Makala

ZUENA ABDALLAH: Dhamira yagu ni kukuza vipaji ibuka

June 4th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

UKWELI wa mambo ni kwamba wahenga waliposema penye nia pana njia hawakupaka mafuta kwenye mgongo wa chupa, maana ndivyo ilivyo tangu zama hizo mpaka sasa. 

Usemi huo umeonyesha mashiko ya haja miongoni mwa jamii. Aidha ni msemo unaozidi kudhihirishwa na wengi ambao wameamua kujituma kisabuni kwa kujiamini wanaweza huku wakilenga kutimiza malengo yao maishani.

Princess Zuena Abdallah ni kati ya waigizaji wanaokuja nchini anayewachana maprodusa wanaopenda kuendeleza kasumba ya kuwadunisha hadhi wanawake.

Kipusa huyu ambaye kisanaa anafahamika kama First Princess, Zawadi pia Nalubega anasema aliwahi kunyimwa ajira mara tatu baada ya kupigia chini ombi la maprodusa waliokuwa wanamtaka kimapenzi.

”Wasichana warembo hupitia wakati mgumu maana wanaume wengi huwa wanataka tuwe na uhusiano wa mapenzi nao ili watupatie ajira ya kuigiza katika filamu wanazosimamia,” alisema na kuongeza kuwa suala hilo limechangia wengi wao kujikuta kwenye wakati mgumu.

Aidha anaponda maprodusa wa hapa nchini kwa kutounga mkono sanaa ya waigizaji wazalendo. ”Pia sina shaka kutaja kwamba maprodusa wetu wamekosa ubunifu kama wenzao katika mataifa yanayoendelea ikiwamo Tanzania, Nigeria na Afrika Kusini kati ya mengine,” akasema na kuongeza kuwa Wakenya wana wivu sana.

Katika mpango mzima msanii huyu amesema amepania kupaisha kipaji chake ili kuinua Kenya kimataifa katika tasnia ya uigizaji.

Mwanzo wa ngoma mwana dada huyu anasema alivutiwa zaidi na masuala ya uigizaji alipotazama filamu iitwayo ‘Heaven Sent’ ya kati ya wasanii wa Bongo, Jacqueline Wolpher.

Kisura huyu raia wa Uganda aliyedhamiria kuhitimu kuwa mtangazaji kwenye runinga alianza masuala ya burudani kama dansa katika kundi la Pillars of Kibra mtaani Kibera, Nairobi miaka kumi iliyopita. Kisha mwaka mmoja baadaye alijiunga na makundi ya kuzalisha filamu kupitia mwongozo wa vitabu vya riwaya

Kisura huyu anajivunia kushiriki filamu nyingi tu ikiwamo ‘Papa Shirandula (Citizen TV),’ ‘Anikwa (Swith TV),’ Kelele FM (K24 TV)  na ‘Nyundo Utosini  (KBC, Maisha Magic East na K24).’

Demu huyu aliyevutiwa na uigizaji tangia akiwa mtoto anasema anatamani sana kutinga upeo wa kimataifa na kuwapiku kati ya wana maigizo mahiri kama Jacqueline Wolpher (Tanzania) na Mercy Johnson (Nigeria). Johnson ni kati ya waigizaji mahiri ambao hushiriki filamu za Kinigeria (Nollywood) ikiwamo ‘Weeping Soul,’ ‘Husters,’ ‘Heart of a fighter,’ ‘Royal Tears,’ na ‘Dumebi the Dirty Girl,’ kati ya wengine.

Kisura huyu anamiliki brandi yake inayofahamika kama Vuma Productions aliyoanzisha mapema mwaka huu. Chini ya brandi yake mwigizaji huyu aliyezaliwa mwaka 1992 anatarajia kuzindua filamu ya kwanza inayofahamika kama ‘Mpango wa kando.’ ”Chini ya brandi yangu ninalenga kukuza wasanii wanaokuja maana wapo wengi tu mitaani lakini hawajafaulu kupata nafasi popote,” alisema.

Katika masuala ya mahusiano anasema amebarikiwa mtoto mmoja pia ana mpenzi Mkenya wanayepanga kufunga ndoa naye mwaka ujao.

Anashauri wenzie wafahamu wanachotaka katika tasnia ya filamu kutokana na suala la wanaume wengi kuwataka kimapenzi. Pia anahimizi wasanii wanaokuja wajitume wanapopata nafasi ya kuigiza na kamwe wasivunike moyo.