Maoni

MAONI: Ni ukatili kuadhibu wanafunzi kwa kuwarushia vitoza machozi

Na WANTO WARUI April 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

JUMA hili, katika shule ya msingi ya Melvin Jones, Kaunti ya Nakuru, wanafunzi wa shule ya Upili ya Wasichana ya Butere walitua kuwasilisha mchezo wao wa kuigiza maarufu kama “Echoes of War”.

Wanafunzi hao walitarajiwa kuuwasilisha mchezo wao ukumbini saa mbili asubuhi, jambo walilopinga kutokana na sababu kuwa hawakuwa na mwelekezi wao na nyenzo za kutumia wakiigiza.

Badala yake, waliamua kuimba wimbo wa taifa, wakatulia kimya kwa muda wa dakika moja kisha wakaondoka ukumbini.

Hata hivyo, jambo lililozua mtafaruku ni kisa cha askari cha kuwarusha wanafunzi wale vitoza machozi.

Wanafunzi hao ambao huenda walikuwa wa chini ya miaka kumi na minane (18), walidai kuruhusiwa kuwasilisha mchezo huo chini ya uongozi wa mwelekezi wao na mwandishi wa mchezo huo, aliyekuwa Seneta, Cleopas Malala.

Kukosa kwa mwelekezi huyo ndiko kuliwafanya kuteta wakishangaa alikokuwa.

Kwa kawaida, hili halikuwa jambo la kutumia nguvu kupita kiasi kwa wanafunzi hao.

Pia soma https://taifaleo.nation.co.ke/habari/habari-za-kitaifa/ian-mbugua-ni-aibu-kwa-ruto-kuvuruga-wanafunzi-wa-butere-girls-kuonyesha-ugwiji-wao-katika-usanii/

Lilikuwa ni suala tu la kuwasikiliza wanafunzi watoe malalamishi yao kisha waigize au wakose kuigiza maana hao wenyewe hawasababishi fujo.

Uhalali wa mchezo huo ulikuwa umethibitishwa na mahakama ambayo ilikuwa imeruhusu mchezo ufanyike kama ilivyopangwa.

Ingawa kuna vipengele vya mchezo huo ambavyo huenda vilikashifu serikali, mwandishi wa mchezo hakuwa mwanafunzi wala mwalimu.

Ilistahili kumkabili yeye mwenyewe ikiwa alikuwa amefanya makosa na afikishwe mahakamani kujibu mashtaka.

Wanafunzi walikuwa tu wakitekeleza wajibu wao wa kuwasilisha igizo kulingana na mafunzo waliyokuwa wamepewa.

Kabla ya igizo hilo kufika kiwango hicho cha kitaifa, bila shaka lilikuwa limekaguliwa mara kadhaa na wakaguzi ambao pia ni walimu.

Vile vile, wanafunzi hao walikuwa wakifanya mazoezi shuleni mwao, thibitisho kuwa hata mwalimu mkuu wa shule yao alikuwa na ufahamu kamili kuhusu mchezo wenyewe.

Hao ndio walistahili kurekebisha mambo mapema kama kulikuwa na dosari.