Maoni

Bakora ya Rais Trump haibagui Waamerika wala raia wa kigeni

Na DOUGLAS MUTUA February 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIS wa Amerika, Donald Trump, ameunganisha dunia nzima kwa hofu. Hakuna taifa lolote duniani ambalo halijiulizi hii bomoa-bomoa na tishia-tishia ya Trump itaishia wapi.

Anatishia kila mtu, kuanzia Waamerika wenyewe wanaofanya kazi serikalini, wahamiaji wanaoishi Amerika, hadi raia wa mataifa ya mbali ambao, juma moja tu lililopita, hawakujua mishahara yao ilikuwa inatoka Amerika.

Tangu aingie madarakani kwa mara ya pili yapata majuma matatu yaliyopita, Trump ameagiza kusitishwa kwa misaada yote ambayo nchi yake huyapa mataifa ya kigeni.

Agizo hilo litadumu kwa muda wa miezi mitatu, wakati wapambe wake kama kichaa Elon Musk wataweka kila kitu kwenye mizani na kukadiria iwapo kinaendana na sera yake ya ‘Amerika kwanza’, ambayo inalenga kulinda maslahi ya taifa hilo pekee.

Hakika Trump ametuunganisha kwa kuwa anatishia mataifa makuu kwa vikwazo vya ushuru wa bidhaa, ametishia kutwaa Canada iwe sehemu ya Amerika, na pia anamtishia mfanyakazi wa kiwango cha chini aliye barani Afrika na mabara mengine maskini.

Ninapoandika makala hii, tayari nimepokea jumbe za simu na baruapepe kutoka kwa marafiki zangu walio Afrika na ambao walishangilia ushindi wake kwa shangwe wakidhani angewahujumu wahamiaji wanaoishi Amerika pekee.

Walioniandikia wakiniuliza kulikoni ni baadhi ya wafanyakazi wa mashirika ya kimataifa ambao wamesimamishwa kazi – na kuna uwezekano mkubwa kwamba hatimaye watafutwa kabisa – kutokana na agizo hilo la kusitishwa kwa misaada.

Mashirika yaliyowaajiri, kwa kuwa hayana njia nyingine za kupata pesa ili yawalipe, yamewaagiza waende likizo kavu bila hela zozote kwa kuwa mhisani wao mkuu amekataa kuendelea kuwafanyia hisani.

Jumla ya wafanyikazi 35,000 nchini Kenya wanasemekana kuathiriwa na agizo hilo, kwa hivyo inatarajiwa kwamba, watu wengi zaidi watakumbwa na matatizo ya kiuchumi kutokana na ukosefu wa mapato. Tayari Kenya ina ukosefu wa ajira, hivyo tatizo hilo litaongezeka.

Wala usihadaike kwa kusikia eti misaada inayotolewa na Amerika kupitia wakfu wa rais, PEPFAR, itaendelea kuwafikia watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi.

Tuombe Mungu ule mradi wa kujenga barabara kuu kati ya Mombasa na Nairobi, ambao unatekelezwa na Amerika, unusurike makumbo ya Trump.

Kwa Wakenya wanaotaka kuhamia Amerika, ama kusoma au kuishi huko, basi na wajue Trump ameapa kubadilisha au kufutilia mbali kabisa ile bahati nasibu iitwayo ‘Green Card.’
[email protected]