Maoni

Maoni: Fursa na changamoto za Raila katika uchaguzi wa Afrika

Na DOUGLAS MUTUA September 7th, 2024 3 min read

HUKU ukijikuna kichwa na kujiuliza iwapo kweli Gavana wa Nairobi, Bw Johnson Sakaja, aliondolewa kwenye orodha ya waliopangiwa kusafiri na Rais William Ruto hadi Uchina, wengine wanawaza mambo muhimu zaidi.

Madai yaliyotolewa mtandaoni, ila yakakanushwa na Bw Sakaja mwenyewe, ni kwamba safari yake ilivunjwa dakika za mwisho ili nafasi yake ichukuliwe na kinara wa chama cha Orange Democratic Movement, Bw Raila Odinga.

Hata fununu kwamba kuna watu wanaokula njama kumwondoa mamlakani Bw Sakaja si muhimu. Wala si rahisi. Wameru wamejaribu mara tatu kumtungua Gavana Kawira Mwangaza na bado hawajafaulu.

Hivyo ni vioja ambavyo vinamburudisha Mkenya wa kawaida tu, ila kwa mataifa tajiri na yenye ushawishi duniani, wanadiplomasia wanajiuliza swali muhimu: Kwa nini ghafla ikawa lazima Bw Odinga aende Uchina?

Kumbuka huyo si yule Raila wa kawaida tena, aliyewania urais kwa mara tano, akashindwa mara nne kati ya hizo na kuibiwa kura mara moja. SItaki ubishi kuhusu hili, naamini marehemu Rais Mwai Kibaki aliiba kura za Raila katika Uchaguzi Mkuu wa 2007.

Sasa Raila ni mtu mashuhuri mno barani Afrika na kote duniani kwa kuwa anawania wadhifa wa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) katika uchaguzi utakaofanyika mwezi Februari mwakani.

Nimewahi kukuandikia hapa kwamba shughuli zozote zinazoendelea katika Umoja wa Afrika (AU) zinafuatiliwa na kushawishiwa kutoka mbali, hasa na mataifa yanayohasimiana.

Si siri kwamba ushindani, hasa kati ya Amerika, Uchina, Urusi na kadhalika unaendelea barani Afrika, kila taifa likitaka kuiweka Afrika chini ya kwapa lake na kuitumia dhidi ya mahasimu wake.

Usishangae kuwaona Wachina wakijenga miundo-mbinu takriban kila pembe ya Afrika; usione ajabu kwamba Urusi ina Mamluki kwenye bara letu, wanaojasiria kutishia serikali za Afrika.

Sihitaji kukukumbusha kuwa Amerika pia inajenga miundo-mbinu, ina kambi nyingi za kijeshi ndani ya bara letu, sikwambii mipango ya kiuchumi na kisiasa inayonuiwa kuyazuia mataifa yanayoshindana nayo.

Taifa lolote linalotaka kuishawishi Afrika halitaona ugumu kufanya hivyo kupitia mwenyekiti wa AUC, cheo ambacho Raila anakamia si haba, hivyo huenda akasafiri kote kuanzia sasa hadi wakati wa uchaguzi huo wa AUC.

Amerika imekuwa ikitumia mbinu maalum ya kuhusiana na mataifa ya kigeni; badala ya kwenda moja kwa moja katika mahusiano hayo, inalenga miungano ya mataifa kama vile Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC); Ecowas (magharibi); Sadc (kusini) na kadhalika.

Hii ina maana kwamba siasa za AUC ni shughuli muhimu mno kwa Amerika, na lolote linaloivutia Amerika linawashughulisha washindani wake.

Hata hivyo, haina maana kwamba Raila ndiye mwaniaji anayeungwa mkono na mataifa hayo. Labda bado hayajaamua yatamuunga mkono nani, na ndio maana nasisitiza kuwa itamlazimu kufanya kampeni na kuchangisha fedha kote-kote.

Hali ni tete kwa Bw Odinga, hasa ikizingatiwa fununu kwamba mpinzani wake mkuu katika kinyang’anyiro hicho, Bw Anil Gayan, aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Mauritius, anaungwa mkono mataifa mengi yaliyotawaliwa na Ufaransa.

Tangu utawala wa kikoloni uishe, kumekuwa na uhasama mkuu kati ya mataifa yaliyokuwa chini ya utawala wa Ufaransa na yale yaliyotawaliwa na Uingereza. Ukijitokeza mara hii utakula kwa Raila, si mpinzani wake huyo.

Sharti nikwambie kuwa ushawishi wa mataifa tajiri yaliyo nje ya Afrika si kigezo pekee cha kupimia nguvu za mwaniaji; yapo mambo mengine mengi tu ya ndani kwa ndani ambayo yanaweza kushurutisha mkondo utakaofuatwa.

Mathalan, viongozi wa mataifa mengi watamwogopa Raila kwa sababu ya harakati zake za muda mrefu za kutetea demokrasia nchini Kenya. Kumbuka AU ni kama ushirika wa madikteta, hivyo wao na demokrasia ni pamba na moto!

Mazoea ya Raila kuwakaba koo kweli-kweli marais wa Kenya si siri, hivyo hofu ikiyaingia mataifa hayo ya Afrika kwamba kwao kutakuwa na mwamko mpya wa kidemokrasia Raila akiwa mwenyekiti wa AUC, wataingia baridi na kupiga kura dhidi yake.

Tuambizane ukweli: Tukio la mwaka 2018 ambapo Raila, baada ya kushindwa uchaguzi wa urais, alijiapisha na kujiita ‘rais wa watu’ na kusababisha msukosuko wa kisiasa nchini Kenya, litaogofya wengi.

Pamoja na hayo ongeza zile tuhuma dhidi ya Raila kwamba alihusika na jaribio la mapinduzi ya serikali la mwaka 1982, uniambie hali itakuwaje.

Vilevile, tabia zetu Wakenya zinatisha kishenzi! Sisi ni wanoko wa bara hili, hatupendwi. Dunia haijasahau maandamano ya kizazi kipya (Gen G) ambayo yalimtetemesha Rais Ruto akahema na kuunda serikali ya mseto kwa msaada wa Raila.

Ruto angatanua kifua namna gani, kila mtu duniani kote anajua yeye ni manusura tu, labda hangekuwa uongozini Raila asingemnusuru na kumpa tena fursa ya kuishi.

Ikiwa Raila anataka kukabiliana kikamilifu na propaganda yoyote ambayo inaweza kuanzishwa na wapinzani wake, basi na asiwategemee wataalamu wa siasa na mawasiliano ambao wamekuwa wakisimamia kampeni zake za urais nchini Kenya.

Anahitaji walaalamu walio mashuhuri Afrika, hasa kutoka maeneo yote ya bara hili, na pia asitoe hotuba ambazo zitaashiria kuwa anajiona kama rais wa Afrika nzima. Wadhifa anaotaka hautafutwi hivyo. Msasi mtaka mawindo haingii porini na kelele.

[email protected]