MAONI: Ruto anapaswa kuelewa kwamba urafiki wake na Museveni haufai kitu ikiwa utawaumiza raia
KATIKA taifa la watu wenye akili timamu kama Kenya, kuna faida gani kumteka nyara kiongozi maarufu wa upinzani wa taifa jirani kama Dkt Kiiza Besigye wa Uganda?
Ni hivi majuzi tu ambapo nimekuandikia hapa kwamba Kenya imekuwa uwanja wa watekaji nyara, si wa ndani kwa ndani tu, bali pia wa kimataifa.
Inasemekana kwamba Dkt Besigye alitekwa nyara mnamo Jumamosi iliyopita jijini Nairobi baada ya kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa kitabu cha ‘Against The Tide’ (Dhidi ya Mawimbi) kilichoandikwa na mwanasiasa mbishi, Bi Martha Karua.
Bi Karua alikuwa mgombea-mwenza wa kinara wa Muungano wa Azimio, Bw Raila Odinga, katika Uchaguzi Mkuu uliopita, na ingawa Bw Odinga amesharidhiana na Rais Willaim Ruto aliyemshinda, Bi Karua angali mkosoaji mkali sana wa utawala wa sasa wa Kenya.
Mke wa Dkt Besigye, Bi Winnie Byanyima, amesisitiza kwamba mumewe alitekwa nyara jijini Nairobi, na sasa amezuiliwa katika jela ya kijeshi nchini Uganda.
Akiishinikiza serikali ya Uganda imwachilie huru mumewe bila masharti yoyote, Bi Byanyima ameuliza inawezekanaje mumewe akazuiliwa katika jela ya kijeshi ilhali yeye si mwanajeshi?
Kutekwa nyara kwa Dkt Besigye nchini Kenya kuna maana kubwa ya kisiasa kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Je, viongozi wetu, ambao wanajulikana kwa kutukandamiza, wameungana kusaidiana katika kutudhibiti kisiasa?
Hivi unakumbuka kwamba wanaharakati wa kisiasa 36 waliohusishwa na Dkt Besigye walitekwa nyara mjini Kisumu mwezi Julai mwaka huu na kurejeshwa Uganda, ambako walifunguliwa mashtaka ya uhaini?
Ikiwa Dkt Besigye, aliyewahi kuwania urais wa Uganda kwa mara nne, alivunja sheria zozote za Kenya, kwa nini hakushtakiwa kwenye mahakama za Kenya?
Kwa kumteka nyara na kumkabidhi kwa serikali dhalimu ya dikteta Yoweri Kaguta Museveni, Kenya imekuwa mshirika wa mnyanyasaji huyo ambaye ameitawala Uganda kwa miaka 38!
Si siri kwamba mataifa hushirikiana kisheria kubadilishana washukiwa, lakini ushirikiano huo hufuata mchakato halali ambapo kibali cha kumsafirisha mshukiwa hadi anakotakikana hutolewa na mahakama. Kwa nini mchakato huo haukufuatwa katika kisa cha Dkt Besigye?
Je, ni kosa la uhaini kwa Waganda walio na mwamko wa kisiasa kuzuru Kenya? Si tumetembeleana na Waganda siku zote hata wakati ambapo serikali zetu hazikushirikiana? Si tumeoana na kuzaliana nao siku zote?
Kisa cha Dkt Besigye kinatufundisha nini kuhusu makubaliano ya mataifa wanachama wa EAC kwamba raia wao wanaweza kutembelea kokote bila kuhitaji viza za kusafiria?
Hivi nikizuru jiji la Kinshasa walikotokea wahenga wangu takriban miaka 700 iliyopita nitarejea salama au nitasingiziwa uhaini na kurejeshwa Kenya na kuozea jela?
Ukweli ni kwamba wananchi wa mataifa yote ya EAC hatuna tatizo na uhuru wa kutembeleana, hakika tunaufurahia, ila viongozi wetu ndio wanaohofia kuwa tukishirikiana na kuinuka pamoja hawataendelea kutukalia migongoni huku wakinyofoa chumi zetu kama minofu.
Ikiwa hujui, maandamano ya kizazi kipya, almaarufu Gen-Z, yaliyotokea nchini Kenya yaliwahofisha viongozi wa Eneo la Maziwa Makuu, na Afrika kwa jumla, hivyo huko kutembeleana hakuwakai vizuri.
Haikosi wamejipata kwenye njia-panda kwa sababu ushirikiano wa kisiasa kati ya mataifa wanachama wa EAC, ambao wamezembea kuhuisha miaka yote hii, unaweza kuota na kukita mizizi bila idhini yao. Tangu hapo mjinga akierevuka, mwerevu huwa mashakani!
Kenya inajichafulia jina kwa kumteka nyara Dkt Besigye siku si nyingi zilizopita tangu raia wanne wa Uturuki watekwe na kusafirishwa upesi hadi nchini kwao ambako walitupwa jela!
Kumbuka kisa cha kuatua moyo ambapo mwanahabari wa Pakistan, Bw Arshad Sharif, aliuawa nchini Kenya katika hali ya kutatanisha mnamo Oktoba 23, 2022. Wapakistani bado hawajatusamehe, na baadhi yao wanaamini mwenzao huyo aliuawa kwa sababu za kisiasa.
Ushirikiano wa kimataifa hufanikishwa na wananchi, si serikali. Raia wa taifa lolote lile akijua kuwa si salama kuzuru Kenya atajikalia kwao au azuru nchi nyingine. Hivyo ndivyo sekta yetu ya utalii inavyokosa wateja huku ya Tanzania ikinawiri.
Ushirikiano wowote kati ya mataifa unapaswa kuwanufaisha, si kuwadhulumu wananchi. Dkt Ruto anapaswa kuelewa kwamba urafiki wake na Museveni haufai kitu ikiwa utawaumiza raia. Viongozi ni wapita-njia, wenye nchi ni raia.