Maoni

MAONI: Itakuwa kitanzi kwa Ruto kumtema Gachagua ilhali hajui kama Raila atamuunga 2027

Na CECIL ODONGO September 23rd, 2024 2 min read

UTAWALA wa Rais William Ruto haufai kumhangaisha Naibu wa Rais Rigathi Gachagua kwa matumaini kuwa utaungwa mkono na ngome za upinzani za Raila Odinga.

Naibu Rais siku chache zilizopita amekuwa akilalamika kuwa anahangaishwa na serikali ambayo walitafuta pamoja na Rais Ruto mnamo 2022.

Jumapili mwandani wake Cleophas Malala alitoa madai kuwa hoja ya kumng’atua Bw Gachagua inaendelea kusukwa na baadhi ya wabunge wa ODM wakishirikiana na wenzao wa Kenya Kwanza ambao wanaegemea mrengo wa Rais Ruto.

Ukweli ni kuwa ndoa kati ya Rais na Naibu Rais sasa imeingi mdudu na kuna kila dalili kuwa wanasiasa hao wawili watatengana kufikia 2027.

Kutokana na ufichuzi wa Bw Gachagua na hatua ya baadhi ya wabunge kutoka Mlimani kusema hawatafanya kazi naye, ni dhahiri kuwa sasa hatakiwi serikalini.

Hata hivyo, Rais Ruto na baadhi ya wandani wake ambao wanaonekana kuchangamkia Bw Gachagua atimuliwe serikalini, wanastahili kufahamu kuwa kutenga Mlima Kenya ni kosa kubwa kisiasa.

Mwanzo, huenda wanafanya hivi kwa sababu ya kumleta Bw Odinga serikalini lakini kuna uwezekano finyu kuwa waziri huyo mkuu wa zamani atawasaidia 2027.

Ngome za Raila huwa hazipigi kura kwa kishindo kama Mlima Kenya hata kama yuko debeni. Sasa iwapo hawajitokezi kwa winga Bw Odinga akiwa debeni, sembuse asipokuwamo.

Katika uchaguzi wa 2022, Rais Ruto alimbwaga Bw Raila kwa kura 200,000 lakini katika ngome ya Raila ya Nyanza, kulikuwa na zaidi ya watu 700,000 ambao walijisajili kama wapigakura ila hawakujitokeza kumpigia.

Pili, kwa kumtema Bw Gachagua kunamaanisha kuwa Rais Ruto lazima ahakikishe kuwa Bw Odinga anafaulu kwenye azma yake ya kupata uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Tayari Raila anakabiliwa na kibarua kwenye azma hiyo kutoka kwa mwaniaji kutoka Djibouti ambaye anaonekana kuwa kifua mbele kutokana na madai ya kuungwa mkono na mataifa yanayozungumza Kifaransa.

Iwapo Bw Raila ataanguka AUC, basi Ruto atajipata pabaya na kujutia kumtema Bw Gachagua.

Bw Raila ni mwanasiasa mwenye karata kali ambaye anaweza kurejea na kuwania urais kwa mara ya sita kupitia kuanikia maovu yote ya serikali.

Haitashangaza iwapo Raila huyo huyo akipoteza AUC, akishirikiana kisiasa na Bw Gachagua ambaye katika siku chache zilizopita ameonekana kumsifu kuwa si kiongozi mbaya jinsi alivyokuwa akifikiria.

Hata Raila akipata AUC, si hakikisho kuwa atawaongoza wafuasi wake kumuunga Rais kwa sababu naye ana matakwa yake ambayo ni lazima yatimizwe.

Uchaguzi wa 2027 huenda ukawa kibarua kikubwa kwa Rais kwa sababu Gen-Z ambao walitikisa serikali yake nao wameamua kuwa hawataachwa nje tena katika masuala ya serikali.

Wametangaza kuwa watachukua kura baada ya mchakato wa kuwateua Makamishina wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) kukamilika.

Iwapo Gen-Z nao watakuwa na mwaniaji na waamue kwa kauli moja kuwaondoa wanasiasa wanaosema wamesababishia nchi hii mateso makubwa kupitia uongozi mbaya, basi Rais Ruto hatakuwa na lake 2027.

Kumtema Bw Gachagua, Bw Odinga kutomuunga na ukakamavu wa Gen Z 2027 kutafanya iwe vigumu kwa Rais Ruto kuwahi awamu ya pili ya urais.

Hii ndiyo maana Rais na utawala wake unapofurahi masaibu ya Bw Gachagua wafahamu kuwa mbele itakuwa vigumu sana kwao kwa sababu Mlima Kenya nao wanasaka ramani nyingine ya kuwarejeshea urais.