Makala

Jumbe za WhatsApp zinavyosukuma Wakenya jela

Na JOSEPH WANGUI August 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KATIKA kipindi ambapo matumizi ya vifaa vya kidijitali yanaendelea kuongezeka nchini Kenya, idadi ya Wakenya wanaofikishwa mahakamani na kuhukumiwa kwa jumbe za matusi, kashfa au chuki zinazochapishwa kwenye makundi ya WhatsApp imeongezeka kwa kasi.

Mwelekeo huu unatokana na matumizi ya mfumo wa haki ya jinai kushughulikia mizozo ambayo inachochewa na teknolojia ya mawasiliano inayobadilika kwa kasi.

Hali hii ilikuwa nadra sana miaka 15 iliyopita.

Aliyehukumiwa hivi karibuni kwa kosa la jinai kutokana na ujumbe wa WhatsApp ni Donald Mwendwa Nzau, anayejulikana pia kama Password Mwendwa au Abdulaziz Mwendwa.

Wiki mbili zilizopita, alihukumiwa kulipa faini ya Sh25,000 au, la sivyo, atumikie kifungo cha miezi sita gerezani.

Alipatikana na hatia kwa kosa la kuchapisha taarifa za uongo, kinyume na Kifungu cha 23 cha Sheria ya Uhalifu wa Mtandao na Matumizi Mabaya ya Kompyuta, Sheria ya 2018.

Sheria hiyo inakataza kuchapisha taarifa za uongo kupitia mfumo wa kompyuta au vyombo vingine vya habari kwa nia ya kusababisha hofu, ghasia, au kuchafua sifa ya mtu.

Mkosaji anaweza kutozwa faini ya hadi Sh5 milioni, kifungo cha hadi miaka 10, au vyote viwili.

Katika kesi ya Mwendwa, ujumbe huo ulichapishwa katika kundi la WhatsApp lijulikanalo kama Lamu Yetu Sote. Ujumbe huo ambao gazeti hili haliwezi kuuchapisha ulimkera Bw Shee Kupi Shee, ambaye aliripoti kwa polisi na kusababisha kukamatwa kwa Mwendwa.

Mwendesha mashtaka alidai kuwa ujumbe huo haukuwa wa kweli na ulikusudiwa kuchafua sifa ya Bw Shee.

Kulingana na ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (CA) kwa robo ya Januari–Machi 2025, idadi ya usajili wa simu ilifika milioni 42.35, ongezeko la asilimia 2.1 kutoka robo iliyotangulia.

WhatsApp ni mojawapo ya majukwaa maarufu zaidi, ikitumiwa na asilimia 54.4 ya Wakenya kufikia Desemba 2024, ikiwa ya pili baada ya Facebook (asilimia57.1), kulingana na takwimu za CA zilizotolewa Machi 2025.

Hata hivyo, wakosoaji wanasema sheria hiyo imetumiwa kama silaha na serikali pamoja na watu wenye ushawishi kuwanyamazisha wakosoaji.

Mwezi uliopita, wanaharakati watatu wa haki za binadamu Joshua Okayo, kiongozi wa wanafunzi katika Kenya School of Law, pamoja na Davis Thuranira na Brian Kithinji waliwasilisha ombi bungeni kutaka kurekebishwa kwa Vifungu vya 22 na 23 vya Sheria hiyo.

“Tangu 2018, watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii wakiwemo wanablogu, wanahabari, watoa taarifa na watengenezaji wa maudhui wamekuwa wakikamatwa kiholela, kutishwa, kuzuiliwa au kushtakiwa kwa sababu tu ya kuchapisha ,katuni au taarifa inayoitwa ya ‘uongo’,” linasema ombi hilo.

Katika Mahakama ya Makadara jijini Nairobi, mtumiaji wa WhatsApp alifikishwa kortini mwaka jana kwa madai ya unyanyasaji wa mtandaoni katika kundi la Woodley Residents Welfare.

Kesi hiyo bado inaendelea.

Mjini Kisumu, mwanamume mwenye umri wa miaka 24, Abdala Mustafa, alipigwa faini ya Sh50,000 au afungwe miaka mitatu kwa kupatikana na video zinazohusiana na ugaidi.

Alikiri kupokea video hizo kupitia kundi la WhatsApp lakini alidai hakuwa anajua kuwa ni kosa. Mahakama ilikataa utetezi huo, ikisema kundi hilo pia lilikuwa likieneza ujumbe wa kuhamasisha vijana kujiunga na kundi la kigaidi.

Hata kabla ya Sheria ya Uhalifu wa Mtandao kuanza kutumika mwaka 2018, wasimamizi wa makundi ya WhatsApp tayari walikuwa wakishtakiwa.

Katika miji ya Malindi na Kajiado, wasimamizi wawili walifunguliwa mashtaka kwa kusambaza jumbe za uchochezi na picha za miili ya watu waliokufa.