MAONI: Sharti Serikali ichukue hatua kukomesha visa vya polisi kugeuka wahalifu
POLISI wanapaswa kuwa nguzo ya usalama na ulinzi katika jamii, lakini wakati wanaposhiriki katika vitendo vya uhalifu, wanaacha jamii bila kinga.
Hali hii inahatarisha usalama wa wananchi na inavunja imani kati ya umma na vyombo vya usalama, ambayo ni muhimu sana kwa utulivu na ustawi wa taifa.
Katika hali ya kawaida, polisi wanapaswa kuwajibika kwa uadilifu usio na doa, kulinda raia, kutoa huduma za dharura, na kuhakikisha sheria zinaheshimiwa.
Lakini wanapovunja sheria na kuwa wahalifu, wanatishia usalama wa jamii na kufanya raia kuhisi kuwa iko katika hatari zaidi.
Katika mazingira kama haya, ni vigumu kwa wananchi kuamini kwamba polisi watawasaidia katika hali ya dhiki au kushughulikia matatizo yao.
Madai ya uhalifu miongoni mwa maafisa wa polisi yanahitaji kuchunguzwa kwa kina na hatua kuchukuliwa ili kurejesha imani ya wananchi kwa huduma ya polisi.
Kwa hakika, inapaswa kuwa huduma lakini hili limebaki kwa maandishi tu ilivyonakiliwa katika katiba. Ikiwa hali hii itapuuziliwa mbali, itakuwa vigumu kwa raia kutafuta haki na usalama wao kwa maafisa wa usalama.
Hata kama serikali itachukua hatua dhidi ya polisi wahalifu, bado kuna haja ya kubadilisha mifumo kuanzia mafunzo, na udhibiti ili kuhakikisha kuwa maafisa wa polisi wanawajibika kwa vitendo vyao na kuleta ufanisi katika kutekeleza majukumu yao.
Ukweli usiopingika ni kuwa ikiwa polisi ndio wahalifu, basi jamii inaweza kushawishika kuchukua sheria mikononi kwa kukosa imani na maafisa hao wa usalama na hii ni hatari kwa nchi.
Katika hali hii, ni muhimu kuwa na mifumo ya kuripoti na kushughulikia vitendo vya polisi vinavyokiuka haki za raia.
Serikali lazima itie msisitizo katika uadilifu wa maafisa wa polisi na kuhakikisha kuwa hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi ya wahalifu wote, iwe ni raia au maafisa wa polisi.
Hii itarudisha imani ya raia kwa maafisa wa usalama.