TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inastahili kung’ata na kuwazima wawaniaji ambao wanahusishwa na ghasia wakati huu ambapo kampeni za chaguzi ndogo ziko katika mkondo wa lala salama.

Maeneobunge ya Kasipul na Mbeere Kaskazini yanaonekana kama yanayomulikwa kutokana na cheche kali ambazo zimekuwa zikiendelea kati ya mirengo inayosaka viti hivyo.

Huwezi kufikiria kuwa kuna kampeni ambazo zinaendelea za ubunge Ugunja na useneta wa Baringo kutokana na utulivu ambao umekuwa ukishuhudiwa katika kampeni za chaguzi ndogo za Novemba 27.

Hata Malava ambako kampeni pia zimechacha, kila mrengo umekuwa ukiuza sera zake wala hakuna visa vyovyote vya ghasia ambavyo vimeripotiwa.

Hii ni licha ya kwamba kumekuwa na uhasama mwingi na propaganda kati ya wawaniaji mbalimbali wanaomezea mate kiti hicho.

IEBC inastahili kuangazia kwa jicho la ndani yanayoendelea Kasipul ambako watu wawili tayari wameaga dunia kutokana na ghasia za kisiasa.

Kumekuwa na uhasama mkubwa kati ya wafuasi wa mgombeaji wa ODM Boyd Were na mpinzani wake Philip Aroko ambaye anawania kama mwaniaji huru.

Makabiliano yamekuwa yakishuhudiwa Kasipul kiasi kwamba maafisa kutoka Idara ya Upelelezi nchini (DCI) walizuiwa kuwanyaka washukiwa wa mauaji ya watu wawili.

Ni vyema kwa mwaniaji kuuza sera yake lakini ni jambo baya kwa kijana kufa kwa sababu ya uhasama wa kisiasa.

Bw Boyd mwenyewe amekuwa akilalamikia utovu wa usalama ambapo magari yake ya kampeni yalipigwa mawe na kuharibiwa.

Wakati umefika ambapo IEBC na vyombo vya usalama vinastahili kuchukua hatua na kuzuia uharibifu wa mali na maafa yanayoendelea kushuhudiwa Kasipul.

Ulimwengu hautaisha iwapo Bw Were au Bw Aroka watazuiwa kuwania ubunge wa Kasipul iwapo mirengo yao itapatikana imehusika na ghasia za uchaguzi mdogo eneo hilo.

Ikumbukwe kuwa uchaguzi ni siku moja na Kasipul haitakosa kuwa na mwakilishi bungeni eti kwa sababu Bw Boyd au Aroko wamezuiwa kuwania kura.

Wanasiasa hao wawili hawafai kuwa chimbuko la mauaji ya raia hasa vijana eti kwa sababu tu wanasaka nafasi za uongozi.

Ghasia hizi si geni na zimekuwa zikiendelea hata wakati ambao ODM ilikuwa ikielekea kuandaa mchujo wake.

Wakati huo, hospitali ya Newton Ogada ilivamiwa na kuharibiwa na wahuni na hadi leo haifahamiki iwapo hatua zozote zilichukuliwa dhidi ya walioivamia mchana peupe.

Vyombo vya usalama viwe ange kuhakikisha kwamba uchu wa uongozi hausababishi wanasiasa kufanya raia wauawe.

Kule Mbeere Kaskazini, ni dhahiri ngoma za kivita zimeanza kupigwa hasa kutoka kwa mrengo wa upinzani na serikali.

Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua alidai kuwa kuna mpango wa kufadhili fujo dhidi yake akiendelea kumpigia kampeni kali Newton Karish wa DP.

Upande wa serikali nao unataka Bw Gachagua azuiwe kufanya kampeni eneo hilo eti kwa sababu chama chake cha DCP hakina mwaniaji.

Iwapo uhasama kati ya mirengo hii miwili itaendelea, basi IEBC nayo ichukue hatua badala ya kufumbia macho uchochezi wa wazi unaonezwa na wanasiasa.