MAONI: Tusidanganyane, umaarufu wa Trump umechochewa na rangi yake na itikadi kali
WAAMERIKA watapiga kura siku mbili zijazo kuchagua rais mpya, na chochote kinaweza kutokea. Athari za shughuli hiyo zitasambaa kote duniani.
Ipo kauli isiyopendwa na wengi ambayo husema kuwa Amerika ikipiga chafya tu, kila nchi inapata mafua, hivyo Kenya, na Afrika kwa jumla, haiwezi kujitia hamnazo kuhusu uchaguzi huo.
Aliyekuwa rais, Bw Donald Trump, atapambana na Makamu wa Rais wa sasa, Bi Kamala Harris, katika kinyang’anyiro kinachotabiriwa kuwa chenye ushindani mkubwa zaidi katika historia ya taifa hilo.
Tayari wawili hao wametoa hotuba za kufunga kampeni, hivyo watu wengi wameamua watamchagua nani, lakini makundi yao ya kampeni yangali mashinani yakijaribu kuwashawishi watu wachache ambao bado hawajaamua ni nani watakayemchagua.
Kura za maoni zinaonyesha kuwa yeyote kati yao anaweza kuibuka mshindi, jambo ambalo limewaduwaza wengi walio na akili razini.
Nimesema walio na akili razini kwa sababu nadhani idadi ya watu walio na kichaa imeongezeka kote duniani, na Amerika ni sehemu ya dunia.
Vinginevyo, utanisadikishaje kwamba dunia haina vichaa wengi ikiwa mtu kama Trump, na madhaifu yake yote, angali mshindani mkuu katika nchi inayojivunia demokrasia na utawala wa kisheria?
Trump, bwanyenye mtundu aliye na matusi zaidi ya maneno matamu katika msamiati wake, ni mhalifu aliyekutwa na hatia katika mashtaka karibu 40.
Hicho ndicho kizungumkuti ambacho kinawazuga wengi akili wakajipata wakijiuliza maswali wasipate majibu: Kwa nini umaarufu wa Trump haufifii hata akihusishwa na kashfa ya aina gani? Ingekuwa mtu mwingine kama vile Kamala ingekuwaje?
Ikiwa wahalifu hawaruhusiwi kupiga kura Amerika, kwa nini mhalifu aruhusiwe kuwania urais wa Amerika, ofisi kuu zaidi duniani?
Hivi wafuasi wa Trump ndio kina nani hao wasiomuacha hata wakati ambapo kila mwanadamu anapaswa kumuambaa kama jini au shetani?
Akishinda uchaguzi, hatima ya kesi nyingine nyingi ambazo ziko mahakamani ni gani? Na akishindwa atafungwa jela kwa makosa ambayo tayari amehukumiwa?
Moja kwa moja, tena bila kificho, nitakwambia kuwa Trump anasaidiwa na uzungu wake! Ni suala la ubaguzi, au mapendeleo ukipenda, yaliyojikita katika rangi ya ngozi yake.
Angekuwa mtu mweusi, mtu wa asili ya Asia na kadhalika, hata bila kushtakiwa mahakamani, hangepata watu wa kumuunga mkono na kumwezesha kushinda uchaguzi wa mchujo ili afikie alipo.
Makosa mengi anayofanya, yakiwepo yasiyomithilika wala kuandikika hapa ya kujikwaa ulimi, yanafumbiwa macho na kuzibiwa masikio na watu wanaofanana naye kwa sababu baadhi yao wanamwona kama mwokozi wao. Wana visingizo tele vya kumtakasa.
Tafiti kadhaa zinaonyesha kwamba Wazungu wanaendelea kupungua nchini Amerika kwa sababu wanazaa watoto wachache, huku wahamiaji wakimiminika humo kwa fujo na kuzaa watoto wengi.
Inatabiriwa kuwa katika muda wa miongo michache tu, Wazungu ndio watakaokuwa wachache Amerika, na ukweli huo unawashtua sana, hasa wale wasiowahi kutangamana kwa karibu na watu wa asili nyingine.
Ukipiga soga nao wanakuuliza ungehisije ungeona jamii yako, ambayo imetawala dunia kwa miaka mingi tu, ikiondolewa mamlakani na watu wasiochukuliwa kuwa wa asili ya nchi hiyo.
