Wito afisa aliyesimamia ujenzi wa nyumba iliyoporomoka South C atimuliwe
KUFUATIA kuporomoka kwa jengo mtaani South C mnamo Januari 5,2026 ambapo watu wawili walikufa, Mahakama Kuu ya Milimani imeombwa iamuru afisi ya Rais na Serikali ya Kaunti ya Nairobi imtimue kazini afisa mkuu anayesimamia ustawi na ujenzi jijini Bw Patrick Analo Akivaga.
Kwenye kesi iliyoshtakiwa na mwanaharakati Francis Awino, Mahakama kuu imeelezwa Bw Akivaga alizembea kazini mwake na kuruhusu ujenzi wa jengo hilo la orofa 14 uendelee ilihali mamlaka ya kitaifa ya ujenzi ilikuwa imetoa onyo ujenzi usiendelee.
Bw Awino amemlaumu Bw Akivaga kuruhusu ujenzi uendelee bila ya kuidhinishwa na kamati ya ujenzi inayokagua ramani za ujenzi kuona ikiwa zinaambatana na sheria.
Mahakama imeambiwa mbayana Bw Akivaga alimruhusu mmiliki wa jengo hilo kuongeza orofa kutoka 12 hadi 14 bila ya kuzingatia sheria na mwongozo wa ujenzi.
Na wakati huo huo Mahakama kuu imeambiwa Bw Akivaga aliyetwikwa majukumu ya kuhakikisha ujenzi wa mijengo yote katika kaunti ya Nairobi umefanywa kwa mujibu wa sheria za ujenzi “hajawahi zuru mradi huo kuukagua na kuhakikisha uko sambamba na sheria za ujenzi.”
Kutokana na kuzembea kwake kazini mwanaharakati huyu ameelezea korti Bw Akivaga alikaidi Vifungu nambari 10, 21,22,23,26,35,47,73 na 201 vya Katiba ya Kenya vinavyotoa haki ya kuishi katika mazingira safi, kutotishwa , kuhatarishiwa maisha na watumishi wa umma kuhakikisha kuna usawa , uangavu, uwajibikaji na udumishaji wa sheria.
Mahakama imeambiwa Bw Akivaga ambaye ndiye afisa mkuu katika serikali ya kaunti ya Nairobi aliidhinisha kinyume cha sheria ujenzi huo kuendelea ilhali mamlaka ya kitaifa ya ujenzi (NCA) na chama cha wahandisi nchini (EBK) vilikuwa vimeelezea wasi wasi wake na uthabiti wa jengo hilo.
Bw Awino anaomba mahakama kuu imwagize Bw Akivaga ashirikiane na wachunguzi kutoka NCA , EBK na taasisi nyingine zinazohusika na ujenzi ndipo ukweli upatikane.
Mahakama pia imeombwa imshurutishe Bw Akivaga akabidhi nakala za mawasiliano yote aliofanya na mwenye kandarasi aliyesimamia ujenzi wa jengo hilo tangu 2023.
Mahakama imeelezwa Bw Akivaga ameungama kwamba aliruhusu ujenzi kuendelea kabla ya idara nyingine husika kuruhusu ujenzi uendelee.
Pia korti imeelezwa kwamba Gavana wa Nairobi aliyezuru eneo la mkasa huo alisema uchunguzi kamili utafanywa na mwenye kupatikana na utepetevu atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Mahakama imeelezwa kutokana na tabia ya Bw Akivaga maisha ya wafanyakazi katika mjengo na wananchi yalihatarishwa ndipo watu wawili waliaga.
Korti imeombwa iratibishe kesi hiyo kuwa ya dharura na kutoa maagizo Bw Akivaga atimuliwe kazini.