Makala

Makuu aliyokusudia kufanya Jenerali Ogolla katika eneo la Boni

April 26th, 2024 3 min read

NA KALUME KAZUNGU

VIONGOZI na wakazi wa maeneo yanayokumbwa na utovu wa usalama Kaunti ya Lamu wamefichua jinsi kifo cha ghafla cha Mkuu wa Majeshi nchini, Jeneral Francis Ogolla kilivyowaacha na huzuni wakikumbuka jinsi ambavyo jeshi linawasaidia kukabili adui.

Wakazi, hasa wale wa vijiji vya ndani ya msitu wa Boni na mpakani mwa Lamu na Somalia, kwa miaka mingi wamehangaika kufuatia kukithiri kwa utovu wa usalama unaochangiwa na magaidi wa Al-Shabaab.

Hali hiyo ilifanya serikali kuu kuzindua operesheni ya kuwasaka na kuwamaliza Al-Shabaab ndani ya msitu wa Boni unaoaminika kuwa maficho makuu ya magaidi hao.

Operesheni hiyo ilizinduliwa Septemba 2015.

Inatambulika kwa jina Amani Boni (OAB) na inaendelezwa chini ya uongozi wa Wanajeshi wa Ulinzi Kenya (KDF) kwa ushirikiano na vitengo vingine mbalimbali vya usalama nchini.

Licha ya operesheni hiyo kuendelea kwa karibu mwongo mmoja sasa, visa va Al-Shabaab kupenya kutoka msitu wa Boni na kuingia maeneo mengine ya Lamu kushambulia, kuua walinda usalama na raia na kuharibu mali bado vimekuwa vikirekodiwa, japo kwa uchache ikilinganishwa na miaka kabla operesheni hiyo izinduliwe.

Aidha imefichuka kuwa kabla ya Jenerali Ogolla kufariki kwenye ajali ya helikopta ya kijeshi iliyoanguka na kulipuka eneo la Elgeyo Marakwet Aprili 18, 2024, alikuwa amepanga mikakati kabambe ya kuzuru msitu wa Boni mwezi huu Aprili.

Katika mahojiano ya kipekee na Mbunge wa Lamu Mashariki Ruweida Obo, ambaye alikuwa akishirikishwa pakubwa katika kuiandaa ziara hiyo, ikizingatiwa kuwa ni kiongozi mwenyeji, ajenda kuu ya Jenerali Ogolla kufika msitu wa Boni ilikuwa ni kushughulikia vilivyo na kuweka sawa mambo ili kuimarisha usalama Lamu.

Mbunge huyo anafafanua kuwa miongoni mwa masuala aliyofaa kuyatekeleza Jenerali Ogolla ni kuelekeza jinsi ambavyo miundomsingi, zikiwemo barabara za kiusalama zilifaa kufanywa ili iwe rahisi kwa walinda usalama kutekeleza kikamilifu operesheni inayoendelea ya Amani Boni msituni Boni.

Pia kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wakazi, hasa jamii ya walio wachache ya Waboni kuhusiana na jinsi eneo zima la msitu wa Boni limetelekezwa.

Bi Obo alikiri kuwa utelekezaji wa wana Lamu Mashariki na serikali ni suala linaloendelea kuwavunja moyo wenyeji.

Anasema wengi wamekosa Imani na serikali, hivyo kukosa kabisa morali ya kushirikiana na walinda usalama ili kumpiga vita adui ambaye ni Al-Shabaab.

Hivyo Bi Obo alisema miongoni mwa mambo yaliyomsukuma Jenerali Ogolla kutaka kufika msitu wa Boni yeye mwenyewe kabla ya mauti kumchukua ilikuwa kwamba alitaka kukaa na jamii na kujadiliana masuala ambayo yangehakikisha kuna mabadiliko, hasa ushirikiano kati ya serikali, walinda usalama na wananchi hao.

