Maoni

MAONI: Mwafrika awe huru kujiamulia mustakabali wa maisha yake

Na DOUGLAS MUTUA June 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KUNA msemo kuwa hata saa iliyovunjika huwa sahihi angalau mara mbili kwa siku. Kwa muda mrefu sana, nimeyakosoa matamshi na matendo ya Rais wa Rwanda, Paul Kagame, kisa na maana udikteta.

Bw Kagame amewakalia mguu wa kausha raia wa nchi yake kwa muda mrefu, na kila anayempinga ama huuawa au akatoweshwa asionekane tena.

Hata hivyo hivi majuzi, amesema jambo fulani likanipa tafakuri, nikajiambia linapaswa kufikiriwa hata ikiwa limesemwa na mkosaji.

Amehoji kwa nini mataifa ya magharibi yanayoringia demokrasia huwa na sheria kali za kuwazuia raia wa kigeni kuingilia siasa za mataifa hayo ilhali wageni huvuruga mambo Afrika wanavyojitakia.

Kama mtu aliyeishi ughaibuni kwa muda, nitakwambia kuwa utachekwa, kudharauliwa na hata kuambiwa ufyate mdomo ikiwa utazuru Amerika au Uropa kisha uthubutu kuingilia siasa za huko.

Hata ukitoa maoni ya kawaida tu kuhusu siasa zao, unaonekana kama kiherehere anayeingilia mambo yasiyomhusu, asiye na kazi ya kufanya, kazi kupoteza muda tu. Na watakwambia peupe: sisi hufanya mambo yetu hivi, hayakuhusu.

Sasa ngoja mtu huyo afike Afrika usikie malalamishi kuhusu demokrasia na mambo mengine yasiyomridhisha! Wakati mwingine unasalitika kujiuliza alialikwa na nani kuingilia mambo yasiyomhusu.

Tukubaliane: ni kweli kwamba makosa yakionekana hata na mgerni ni bora yakemewe; ni kweli kwamba Afrika kumejaa viongozi watundu na dhalimu wasiowaheshimu wala kuwahurumia raia.

Afrika kuna viongozi ambao watafanya kila kitu, hata kuua, ili wasalie madarakani. Watawanyanyasa na kuwatowesha wapinzani wao, mtu mmoja akikosana nao familia yake nzima inafyekwa na isahaulike!

Hivyo basi, kila anayeyataja makosa hayo anapaswa kusikilizwa hata ikiwa si mwenzetu. Ukweli usemwe hata na ibilisi mwenyewe.

Hata hivyo, mataifa ya magharibiu yanayojipa udarai wa kutufundisha demokrasia yanapaswa kujua kuwa demokrasia ni rinda linalomtosha kila mtu; kila taifa lina maadili na tamaduni zake ambazo haziwezi kuondolewa na demokrasia ya kimagharibi.

Ikiwa demokrasia hiyo inakuja kunogesha ubora wa Mwafrika, basi inakubaliwa. Mambo yanaenda tenge tunapolazimishiwa vitu kama ushoga, uavyaji mimba na uozo mwingineo wa kimagharibi.

Kwa kuwa sasa tumefundishwa demokrasia ya kimagharibi na hatutaisahau kamwe, ni heri basi tuachwe huru tuunge ubora wake na ubora wa mifumo iliyokuwa ya Mwafrika tangu mwanzo ili tuwe na mfumo wa kutufaa.

Tusilazimishiwe mambo!

[email protected]