Makala

Wauguzi washtakiwa kwa kuwamwagia asidi polisi waliokuwa wanachunguza uavyaji mimba Ngara

Na RICHARD MUNGUTI, LABAAN SHABAAN December 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KIFUNGO cha maisha kinamkodolea macho muuguzi Jonah Kipsiror Marori aliyeshtakiwa  kwa madai ya kuwamwagia maafisa watatu wa polisi asidi.  

Haya yalijiri katika kipindi ambacho walikuwa wakichunguza visa vya uavyaji mimba kwenye kliniki yao iliyo katika mtaa wa Ngara, Kaunti ya Nairobi.

Mahakama ilifahamishwa kwamba maafisa hao wa polisi walichomwa usoni, katika viganja vya mikono, tumboni huku nguo zao pia zikichomeka.

Marori alishtakiwa pamoja na Ephraim Mwaura Karumbi mbele ya hakimu mkuu wa Mahakama ya Milimani Ben Mark Ekhubi.

Walikana mashtaka sita ya kuwapa majeraha ya kudumu maafisa watatu wa polisi pamoja na kuendeleza huduma za hospitali bila leseni.

Pia walishtakiwa kwa kuhifadhi sumu na kuendeleza biashara bila idhini ya bodi ya kudhibiti maduka ya dawa.

Marori anashukiwa kuwa aliwamwagia asidi maafisa wa polisi Tom Mbuku, Joyce Otieno na Moses Lelei.

Kiongozi wa mashtaka Bi Virginia Kariuki alieleza mahakama kwamba maafisa hao wamelazwa katika hospitali moja jijini Nairobi wanapopokea matibabu.

Bi Kariuki alipinga agizo la kutaka wawili hao waachiliwe kwa dhamana akisema kesi hii imezua hisia kali na maafisa wa polisi wanahofia maisha yao baada ya shambulizi la Novemba 25, 2024.”

Kiongozi huyo wa mashtaka aliomba mahakama isimwachilie Marori kwa dhamana ya pesa taslimu akishikilia alitekeleza kitendo hicho cha unyama.

Maafisa hao wa polisi waliathiriwa walipoenda kuchunguza ripoti kwamba zahanati hiyo ya kibinafsi ilikuwa ikitumika kuwezesha wanawake kuavya mimba.

“Baada ya kubisha mlango, Marori aliufungua akiwa na jaa la asidi na kuwamwagia kila mmoja wa maafisa hao usoni, mikononi na kwenye tumbo,” Bi Kariuki alieleza mahakama.

Marori alikana mashtaka yaliyomkali likiwemo la kuwapa polisi majeraha ya kudumu.

Akipatikana na hatia, Marori atahukumiwa kifungo cha maisha gerezani.

Washtakiwa waliomba waachiliwe kwa dhamana wakisema “watatii masharti ya korti kuhusiana na dhamana.”

Bw Karumbi, mwenye umri wa miaka 61, aliomba mahakama imwachilie kwa dhamana ya pesa taslimu.

“Mheshimiwa, naomba uniachilie kwa dhamana isiyo ya kiwango cha juu. Mimi nimepoteza uwezo wa kusikia kwa sababu ya kulala kwenye sakafu tangu Novemba 25, 2024 tulipokamatwa,” Bw Karumbi alijitetea.

Aliongeza: “Nimechangia kukua kwa uchumi wa nchi hii kwa miaka mingi. Nimekuwa nikilipa kodi kwa mamlaka ya ushuru nchini tangu zamani. Kwa hivyo, ninaomba uniachilie kwa dhamana ndogo niwaombe marafiki wangu watatu waliofika kortini kufuatilia kesi hii.”

Bw Marori aliomba mahakama izingatie kwamba yeye ni baba wa watoto watano na wawili wanasoma katika vyuo vikuu.

Korti iliambiwa watoto wengine wako shule za upili na wengine shule za msingi.

“Ikiwa nitapewa dhamana ya juu basi elimu ya wanangu itavurugwa. Ninaomba unionee huruma,” Marori alimsihi hakimu.

Akitoa uamuzi wa dhamana, hakimu alisema upande wa mashtaka haupingi iwapo washtakiwa wataachiliwa kwa dhamana iliyo na mdhamini.

Bw Ekhubi alimwagiza Marori alipe dhamana ya Sh600,000 na mdhamini mmoja wa kiasi sawa na hicho.

Bw Karumbi aliyekabiliwa na mashtaka ya kuendeleza kliniki bila leseni na kuuza dawa kinyume cha sheria, aliachiliwa kwa dhamana ya Sh300,000 na mdhamini mmoja au alipe dhamana ya pesa tasilimu Sh200,000.

Bw Ekhubi aliamuru kuwa kesi hiyo itatajwa baada ya wiki mbili ili kutengewa siku ya kusikizwa.

Wauguzi hao wanadaiwa kutekeleza uhalifu huo mnamo Novemba 25, 2024 katika eneo la Ngara jijini Nairobi.

Wauguzi Jonah Marori (kulia) na Ephraim Mwaura wakiwa kizimbani katika Mahakama ya Milimani Desemba 2, 2024 waliposhtakiwa kwa madai ya kuwachoma maafisa watatu wa polisi kwa asidi na kuendesha kliniki bila leseni. Picha|Richard Munguti