“Tulikuwa tumeipanga vyema ziara ya Jenerali Ogolla. Azma yake ilikuwa ni kufika msitu wa Boni mwenyewe, aonane na sisi viongozi na wananchi na kujadiliana jinsi tutadumisha umoja katika kumkabili adui. Ninaamini hatua yake ingefaulisha pakubwa vita dhidi ya Al-Shabaab na usalama kurejea eneo hili,” akasema Bi Obo.

Pia alitaja malalamishi ya wavuvi wa Lamu Mashariki kuhangaishwa na walinda usalama wanapokuwa baharini kuvua kuwa miongoni mwa masuala yaliyofaa kushughulikia na Jenerali Ogolla kwenye ziara aliyonuia msitu wa Boni kabla ya kukatizwa na kifo chake.

“Pia tulimtarajia afike kufungua miradi mbalimbali iliyojengwa au kutekelezwa na kukamilishwa kupitia ufadhili wa KDF. Kuna visima vya maji vilivyochimbwa na wanajeshi wetu na kukamilika Basuba, Mangai na Kiunga,” akasema Bi Obo.

Wakazi waliohojiwa pia walikuwa na matarajio kwamba ziara ya Jenerali Ogolla ingesaidia kuzifungua kikamilifu shule zao ambazo kwa miaka mingi zimekuwa zikihudumu nusunusu.

Shule hizo ni Milimani, Basuba, Mangai, Mararani, Kiangwe na Bodhei.

Bw Ali Abdi alisema wamechoka kuona watoto wao, hasa wale wa madarasa ya juu wakisafiri maeneo ya mbali kama vile Mokowe Arid Zone kwenda kutafuta elimu ilhali shule wako nazo vijijini mwao.

“Inasikitisha kuona shule zetu zikihudumia tu wanafunzi wa chekechea hadi Darasa la Nne ilhali wale wa madarasa ya juu wakisafiri sehemu za mbali kila muhula unapoanza kusoma. Ninaanimi ziara ya Jenerali Ogolla ingefaulu mabadiliko yangetekelezwa na hizi shule kufunguliwa kuhudumia madarasa yote,” akasema Bw Ali.

Bi Maryam Gobu, mkazi wa Mararani, alisema anaamini ujio wa Jenerali Ogolla ungeleta mwamko mpya katika vita dhidi ya Al-Shabaab, hivyo kumaliza kabisa visa vya kila mara vya Al-Shabaab kujitokeza na kushambulia Lamu.

“Jenerali Ogolla ni mtu mkubwa na kufika kwake hapa kungemaanisha amri kubwa ya vita kuongezwa nguvu. Ni masikitiko kwamba mpango wake wa kutaka kuzuru msitu wa Boni ulizimwa na kifo cha ghafla,” akasema Bi Gobu.

Mara kwa mara maafisa wakuu jeshini wamekuwa wakizuru msitu wa Boni kutathmini hali na hata kuwatia moyo wenzao wanaoendeleza makabiliano dhidi ya Al-Shabaab.

Kwenye ziara hizo, wakuu hao wamekuwa wakifanya mikutano na wenyeji wa msitu wa Boni, ambapo huwauliza kutoa mapendekezo ya miradi ya maendeleo wanayohisi serikali yafaa iwatekelezee katia harakati za kurejesha hali shwari ya maisha vijijini mwao.

Katika ziara ya awali msituni Boni iliyojumuisha Meja Jenerali Juma Mwinyikai, mbunge Obo, Naibu Gavana wa Lamu Raphael Munyua na wakuu wengine wa usalama, wakazi walihakikishiwa kuwa jeshi halitaondoka ndani ya msitu wa Boni hadi usalama na hali shwari kurejeshwa eneo hilo.

“Majeshi hayataondoka eneo hili. Tutazidi kupigana na wahalifu. Pia tutaendeleza miradi ya maendeleo na yenye kuinua maisha ya mwananchi hapa. Furaha yetu ni kuona msitu wa Boni umebadilika kuwa eneo la amani na utulivu huku maisha ya wananchi yakiendelea hapa kama eneo linguine lolote la Kenya,” alisema meja jenerali Mwinyikai.