Maoni

MAONI: Dalili Raila akikosa AUC, atarejelea siasa za kusumbua Ruto

Na CECIL ODONGO October 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

UHUSIANO kati ya Rais William Ruto na Kinara wa Upinzani Raila Odinga utakuwa na mashiko au unaweza kusambaratika kutokana na hatima ya waziri huyo mkuu wa zamani katika azma yake ya uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC)?

Bw Odinga ambaye ameanguka urais katika chaguzi tano zilizopita mara hii ameamua kujaribu bahati yake kwenye siasa za Afrika akilenga uenyekiti wa AUC.

Hata hivyo, kiongozi huyo wa ODM anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Waziri wa Masuala ya Nje wa Djibouti Mahamoud Ali Youssouf ambaye hata anaungwa mkono na baadhi ya Wakenya waliokasirishwa na ushirikiano wa Raila na serikali.

Kwa sasa kura hiyo inaonekana ni ngumu wawili hao wakitarajiwa kuimarisha kampeni zao lakini matokeo yake yatakuwa na athari hasi au chanya kwa Rais Ruto ambaye atakuwa akisaka kuchaguliwa kwa muhula wa pili mnamo 2027.

Wikendi iliyopita Mbunge wa Homa Bay mjini Peter Kaluma na Seneta wa Migori Eddy Oketch waliandamana na Rais katika Kaunti ya Uasin Gishu ambapo walimhakikishia kuwa ODM ipo ndani ya serikali.

Bw Oketch alionekana kuwa kibaraka zaidi kwa kudai kuwa sasa uchumi umekuwa dhabiti kutokana na ushirikiano kati ya Rais na Bw Odinga. Naye Bw Kaluma alisema wapo tayari kumtetea Rais dhidi ya uongozi wake kutatizwa na wandani wa Naibu Rais aliyengátuliwa Rigathi Gachagua.

Iwapo Raila atakosa cheo cha uenyekiti wa AUC, basi kuna uwezekano mkubwa utawala wa Kenya Kwanza utakipata. Mwanzo, ni dhahiri kuwa Raila bado ana malengo yake ya kisiasa nchini ndiposa amekataa kuachilia ODM.

Badala ya kuacha ODM mikononi mwa kiongozi chipukizi wa kuijenga upya, amehiari kuiachia Gavana wa Kisumu Profesa Anyang’ Nyongó ambaye ni kiongozi mkongwe ambaye huenda hana ndoto zozote za uongozi akitamatisha muhula wake.

Si siri kuwa Raila, 79 akikosa wadhifa wa AUC basi atarejea nchini na matakwa mapya ya kuunga serikali au aanzishe mikakati ya kuwania urais mnamo 2027.

Bw Odinga kwa sasa ndiyo mhimili wa uongozi wa Rais Ruto baada ya kumwokoa wakati wa maandamano ya Gen Z miezi miwili iliyopita na wabunge wake kuchangia kungátuliwa kwa Bw Gachagua.

Akikosa AUC huenda akataka awe na mkataba wa ushirikiano na serikali ambapo atapokezwa nyadhifa zaidi katika utawala wa sasa. Aidha huenda akaweka masharti makali kuunga Rais Ruto mnamo 2027 ikizingatiwa sasa haya ndiyo maeneo yanayolengwa na Rais baada ya kupoteza uungwaji mkono wa Mlima Kenya.

Raila akiamua kuendea Urais 2027, Rais atakuwa pabaya zaidi kwa sababu hana hakikisho kuwa Mlima Kenya utarejea kwenye kapu lake la kisiasa.

Isitoshe, waziri huyo mkuu anaweza kumwaga mtama na kutumia udhaifu wa Rais Ruto na dhana hasi dhidi ya serikali yake kujivumisha kisiasa.

Kwa sasa Rais ana kazi ngumu ambayo lazima atimize na hilo ni kuhakikisha kwa Raila anafanikiwa AUC ndipo naye awe na matumaini ya kuchaguliwa tena 2027.

Iwapo malengo hayo hayatatimia basi ajiandae kwa kivumbi kikali ambacho kitamwongezea uadui wa kisiasa na kulemeza nafasi yake ya kuchaguliwa tena.