MAONI: Tuwapinge wakoloni wa kisiasa
HIVI aliyeturoga sisi Waafrika ni nani? Hilo ndilo swali ambalo, kwa mujibu wa Biblia Takatifu, Mtume Paulo aliwauliza Wagalatia waliokubali kupotoshwa na makuhani waongo.
Nimesalitika kuliuliza baada ya kushuhudia chaguzi kadha barani Afrika ambapo watu wasiofaa kukaribia ikulu wametutishia na kutunyamazisha kabisa, yaani wakajipa majukumu ya kututawala bila hiari yetu, nasi tumenywea tu kana kwamba tukiwapinga tutaangamizwa.
Aibu iliyoje kwamba mkongwe Rais Paul Biya wa Cameroon amechaguliwa juzi kwa muhula wa nane, Allasane Ouattara wa Ivory Coast amechaguliwa kwa muhula wa nne, naye Samia Suluhu Hassan wa Tanzania amewaengua wapinzani wote ili kuwania urais peke yake!
Utadhani Waafrika wamekwenda safari za mbali, wakarejea nyumbani na kupata makosa yote hayo keshatendeka, lakini ukweli ni kwamba sote tumo mumu humu, akili tunazo, lakini ujasiri wa kuwakataa na kuwafukuzia mbali wakoloni wa kisasa hatuna.
Labda swali linaloafiki kikweli katika muktadha huu ni tofauti kidogo na lile la kurogwa lililoulizwa na Mtume Paulo: Waafrika, ni nani aliyetuhasi sote tukakosa maguvu na ujasiri wa kuwakabili nduli wanaotutawala kiimla?
Siku moja kabla ya uchaguzi wa Tanzania kufanyika, polisi walimiminika barabarani na magari makubwa ya kivita ili kuwatishia wananchi walionuia kuandamana kupinga uchaguzi huo usiokuwa wa haki.
Hiyo imekuwa desturi ya polisi wa Tanzania kila wakati wananchi wakitishia kuandamana ili kutetea haki zao. Walifanya hivyo wakati wa utawala wa mwendazake John Magufuli, dikteta aliyenuia kurejesha utawala wa chama kimoja ila akafa kabla ya kutimiza ndoto hiyo.
Juzi ilipofika siku ya uchaguzi, intaneti ilizimwa mchana kutwa, jioni polisi wakatoa amri ya kutotoka nje wakihofia kuwa maandamanao na ghasia zilizotawala mchana mzima zingezagaa hadi usiku wa kiza. Hiyo ni ithibati kwamba serikali ilijua imepoteza umaarufu pakubwa.
Maovu waliyofanya marais Biya, Ouattara na Samia hayakubaliki kamwe, lakini hakujawa na watu wa kutosha kuwakabili na kuwazuia kuendelea kunata madarakani. Wanawezeshwa na vyombo vya dola, yaani asasi za watu Weusi zinatumika kuwanyanyasa Weusi wenzao.
Inaonekana Mwafrika ameridhia kunyanyaswa. Amekubali kuishi huku kapiga magoti badala ya kufia haki yake akiwa wima. Jiulize hali ingekuwaje mkoloni angalirejea kututawala tena. Je, kizazi cha kisasa – kinachojali tu kuhusu uwepo wa mlo na bando za simu – kingemkabili.
Hivi majuzi ulijionea mkongwe wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, akiwasihi Waganda wampe fursa ya mwisho ya kuwatawala, awanie urais mapema mwakani, eti kuna miradi ambayo anahitaji kukamilisha ilhali amewaongoza kwa miaka 39.
Hali ni hiyo-hiyo nchini Rwanda. Paul Kagame amekuwa mamlakani tangu alipopindua serikali mnamo mwaka 1994, na ananuia kunata hapo mpaka mwaka 2039. Yeyote anayethubutu kumkabili au kumkosoa anapotezwa au kuuawa ili awe funzo kwa wengine wenye nia kama hiyo.
Huenda ukasema Kenya hatuna tatizo hilo, lakini nimewasikia watu kadha, hasa wanaoiunga mkono serikali ya sasa, wakipendekeza kuwa mtawala wa sasa, Dkt William Ruto, anapaswa kuondoa ukomo wa mihula ya urais ili atawale milele.
Unaweza kupuuzilia mbali uvumi huo, lakini hata mambo makubwa ambayo yamewahi kufanyika huanza kwa uvumi kisha yakaja kuwa ya kweli, hasa kwa kuwa yanatokana na habari ambazo huvujishwa na dola ili kukadiria ilivyo ghadhabu ya wananchi.
Kenya, isipokuwa uhuru wa kujieleza, ina tabia za kidhalimu za mataifa mengine ya jirani: matumizi ya nguvu, utekaji, mashtaka ya kusingizia, sheria kandamizi zinazoandikwa na kupitishwa kisiri.
Juzi imebainika kwamba hata ule mswada wa kifedha ambao ulisababisha maandamano mabaya ya kizazi kipya cha Gen – Z mwaka jana nchini Kenya uligawanywa kwa miswada minne midogo na ukapitishwa kimya-kimya.
Kabisa hakuna tofauti kati ya mkoloni mweupe aliyewatesa mababu zetu na huyu mweusi anayeamini hatupaswi kumwambia kitu, nasi tunaonekana kujipa hamnazo kuhusu maonevu yake. Tunahitaji mwamko mpya pembe zote za Afrika.