Makala

Wataalamu wa Jamii ya Waluo sasa wataka ODM ikomesha vita wakiunga mkono Serikali Jumuishi

Na WINNIE ONYANDO January 21st, 2026 Kusoma ni dakika: 2

MUUNGANO wa wataalamu kutoka jamii ya Waluo wamewataka viongozi wa chama cha ODM kudumisha umoja ili kukipa nguvu na usemi mkubwa katika Serikali Jumuisha na mazungumzo ya kubuni muungano na chama cha United Democratic Alliance (UDA) kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Kwenye kikao na wanahabari Jumanne, Januari 20, 2026, jijini Nairobi, walisema kuwa hiyo ndio njia ya kipekee itakayoliwezesha eneo la Luo Nyanza kufaidi kimaendeleo katika serikali hii inayoongozwa na Rais William Ruto na “kusalia serikalini katika utawala ujao.”

“Maendeleo endelevu yanahitaji uwiano wa kisiasa kindani na ushirikiano wa kimkakati katika ulingo wa siasa. Hii ndio maana sisi kama wataalamu kutoka eneo la Luo Nyanza, tunahimiza umoja, nidhamu na uwiano ndani ya ODM, yenye uungwaji mkubwa katika eneo letu, ili kuimarisha nafasi yake ya kutetea utekelezaji wa maendeleo katika serikali jumuisha. Umoja huo pia utaboresha nafasi yake kwenye meza ya mazungumzo kuhusu kuundwa kwa muungano kati yake na UDA kuelekea uchaguzi mkuu ujao,” akasema Bw Fred Okango, akasema aliposoma taarifa kwa niaba ya wenzake.

Kundi hilo linalojulikana kama, ‘Ramogi Professional Caucus” lilikariri kuwa kufaulu kwa mazungumzo kuhusu kuundwa kwa muungamo kati ya ODM na UDA, pamoja na vyama vingine vyenye maono sawa, ndiko kutawezesha eneo la Luo Nyanza kuvuna matunda ya maendeleo baada ya kutwaa mamlaka katika uchaguzi mkuu ujao.

“Kwa miaka mingi eneo letu limesalia nyuma kimaendeleo kwa sababu viongozi wetu na wananch wameegemea mrengo wa upinzani. Tunaamini kuwa hali hiyo itabadiliko baada ya uchaguzi wa 2027 endapo  ODM na UDA zitafaulu kutwaa uongozi wa taifa hili kupitia unahodha wa Rais William Ruto. Msingi wa ufanisi huu uliwekwa na kiongozi huyo pamoja na Hayati Raila Odinga walipotia saini mkataba wa ushirikiano Machi 7, 2025  na kuunda serikali jumuishi,” wakaeleza wanachama wa kundi hilo.

Wito wa Ramogi Professional Caucus umejiri wakati ambapo chama cha ODM kimekumbwa na migawanyiko kuhusu ushirikiano wake na UDA chini ya serikali jumuishi.

Mirengo miwili imeibuka; moja ikiunga mkono serikali jumuishi na kuchaguliwa tena kwa Rais Ruto na mwingi unaoshirikisha viongozi vijana wanaopinga msimamo huo na kushinikiza kuwa ODM iendelee kutekeleza wajibu wake kama chama cha upinzani na idhamini mgombea wa urais 2027.

Mrengo wa wanaounga mkono serikal umeanza mchakato wa mazungumzo kwa ajili ya kuwezesha ODM kubuni muungano na UDA kuelekea 2022, unaongozwa na kiongozi wa chama hicho Dkt Oburu Oginga.

Mrengo wa pili nao unashirikisha Katibu Mkuu Edwin Sifuna na wabunge kadhaa vijana pamoja na mwanawe Raila, Winnie Odinga. Wameonekana kupinga uongozi wa sasa huku wakishinikiza kuandaliwa kwa Kongamano la Kitaifa la Wajumbe (NDC) wa ODM ili viongozi wapya wachaguliwe kukiongoza kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

Wakati huo huo, muungamo wa Ramogi Professional Caucus, pia umemtaka Rais Ruto kufanikisha utekelezaji ahadi 10 zilizoko katika Mkataba wa Maelewano (MOU) ambao yeye na Hayati Odinga walitia saini mwaka jana.

“Ahadi hizo ndizo msingi wa utekelezaji wa mageuzi ambayo yataiwezesha nchi hii kupiga hatua mbele kimaendeleo katika sekta zote. Nguzo zake ni utekelezaji wa mapendekezo ya ripoti ya Nadco, usawa katika uteuzi serikalini, ustawishaji wa ugatuzi, uwezeshaji wa vijana, maadili na uongozi bora, usimamizi bora wa madeni ya nchi, kuendelezwa kwa vita dhidi ya ufisadi, kulinda kwa haki za kikatiba na ulipaji fidia kwa waathiriwa wa maandamano,” akaeleza Bi Rachael Omollo, mtaalamu wa masuala ya Sera za Umma na Utawala.