Makala

Wimbi la ufutaji kazi lagubika kampuni ‘ushuru wa zakayo’ ukilemea biashara nyingi

Na PETER MBURU November 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

HATUA ya kampuni kubwa za humu nchini kutangaza mpango wa kufuta mamia ya wafanyakazi imezidi kufichua hali duni ya kiuchumi inayokumba maelfu ya biashara, kutokana na kupanda kwa ushuru na mauzo kushuka.

Kampuni za G4s na Tile & Carpet na Procter & Gamble (P&G), ni za hivi punde zaidi kutoa ilani za kufuta wafanyakazi zikilaumu ughali wa kufanya biashara, japo mamia ya kampuni zingine zimekuwa zikiwatimua wafanyakazi wao mwaka huu, hali ambayo imeathiri maelfu ya watu na kupunguzia serikali mapato.

Katika barua kwa Wizara ya Leba mapema mwezi huu, kampuni ya G4s ambayo huhudumu katika sekta ya ulinzi ilisema itawatimua wafanyakazi 400 kati ya mwezi huu na Aprili mwaka ujao, ikitaja athari za ugumu wa kiuchumi kuwa chanzo.

“Kutokana na kuendelea kupungua kwa biashara ambako kumechangiwa na athari za changamoto za kiuchumi zikipelekea kupungua kwa mapato na gharama ya juu ya kuendesha biashara, tunajuta kujulisha Wizara ya Leba kuhusu mpango wa kampuni hii kuondoa nafasi fulani za kazi. Mpango huu utaathiri takriban wafanyakazi 400 katika maeneo tofauti Kenya,” barua hiyo kutoka kwa Mkurugenzi wa wafanyakazi G4s, Helgah Kimanani, ikasema.

Bila kutaja idadi ya wafanyakazi watakaoathirika, kampuni ya Tile & Carpet ambayo hutengeneza bidhaa za ujenzi pia imearifu Wizara ya Leba kuwa ina mpango wa kuwafuta wafanyakazi katika idara ya utengenezaji bidhaa iliyoko Athi River kuanzia mwezi ujao.

“Kutokana na kufifia kwa uhitaji wa bidhaa tunazotengeneza, changamoto za kiuchumi na kupanga upya mikakati, imebidi tupunguze shughuli zetu katika kiwanda cha utengenezaji bidhaa ili kampuni iweze kujihimili,” barua ya mkuu wa wafanyakazi Mandeep Degon ikasema.

Japo kampuni hizi ndizo za hivi punde zaidi kuwatimua wafanyakazi kutokana na ugumu wa kiuchumi, mamia ya kampuni zingine zimekuwa zikiwafuta wafanyakazi mwaka huu, zaidi kutokana na kudodora kwa uchumi.Procter & Gamble (P&G), kampuni ya Amerika inayotengeneza bidhaa za usafi kama sodo nayo inasemekana kuwa na mpango wa kutimua wafanyakazi wake hatua ambayo huenda ikaathiri watu zaidi 800 ikinuia kuondoka nchini kufikia Desemba 2024.

Sawa na G4S na Tile and Carpet, kampuni ilitaja gharama ya juu ya kufanya biashara nchini.Biashara nyingi zimezidi kulemewa na mzigo wa wafanyakazi wengi kwani serikali imepandisha ushuru na kuacha gharama ya bidhaa zinazotumika na biashara nyingi zikiwa ghali, licha ya Wakenya wengi kuzidi kupoteza uwezo wa kununua kutokana na mapato yao kuzidi kuvamiwa na ushuru baada ya mwingine.

Utafiti wa hivi karibuni kutoka kwa Benki Kuu ya Kenya (CBK) ulionyesha kuwa, mwaka huu pekee, asilimia 42 ya kampuni zimetimua wafanyakazi wa vibarua, asilimia 31 ya kampuni zimetimua wafanyakazi wa kandarasi na asilimia 25 ya kampuni zimefuta wafanyakazi wa kudumu.

Kulingana na utafiti huo uliohoji wakuu wa kampuni katika sekta tofauti, hii ni kumaanisha kuwa, moja kati ya kila kampuni nne nchini zimefuta wafanyaklazi wa kudumu, huku takriban nusu ya kampuni zikifuta wafanyakazi wa vibarua.

Utafiti huo uliofanywa Septemba ulionyesha kuwa, japo hali katika sekta yabenki imekuwa nafuu huku zikizidi kuajiri, sekta zingine za kiuchumi zimekuwa zikitimua wafanyakazi kutokana na hali ngumu ya kiuchumi.

“Kampuni (kando na benki) zilitarajia kuwa gharama kubwa ya uzalishaji, matumizi mengine, faida ya chini, kufifia kwa biashara, kupungua kwa mapato na gharama ya juu ya utendakazi vimepunguza haja ya kuajiri wafanyakazi 2024,” ripoti ya utafiti huo ikasema.

Kwa jumla, ripoti hiyo ilionyesha kuwa japo asilimia kubwa ya benki (76) zinatarajia kuajiri wafanyakazi wengimwaka huu ikilinganishwa na wafanyakazi ambao ziliajiri mwaka jana, asilimia 62 ya kampuni katika sekta zingine zimehofia kuwafuta wafanyakazi mwaka huu.

Matokeo haya yanawiana na ripoti nyingine kutoka kwa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) mwezi uliopita, iliyoonyesha jinsi ushuru inaokusanya kutoka kwa wafanyakazi wa kampuni katika sekta za kibinafsi ulipungua kwa Sh1.2 bilioni, ndani ya mwezi mmoja pekee.

“Hii ni kutokana na kupungua kwa mshahara wa wafanyakazi kutoka Sh78,034 (wastani) kipindi cha Juni-Septemba 2023 hadi Sh75,781 kipindi cha Juni-Septemba 2024, ikiashiria athari za mageuzi yanayoendelea katika kampuni tofauti ili kudhibiti gharama,” KRA ikasema.

Mamlaka hiyo ilikuwa ikizungumzia hali ambapo kampuni nyingi zimezidi kuwatimua wafanyakazi wanaolipwa mishahara ya juu, kisha kutangaza nafasi zao wazi na kuajiri watu wengine kwa mishahara ya chini.

Shirika la Waajiri nchini (FKE) linatarajiwa kutoa ripoti ya kuonyesha jinsi sekta ya uajiri nchini imeathirika mwishoni mwa mwezi huu. Mwaka uliopita, FKE ilitangaza kuwa angalau wafanyakazi 70,000 walipoteza ajira tangu Novemba 2022.