Wizara yahitaji pesa zaidi kusambaza mbolea ya bei nafuu
WIZARA ya Kilimo inahitaji kima cha Sh20 bilioni ili kusambaza mbolea ya bei nafuu kwa wakulima Mwaka wa Fedha 2024/2025.
Kulingana na Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo, Dkt Andrew Karanja, kiwango hicho kitasaidia kukithi hitaji la taifa la mifuko milioni 12 ya fatalaiza inayotakikana misimu ya mvua ya muda mfupi na mrefu, ijayo.
Tayari, Dkt Karanja anasema msimu wa mvua fupi umeshughulikiwa na sasa Wizara yake inalenga kupata magunia milioni 7.2 ya msimu wa mvua ndefu 2025.
Waziri Karanja alisema hayo Jumatano, Desemba 18, 2024 katika makao makuu ya Bodi ya Kitaifa Kuhusu Uzalishaji wa Nafaka (NCPB), Nairobi, wakati wa uzinduzi wa usambazaji na usafirishaji wa magunia milioni 4.9 ya mbolea.
Pembejeo hiyo inayofadhiliwa na serikali kupitia mpango wa ruzuku ya mbolea, inatarajiwa kuwa imefikia wakulima Januari 2025.
“Tunahitaji kima cha Sh20 bilioni kuhakikisha Mwaka wa Fedha 2024/25 tunawahi magunia milioni 12. Tunaendelea kujadiliana na Wizara ya Fedha na Hazina ya Kitaifa,” Dkt Karanja akasema.
NCPB ndiyo imejukumika kusambaza fatalaiza ya bei nafuu kote nchini, kupitia maghala yake.
Mpango huo ambapo mkulima anauziwa mbolea mfuko wa kilo 50 kwa Sh2, 500 ulianzishwa mwaka jana, na Rais William Ruto ameusifia kuongeza kiwango cha uzalishaji mahindi nchini.
Kuafikia magunia milioni 7.2 yanayohitajika kwa ajili ya msimu wa mvua ndefu mapema 2025, Dkt Karanja alisema Wizara yake ilikuwa imekadiria bajeti isiyopungua Sh9 bilioni, ila kiwango hicho kizima hakikupatikana kwa sababu ya changamoto za kifedha serikalini.
Alidokeza kwamba Wizara yake ilipata Sh7.5 bilioni kwa minajili ya shughuli hiyo.
“Tunazungumza na Hazina ya Kitaifa ili tuwahi kiwango cha mbolea inayotakikana msimu wa mvua ndefu 2025,” Waziri Karanja alielezea.
Kuhusu magunia milioni 4.9 yaliyotolewa Jumatano, kampuni 13 ndizo zilipata zabuni ya kusambaza fatalaiza hiyo kwa NCPB.
Dkt Karanja alisema ameweka mikakati kabambe kuhakikisha kwamba wakulima hawasambaziwi mbolea feki kama ilivyoshuhudiwa 2023, ambapo amebuni kikosi maalum kupiga msasa fatalaiza inayopokewa na NCPB.
Mtangulizi wake, Bw Mithika Linturi ndiye alikuwa na mikoba ya uongozi katika Wizara ya Kilimo.
“Timu hiyo inajumuisha maafisa kutoka Wizara ya Kilimo, NCPB, asasi za kitaifa kufanya uchunguzi na ujasusi, KEBS, kati ya wadauhusika wengine kubaini ubora wa bidhaa.”
NCPB inapaswa kupokea mbolea baada ya kupewa cheti kuonyesha pembejeo imeafikia ubora wa bidhaa, na kikosi hicho maalum kinafuatilia usafirishaji kuanzia ngazi ya kitaifa (Nairobi) hadi katika kaunti.
Mbolea inayosambazwa, imezingatia vigezo vya udongo na mahitaji ya mimea, Mkurugenzi Mkuu wa NCPB, Samuel Karogo akisema inajumuisha mbolea ya humu nchini na iliyoagizwa ng’ambo.
“Kwa sababu ya mahitaji ya mimea, tumesawazisha ya kutoka nje na iliyoundiwa nchini,” akasema Bw Karogo.
Afisa huyo, hata hivyo, hakufichua nchi ambazo mbolea iliyoagizwa nje imetolewa.
Alithibitisha kwamba wameshirikisha waundaji wanaotengeza fatalaiza, kwa mujibu wa vigezo faafu vilivyowekwa.
Kampuni zinazosambazia NCPB pembejeo hiyo, zimepewa hadi Januari 15 ili kuhakikisha wakulima wanaipata kwa wakati ufaao.
Kando na maghala ya NCPB kutumika kusambazia wakulima, serikali mara hii inashirikisha vyama vya ushirika na maduka ya kuuza bidhaa za kilimo (agro vets).
Inatolewa kwa wakulima waliosajiliwa kidijitali, na Waziri Karanja alisema karibu maduka 7, 600 ya bidhaa za kilimo yatasaidia kuwafikishia mbolea ili kuwapunguzia gharama.