Akili MaliMakala

Mambo ya miche, achia wataalamu uepuke hasara

Na LABAAN SHABAAN August 18th, 2024 2 min read

WAKULIMA wengi wasio na uzoefu wa kilimo aghalabu hupata hasara wanapojiandalia miche kabla ya upanzi. 

Ili kuziba ufa huu, kampuni ya kuotesha mimea ya Seed Tech Propagators imekuwa mwokozi kwa wakulima wanaotaabika.

Meneja wa shamba hili Maria Kariuki anakiri kuwa sasa wao ni kimbilio kwa maelfu ya wakuzaji mazao ya chakula kutoka sehemu tofauti nchini.

“Watu wengi huja hapa kutafuta miche hasaa za kabeji,” anaeleza Bi Kariuki. “Miche mingine ambayo tunaotesha ni pamoja na ya sukuma, nyanya, spinach  na vitunguu.  

Shamba hili liko karibu na mji wa Nanyuki Kaunti ya Nyeri ambapo kuna wakulima wengi.

Mbali na Nyeri, wakulima ambao wameondokea kuwa soko la mazao haya ni wale wa Kaunti za Meru, Isiolo na Nairobi.  

Miche hii hukuzwa katika kivungulio (greenhouse) ambacho kimeumbiwa hali bora ya hewa kukuza mimea inayostahimili mazingira tofauti.

Miche ya nyanya katika kitalu ndani ya kivungulio. PICHA | LABAAN SHABAAN

Kulingana na Bi Kariuki, kukumbatia stadi bora za ustawishaji miche huwaokolea wakulima muda wa maandalizi katika vitalu.

Faida nyingine ni kuepuka upanzi wa miche mibovu ambayo hatimaye hunyauka ama kuwa na mazao duni.

Uhusishaji wa wataalamu umesaidia kuafikia uotaji wa asilimia 100 kwa miche iliyotundikwa katika udongo vitaluni.

“Kabeji huwa tayari kupandwa baada ya mwezi mmoja huku mimea mingine kama vitunguu na pilipili hoho ikikomaa vitaluni ndani ya mwezi mmoja na nusu,” alieleza Bi Kariuki.

Seed Tech inafafanua kuwa wao hutumia udongo maalum kuepuka magonjwa yanayotokana na udongo.

Meneja wa shamba la Seed Tech Propagators, Maria Kariuki katika mahojiano na Taifa Leo. PICHA | LABAAN SHABAAN

Hii ni baada ya kugundua wakulima wanaopata hasara wamekuwa wakitumia udongo wa kawaida bila kuutathmini kitaalamu.

Katika maandalizi ya vitalu, Bi Kairuki hutilia maanani kutibu miche kwanza kabla ya kupanda ili kuondoa maambukizi ya magonjwa.

Anaeleza kuwa wakulima hufululiza shambani humo kuchukua miche na idadi hiyo imepanda na kuchochea kupanuka kwa kampuni yao.

“Tulianza na greenhouse moja kwa sasa tuna tatu. Mahitaji ya miche miongoni mwa wakulima yamepanda ndiyo maana kampuni yetu imekua upesi,” anafunguka. 

Unyunyizaji hufuata mtindo maalum wa kumwaga maji yanayotiririka kwa michirizi midogo ili isiharibu miche.

Unyunyizaji maji katika vitalu vya mboga. PICHA | LABAAN SHABAAN

Mradi wa maji wa Ruai eneo hilo unawasaidia kupata maji kwa mfululizo ila wakati mwingine wanakumbana na changamoto ya maji nyakati za kiangazi. 

“Hubidi kununua maji kutoka kwa wauzaji maji nyakati za ukosefu,” anafichua Bi Maria. “Ili tuwe na utoshelevu, imebidi kuteka na kuhifadhi maji ya mvua kwenye tenki za juu.”

Shirika hili la kilimo linalenga kupanua mawanda yake kote nchini na kugusa nyoyo za wakulima kabla ya kulenga masoko nje ya nchi. 

Bi Kariuki anaamini kuwa ili kuafikia ndoto yao, ni sharti wakumbatie mbinu za kisasa za teknolojia katika oparesheni na maenezi ya huduma.