Makala

Watoto wa mitaani wanavyotumiwa kutekeleza uhalifu Busia

Na KNA September 25th, 2024 2 min read

MJI wa Busia ulio katika mpaka wa Kenya na Uganda, ni makazi ya watoto wa kurandaranda mitaani wanaoongezeka kila kuchao.

Unapotembea katika mitaa iliyojaa watu, utawaona watoto wenye sura zinazoashiria matatizo, mateso na hali ya kutelekezwa.

Wengi ni wavulana na wengine wana umri mdogo wa miaka 7.

Wanaishi katika hali ngumu wakitumia vipande vya katoni kuwa malazi yao.

Wasipopata kazi ndogondogo ama misaada, wengi huishia kulala njaa

Yamkini kwa sababu ya changamoto hizi, wahalifu wanawatumia kufanya biashara za magendo ama ulanguzi wa mihadarati.

Wakati uo huo, baadhi ya familia hutuma watoto hawa mitaani kuomba misaada ama kuchuuza.

Afisa wa Idara ya Haki za Watoto Busia Patrick Mkolwe anakiri kuwa wamejaribu kuwaondoa watoto hao mitaani mara nyingi bila mafanikio.

“Tumejaribu kuwaondoa tangu mwaka jana (2023). Asilimia 80 ya watoto hawa wanatoka Uganda,” alisema Bw Mkolwe.

“Maisha magumu wanayopitia yanafanya wahalifu wawatumie katika ulanguzi wa bidhaa za magendo na mihadarati.”

Katika msako uliopita, waliokoa familia 56 ambapo 36 walikuwa watoto; kati ya wavulana 36, 12 walikuwa Wakenya.

Bw Mkolwe anaomba kuanzishwa kwa kituo cha urekebishaji tabia ya watoto mjini Busia ili wasipelekwe kwenye makao ya watoto.

“Hatuwezi kuwapeleka watoto katika makao ya watoto kwa sababu wanaweza kuwapeleka wenzao mitaani,” alisema.

Analalama kuwa sera za kutunza watoto Uganda ni tofauti na za Kenya huku watoto wengi wa Uganda wakijaa mitaani Busia.

Disko Matanga

Hafla za maombolezo ambayo hufanywa usiku kwa kupiga muziki na densi maarufu Disco Matanga, zimetajwa kuwa miongoni mwa vyanzo vya upotofu wa maadili na kudorora kwa mfumo wa malezi.

“Wavulana huhudhuria disko hizi na ni wazi kuwa wanatambulishwa kwa utumizi wa dawa za kulevya na uhalifu,” alisema Celestine Wesonga, kiongozi wa jamii.

Hata hivyo, Bi Wesonga anasema, disko matanga ni dalili tu ya tatizo kubwa.

“Wavulana hawa hawana mfumo thabiti wa familia, elimu inayostahili ama maelekezo,” alisema.

“Wanapoingia mitaani, wanatoswa katika desturi ya biashara na uhalifu mipakani. Kwa sababu Busia iko katika mpaka, wao hutumiwa kama wasafirishaji wa sukari ya magendo, mafuta na dawa za kulevya.”

Kauli yake ilikaririwa na Kamanda wa Kaunti ya Busia Ahmed Abdille aliyesema watoto hawa hutumiwa kubeba bangi, kemikali ya kutengeneza pombe maarufu ethanol na chang’aa.

“Watoto hawa hukodishwa ili kutekeleza uhalifu… huning’inia kwenye matrela na kuiba mafuta,” alifichua Bw Abdille.

Mashirika ya kibinafsi yanayojihusisha na haki za watoto na yale ya serikali yana habari kuhusu matukio haya yanayozingira maisha ya watoto wa mitaani.

Yanajizatiti kupata suluhu ya kudumu lakini kufikia sasa, bado iko mbali na upeo wa macho.