WENDAWAZIMU WA LUANDA: Ni bangi au urogi?
NA FAUSTINE NGILA
UNAPOTAJA neno ‘Luanda’ kwa wakazi wa magharibi mwa Kenya, kinachowajia akilini ni taswira ya soko lililojaa wendawazimu na watumizi wa bangi kupindukia.
Luanda ni mji ulioko katika barabara ya kutoka Kisumu kwenda Busia katika kaunti ya Vihiga. Barabara za lami kutoka hapa kuelekea miji ya Maseno, Siaya, Busia na Kakamega huimarisha hadhi yake kama kituo muhimu cha biashara, hasa bidhaa kutoka Uganda.
Pia, ni mji ulio karibu na Chuo Kikuu cha Maseno, shule za upili za Maseno, Bunyore Girls na Chavakali Boys.
Ndio mji wa nyumbani wa aliyekuwa Spika wa Bunge la Kitaifa, Kenneth Marende na aliyekuwa Msemaji wa Ikulu Manoah Esipisu.
Nimesimama kando ya muuzaji wa samaki mjini hapa. Mwanamume wa umri wa makamo anajongea huku mdomo umejaa majani ya kijani kibichi, lakini hayatafuni, hawezi kuongea.
Anatoa kijikaratasi kutoka kwa matambara aliyovaa, anakikunjua kisha kuchukua ungaunga wa kijani kibichi, anaunusia kisha kuulamba mbele ya jumba moja lililo karibu huku amefumba macho. Kisha anainamisha kichwa kwa sekunde tano na kuondoka bila kusema lolote wala kutazama mtu.
Hajavaa viatu na nyayo zake zimepasuka, lakini ukifuata njia aliyopitia utadhani alikuwa amevaa viatu vya kimaasai almaarufu akala. Nywele zake zimechakaa, zina rangi ya kikahawia na ni chafu, utadhani chawa wamefika paradiso pale. Hakuna anayemjali. Aliyovaa si longi, ni tambara jeusi alilofunga kiunoni, hana haja ya shati.
Baada ya kupigwa na butwaa na mwenendo wake, ninamuuliza mama anayeuza samaki karibu nami sababu ya kuinamisha kichwa mbele ya jengo lile kisha kutoweka.
“Hilo kwake ni kama ibada, yeye huja hapa kila alasiri na kuinamishia jumba lile kichwa kama ishara ya heshima. Yeye husema anaheshimu jengo hili kwa kuwa ndilo lilikuwa la kwanza kujengwa hapa wakati wa wakoloni,” ananieleza.
Huo ni mfano mmoja. Siku yoyote ya juma, mji wa Luanda huwa na wendawazimu au watu wenye matatizo ya kiakili ambao hufanya kila aina ya vituko na mambo ambayo yatamshangaza kila mgeni anayezuru mji huu.
Lakini wafanyabiashara wa eneo hili hudai baadhi yao si wendawazimu, wengi hujifanya kuwa punguani ili wapate huruma ya wapita njia wanapoomba vihela vya kujikimu kimaisha.
Kumekuwa na taarifa nyingi kuhusu jinsi baadhi yao hujifanya wana akili taahira mchana wakati wa siku za soko ili kuomba chakula. Katika siku zingine, wao ni wanajamii wa kawaida ambao hufanya vibarua kulisha familia zao.
Na si wanaume tu, wanawake, vijana na watoto pia utawapata wakifanya mambo ya ajabu ajabu.
“Wale ambao walisoma hadi chuo kikuu na kukosa kazi huenda kujiliwaza katika Chuo Kikuu cha Maseno, ambao hufurahia mazingira ya wanafunzi kisha kulala huko,” ananiambia mama huyo.
Lakini wengi ni wale ambao hawasumbui yeyote. Wanafanya mambo yanayoongoa nafsi zao kama kuokota karatasi, kuimba huku wengine wakinengua viuno wakisikia muziki wanaopenda.
Katika Chuo Kikuu cha Maseno kulikuwa na mama mmoja aliyekuwa anafoka kwa njia kwa lugha ya Kiingereza huku akitaja maneno mazito ya usomi.
