MAONI: Polisi wakome kuvamia wanahabari wa michezo viwanjani
KATIKA siku za hivi karibuni, wanahabari wa michezo nchini wamevamiwa na maafisa wa polisi, jambo ambalo linafaa kuingiliwa kati kabla hali haijakuwa mbaya zaidi.
Kisa cha hivi karibuni kilitokea Jumapili iliyopita (Aprili 27, 2025), katika uwanja wa Dandora jijini Nairobi ambapo mpiga picha wa Nation Media Group (NMG) Chris Omollo alivamiwa na afisa wa polisi, alipokuwa akiingia uwanjani kupiga picha mechi kati ya Ligi Kuu ya Wanaume (KPL) kati ya Gor Mahia dhidi ya Mara Sugar.
Omollo alipigwa kichwana na polisi na kujeruhiwa vibaya na kukimbizwa katika hospitali ya Aga Khan jijini Nairobi ambapo, alilazwa kwa siku kadhaa kutokana na jeraha la kichwa.
Omollo akiwa na wenzake waliripoti kwamba, walipojitambulisha kama wanahabari kwenye lango la kwanza uwanjani Dandora, mhudumu aliwaelekeza kwenye lango lingine ambalo lilikuwa na msongamano kutoka kwa mashabiki ambao hawakuwa na tiketi.
Lango linalofuata lilikuwa limejaa mashabiki na kwa sababu Omollo alibeba vifaa vizito vya kazi, alikaribia afisa moja kwa moja na kujitambulisha ili pamoja na wenzake waruhusiwe kuingia saa 20 kabla ya mechi kuanza.
Baada ya kujitambulisha na beji zao za NMG, afisa mmoja alimpiga Omollo kwa nguvu nyuma ya kichwa bila kutarajia na kumfanya kuanguka.
Shirikisho la Soka nchini (FKF) pamoja na Chama cha Wanahabari nchini (SJAK) Jumanne, Aprili 29, 2025 walikashifu vikali unyama huo na kuahidi kwamba uchunguzi utafanywa kwa kina na Omollo apate haki.
Si Omollo tu, wanahabari wengine wa michezo pia wameripoti kwa SJAK kuwa, wamehangaishwa na maafisa wa polisi wakiwa nyanjani.
Inasikitisha kwamba, polisi ambao wamepewa majukumu ya kulinda wanahabari na mashabiki viwanjani, wamegeuza sehemu hizo mahala pa kuwashambulia, kuwarushia vitoza machozi na kuwajeruhi bila sababu.