Jamii inaugua, tusilaumu hasira au maradhi ya kiakili
VIDEO iliyosambazwa mitandaoni mapema wiki hii iliyomwonyesha barobaro mmoja akimpa kichapo cha mbwa afisa wa polisi imeibua hisia mseto miongoni mwa Wakenya.
Ian Ngige, 19, alifikishwa mbele ya Mahakama ya Milimani akikabiliwa na mashtaka ya uhalifu baada ya kuonekana akimrukia kwa makonde na mateke nusura amuue, afisa wa trafiki mwenye umri wa miaka 55.
Kando na kwamba umri wa afisa aliyepigwa kinyama ni sawa na wa baba yake kijana huyo, ilibainika mhasiriwa anaugua kisukari, hali inayoweka wazi sababu ya kushindwa kujitetea kabisa.
Akijitetea alipotiwa mbaroni, Ian alidai alipandwa na mori baada ya afisa huyo kuingia katika gari lake na kumwitisha hongo ya kiasi kikubwa.
Tukio hilo limezua mdahalo mzito huku baadhi ya Wakenya wakimkashifu vikali kwa hatua aliyochukua na kutaka awe funzo kwa wengine.
Idadi kubwa ya waendeshaji au wanaomiliki magari, hata hivyo, wamempongeza Ian wakirejelea maovu yanayohusishwa na polisi hasa maafisa wa trafiki kuhusu ulaji rushwa.
Kisa hiki kimeangazia uhasama uliopo baina ya polisi na raia ikiwemo kitendawili kigumu kinachowakabili walinda usalama wanapotekeleza majukumu yao, kuhusu kujikinga wakati wa hatari na suala tata la haki za kibinadamu.
Ingelikuwa vinginevyo, video kuenezwa ikimwonyesha afisa wa polisi akimnyorosha chipukizi kwa sababu yoyote ile, mitandao ya kijamii na vyombo vya habari ingelifurika viongozi na makundi ya kutetea haki za kibinadamu wote wakilaani polisi.
Ni muhimu kuzipa kipaumbele haki za kibinadamu lakini ni muhimu zaidi kuzingatia kuwa haki zizo hizo, zinawahusu polisi kwa sababu wao pia ni binadamu kwanza kisha nembo ya mamlaka.
Polisi wana mapungufu yao, kuna wanaohudumia Wakenya kwa dhati na hata kuhatarisha maisha yao wakilinda raia na kuna wengine waliopotoka sawia tu na taaluma nyinginezo.
Tusisahau kamwe afisa huyo aliyeshambuliwa pia ni mwana wa mtu, ndugu, mjomba, mume na baba mpendwa kwa watoto wake.
Isitoshe, hali kwamba kijana huyo alikuwa na ujasiri kiasi hicho kumshambulia kikatili peupe afisa wa polisi aliyevalia magwanda rasmi ya kazi, inatisha.
Katika miaka ya hivi karibuni, visa vya ukatili vimeongezeka kiasi kwamba si ajabu tena kwa wanandoa kuuana kinyama, mtu kumrusha mwenzake kutoka kwa gari linaloendeshwa kwa kasi au kutoka ghorofa la saba.
Japo tumekuwa tukilaumu matatizo ya afya ya akili kila wakati, ni bayana jamii inaugua kutokana na kuzorota kwa maadili na utovu wa nidhamu.