kupambana na maafisa wa serikali ambao huenda wakajaribu kuitisha hongo kutoka kwa maelfu ya watu watakaosaka nafasi hizo.
Nasema hivyo kwa sababu hata kabla ya serikali kutangaza rasmi kwamba zoezi la kuwaajiri watu watakaoendesha sensa hiyo litaanza wiki hii, matapeli fulani tayari walikuwa wameanza kuwahadaa vijana kwamba wanaweza kuwasaidia kupata kazi hizo kwa “ada kidogo”.
Ufisadi usiruhusiwe kupenyeza katika uajiri huo wa watu waliohimu. Suala la Wakenya wasio na pesa za kutumia kuwahonga maafisa husika kunyimwa nafasi halifai kuruhusiwa kutokea. Watakaoathirika zaidi, bila shaka, watakuwa vijana kutoka familia zenye mapato ya chini.
Kwa hivyo, serikali ihakikishe kuwa zoezi hilo linaendeshwa kwa njia huru, haki na yenye uwazi ili vijana wengi wasio na ajira wafaidi.