Ajabu makanisa kufungwa Ujerumani waumini wakipungua
NCHINI Ujerumani, mabadiliko makubwa ya kijamii na kidini yamesababisha kupungua kwa idadi ya Wakristo, hali inayolazimisha baadhi ya makanisa kufungwa au kubadilisha matumizi.
Kupungua huku kumeacha majengo wazi jambo linalofanya matumizi ya kanisa kubadilika.
Kanisa la Mtakatifu Anna (St. Anna), lililoko Gildehaus, eneo la Bad Bentheim karibu na mpaka wa Ujerumani na Uholanzi, ni miongoni mwa makanisa yaliyoathiriwa.
Hivi karibuni, kanisa hilo dogo la Kikatoliki lilifungwa rasmi baada ya kuandaliwa misa ya mwisho, iliyohudhuriwa na waumini wengi kwa hisia nzito.
Wakati wa ibada hiyo ya kuaga, kwaya iliimba na misa ilipokamilika, waumini walishiriki katika zoezi la kutoa masalia ya watakatifu (reliquia) kutoka madhabahu, ishara ya mwisho ya kanisa hilo kuacha kuwa mahali patakatifu.
Hatua hiyo, hufanya jengo lililowekwa wakfu kubadilishwa na kuwa jengo la matumizi ya kawaida.
Padre Hubertus Goldbeck alisema tukio hilo lilikuwa la kugusa moyo, akieleza masikitiko yake kutokana na kufungwa kwa kanisa hilo lililohudumia waumini kwa miaka mingi.
Alisema hali hiyo inawakilisha maumivu yanayowakumba Wakristo wengi nchini humo.
Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2024 pekee, Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiinjili la Ujerumani (EKD) yalipoteza zaidi ya waumini milioni moja kutokana na watu kujiondoa kanisani.
Kwa sasa, ni takribani asilimia 45 tu ya Wajerumani wanaosalia kuwa wanachama wa makanisa hayo mawili, ikilinganishwa na karibu asilimia 69 miaka 30 iliyopita.