“Mwanamke huyo alikuwa mhadhiri hapa chuoni lakini akapata kasoro ya akili na akaacha kufundisha. Akichoka kuzurura, atatulia chini ya mti kisha kuanza kufundisha wanafunzi hewa huku akiwapa maagizo,” James Ondimu, ambaye ni mwanabodaboda ananieleza.
Mama mmoja alizua kioja katika benki ya Equity mjini Luanda aliposimama langoni akitaka kila mtu aliyetoka mle ndani ampe hela, lakini noti pekee, ukimpa sarafu za chuma alikuwa anazitupa. Polisi waliojaribu kumwondoa hawakufaulu. Hatimaye alienda zake baada ya kikombe chake kujaa noti. Hakuoenekana tena.
Nilipowahoji baadhi ya wakazi wa mji huu kuhusu kiini cha idadi kubwa ya watu wa aina hii eneo hili, walilaumu bangi, urogi na kujifanya.
“Matumizi ya bangi na dawa za kulevya kutoka Busia na Uganda ndio yameathiri akili zao. Bangi huvutwa, kutafunwa na kuwekwa kwa vyakula peupe. Tumejaribu kuzima uovu huu lakini si rahisi,” akasema afisa mmoja wa usalama ambaye hakutaka kutajwa.
Na kwa kweli unapotembea katika soko hili, utakutana na watu wengi wenye akili timamu wakivuta bangi bila uoga huku wamefuga rasta kichwani.
“Soko hili kwetu ni Jamaica ndogo. Hii ndiyo asili ya wasanii wote wa Reggea unaowajua lakini wamechukua muda sana kurudi hapa nyumbani,” anasema kijana mmoja huku moshi ukimtoka kama lori kuukuu.
La kushangaza ni kuwa familia za walioathirika zaidi na ‘wendawazimu’ huu haziwapeleki hospitali kwa uchunguzi na tiba.
“Wengine ni watu waliokuwa wanaishi maisha ya kufana na familia zao lakini utawapata wakirandaranda hapa. Sisi huamini wamerogwa kwa kuwa si kawaida mtu kuacha familia yake awe akilala kwa jalala,” anasema Stacy Ogoto, mwanachuo wa saikolojia katika Chuo Kikuu cha Maseno.
Ingawa maafisa wa polisi wa Maseno kwa wakati mmoja walizindua Operesheni Rudi Nyumbani, na kuwarudisha baadhi ya wendawazimu nyumbani kwao, tatizo hilo bado lipo.
Wakazi huamini watu hawa hutoka miji jirani hasa Kisumu. “Umaskini na hali kuwa Luanda ni mji mdogo wenye watu wengi, huenda ndio sababu watu hujifanya punguani ili kupata chakula,” anasema Peter Mugenda, mfanyabiashara wa Maseno.
“Tuko karibu na Kisumu ambako kuna wendawazimu, ila Kisumu ni jiji kubwa na huwezi kuwaona, lakini Luanda ni mji mdogo na ni rahisi kuwaona.”
Aliyekuwa mbunge wa eneo hili, mwendazake Wilson Mukuna, kwa wakati mmoja aliirai serikali iwaruhusu wakazi wakuze bangi kwa mauzo ya nje ya nchi kwa kuwa hawana mashamba ya kutosha ya kuzalisha chakula.
Msomi, mtafiti na mchanganuzi wa sera katika Taasisi ya Afrika kuhusu Sera za Umma (APPI), Prof Inonda Mwanje anasema wendawazimu mjini Luanda ni jambo la kawaida kama miji mengine.
Hata hivyo, anasema serikali imetelekeza eneo hilo kwani inafaa kuweka miundomsingi ya kukabiliana na tatizo hilo.
“Serikali inafaa kujenga kituo cha matibabu kuhudumia watu wenye kasoro ya akili kwa kuwa wao pia ni binadamu na kuna haja ya kuwarudisha kwa jamii wachangie makuzi ya taifa,” anasema.