MAONI: Gachagua akitimuliwa, unaibu rais upewe wandani wa Raila, badala ya Kindiki
RAIS William Ruto anastahili kumpa unaibu rais mwanasiasa kutoka ngome za Kinara wa Upinzani Raila Odinga iwapo Naibu Rais Rigathi Gachagua atatimuliwa katika wadhifa huo.
Hoja ya kumtimua Bw Gachagua inatarajiwa kuwasilishwa katika Bunge la Kitaifa wakati wowote kuanzia leo ambapo mchakato wa kumwondoa utaanza rasmi.
Kuna madai kuwa tayari zaidi ya wabunge 300 wametia saini hoja hiyo ya kumng’oa Naibu Rais.
Kwa sasa ni dhahiri kuwa ndoa ya Rais na naibu wake imeingia mdudu hivyo basi kuna uwezekano mdogo sana kuwa wawili hao watashirikiana tena kisiasa 2027.
Kwa ufupi, ni wazi kuwa Rais atakuwa na mgombeaji mwenza mwengine 2027 naye Bw Gachagua pia atalazimika kujipanga, pengine akiwa na matumaini ya kuendea uongozi wa nchi au kuwa mgombea mwenza wa mwaniaji mwengine.
Wikendi, wabunge George Murugara (Tharaka) na Patrick Munene wa Chuka Igambang’ombe walisema wanaunga mkono hoja hiyo ili nafasi ya unaibu rais ipewe Waziri wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki.
Wabunge hao wawili waliendelea kuunga madai kuwa Prof Kindiki ndiye alistahili kupewa wadhifa huo ila Bw Gachagua akatumia ukwasi wake na ushawishi wake kumshurutisha Rais ampe wadhifa huo.
Kuna dhana kati ya wanasiasa wa Kenya Kwanza kutoka Mlima Kenya wanaomuunga Rais Ruto kuwa Bw Gachagua akitimuliwa, basi wadhifa wa mgombeaji mwenza utamwendea Profesa Kindiki.
Hata hivyo, wanastahili kuelewa kuwa mkondo wa siasa umebadilika kwani huenda Rais Ruto hana haja ya kura za Mlima Kenya jinsi ilivyokuwa katika uchaguzi mkuu uliopita.
Hii ni kwa sababu amemleta kambini aliyekuwa hasimu wake wa kisiasa Bw Odinga ambaye anaungwa mkono Magharibi, Nyanza, Pwani na miongoni mwa jamii za wafugaji katika Bonde la Ufa na Kaskazini Mashariki.
Wabunge hawa wanaosema Prof Kindiki apewe unaibu rais wajue kuwa kaunti za Tharaka-Nithi na Meru hazina kura kuliko ngome za Raila ambazo zimemsaidia Rais kunusurika ghadhabu za Gen-Z.
Aidha, ni wazi kuwa Bw Gachagua amefaulu katika kucheza siasa za kuonewa huruma na jamii anakotoka ambayo sasa inamuunga mkono kwa dhati.
Hakuna hakikisho lolote kuwa 2027 hata Prof Kindiki akichukua pahala pa Bw Gachagua, eneo hilo bado litaunga uwaniaji wa Rais Ruto.
Kwa hivyo, Rais Ruto atakapotoa unaibu rais kwa ngome za Raila na ahakikishe kuwa maeneo hayo yananufaika kupitia miradi ya maendeleo, basi atakuwa pazuri kutetea wadhifa wake bila kupata kura za Mlima Kenya.
Kwa sasa Prof Kindiki ana dhana hasi machoni mwa Wakenya kutokana na jinsi vitengo vya usalama vilivyokabiliana na waandamanaji wakati wa maandamano ya Gen-Z mnamo Juni na Julai.
Pia mauaji ya wafuasi wa upinzani wakati wa maandamano ya mapema mwaka jana, yalishuhudia akilalamikiwa kutokana na kiburi alichoonyesha na kuonekana kama mwanasiasa asiyekuwa na utu.
Akipewa unaibu rais, Rais Ruto atakuwa amepoteza zaidi kwani atakuwa amepoteza uungwaji wa sehemu kubwa ya Mlima Kenya na ngome za Raila bado hazitamthamini sana utawala wake.
Wazo bora kwa Rais Ruto kwa sasa ni kutoa unaibu rais kwa mtu wa Raila kama Bw Gachagua ataenda nyumbani kwa kuwa hiii itasaidia sana kupunguza joto la kisiasa nchini.