Ukweli ni kwamba Amerika ni taifa la wahamiaji, hata Wazungu ni wahamiaji, tofauti kati yao na wahamiaji wa hivi majuzi ni kwamba walitangulia.
Trump pia anapata uungwaji mkono kutoka kwa vikundi vya wahamiaji ambao wamekengeuka; wapo wanaoamini ni Mkristo mwenzao kwa sababu chama cha Republican anachowania kwacho kinadai kupendelea sera za imani kwa Mungu na familia.
Usishangae nikikwambia kuwa baadhi ya Wakenya wanaoishi Amerika walifunga na kumuombea Trump alipomenyana na rais wa sasa, Bw Joe Biden, mnamo mwaka 2020.
Walitamauka sana Trump aliposhindwa, wakalia kuwa shetani ameshinda uchaguzi. Sababu nyingine za Wakristo hao kumuunga mkono Trump ni kuwa chama cha Republican kinapinga ushoga na uavyaji mimba.
Hata hivyo, sera hizo haziendani na mienendo ya Trump mwenyewe: anawachukia na kuwatukana wahamiaji, tena imethibitishwa kisheria kwamba yeye ni mbakaji na tapeli mkuu. Hizo si sifa za muumini, hivyo Wakristo wa kweli hawawezi kujihusisha naye.
Ni kweli kwamba Wazungu wengi wenye itikadi kali wanaomuunga mkono wanafanya hivyo kwa kuamini kuwa atalishughulikia suala nyeti la uhamiaji, lakini msukumo wao ni chuki.
Kulishughulikia wanakotamani kuna maana ya kufunga mipaka ya Amerika, kuweka vikwazo kwa wanaonuia kuhamia au kutembelea nchi hiyo, na vilevile kuwafukuza wahamiaji ambao tayari wanaishi Amerika.
Trump mwenyewe ameahidi kuwarejesha kwao wahamiaji zaidi ya milioni 12 iwapo atachaguliwa. Ahadi hiyo imewasisimua Wazungu wengi wanaolalamika kwamba ushuru wanaolipa unatumiwa kuwasaidia wahamiaji wasio na vibali vya kuishi Amerika.
Wapo pia wahamiaji ambao kimya-kimya wanatamani Trump achukue jukumu la kuwazuia wahamiaji zaidi kuingia Amerika ili isalie kuwa nchi ya Wazungu. Wanataka upekee wa uzunguni uhifadhiwe.
Hiyo ni aina ya watu ambao ni sahihi kusema wana akili punguani; wanadhani kwamba wamefanikiwa sana kwa kuishi katika nchi iliyo na Wazungu wengi, hivyo hawataki ipoteze upekee wa kuwa nchi ya kizungu.
Kwa nini changamoto wa kisheria hazimlemazi Trump? Wataalamu wa kikatiba wanasema hakuna sheria inayomzuia mhalifu kuwania urais Amerika. Kisa na maana? Walioandika Katiba hiyo hawakutarajia kuwa mhalifu atapata fursa ya kuwania urais!
Trump mwenyewe ametishia kuwa iwapo atachaguliwa, atatumia mamlaka ya urais kujisamehe makosa yote hayo, hivyo hakuna yeyote atakayewahi kumtia gerezani. Hilo pia ni suala jipya kisheria kwa kuwa Amerika haijawahi kujipata katika hali hiyo.
Swali la iwapo Kamala akishinda Trump atakwenda gerezani linaweza kujibiwa ‘ndio’ na ‘la’ kwa sababu ikiwa anapatikana na hatia kwa mujibu wa sheria za serikali kuu, labda rais Kamala anaweza kumhurumia na kumsamehe ili kuleta maridhiano nchini.
Hata hivyo, rais hawezi kumsamehe katika hali ambapo amepatikana na hatia kuhusiana mashtaka ya majimbo. Hapo hata Trump mwenyewe hawezi kujisamehe, hivyo atakwenda gerezani.
Ingawa Kenya haina ushawishi wowote katika uchaguzi wa Amerika, ni muhimu sana kwa Wakenya kuufuatilia kwa makini kwa sababu utakuwa na athari kuu kwao, na haijalishi mshindi atakuwa nani.