Maoni

MAONI: Ni muhimu kudhibiti matangazo ya kamari kuzima uraibu unaoteka vijana

Na BENSON MATHEKA April 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

HATUA ya serikali kuzima matangazo ya kamari nchini Kenya ni ya busara ikiwa inalenga kukabiliana na uraibu wa kamari unaoenea kwa kasi, hasa miongoni mwa vijana.

Uraibu huu umesababisha madhara makubwa kwa kijamii, kiuchumi na kiafya, na sehemu kubwa ya matatizo haya yamechochewa na mvuto wa matangazo ya kamari katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Matangazo haya mara nyingi huwasilisha kamari kama shughuli ya kufurahisha, yenye mafanikio ya haraka, huku yakificha hatari na hasara zinazoweza kutokea.

Hali hii huwavutia wengi, hasa vijana wasio na ajira, wanaotafuta njia za haraka kujipatia kipato.

Kwa kudhibiti matangazo haya, serikali inazuia kusambaa kwa habari za kushawishi lakini za kupotosha kuhusu kamari, na hivyo kupunguza idadi ya watu wanaoingia kwenye mtego wa uraibu.

Zaidi ya hayo, kudhibiti matangazo kutasaidia kulinda watoto na vijana ambao ni rahisi kushawishika.

Utafiti umeonyesha kuwa vijana wanaotazama matangazo ya kamari mara kwa mara wana uwezekano mkubwa wa kujaribu kucheza kamari wakiwa bado na umri mdogo.

Kamari imehusishwa na msongo wa mawazo, watu kujitoa uhai na familia kuvunjika huku wamiliki wa kampuni za kamari wakijilimbikizia utajiri bila kujali matokeo yake kwa umma na mustakabali wa jamii.

Vile vile, kuna ithibati kuwa baadhi ya zawadi zinazovumishwa kwenye matangazo ya kamari huwa ni hewa na hakuna anayezishinda kwa msingi wa maelezo na kanuni za mchezo. Huu ni utapeli.

Serikali inapaswa kuweka sheria kali kuhusu muda, maudhui, na mahali ambapo matangazo ya kamari yanaweza kuwekwa.

Aidha, wadau wa habari na mitandao wanapaswa kuwajibika kwa kuhakikisha kuwa hawachangii kueneza uraibu huu.

Kwa jumla, kuzima matangazo ya kamari ni njia muhimu ya kushughulikia tatizo la uraibu na kulinda ustawi wa jamii nzima, hasa kizazi cha sasa na kijacho.