MAONI: Uchumi bora unahitaji viongozi wenye maadili si vyama vipya
MFUMO wa vyama vingi vya kisiasa ulianzishwa mnano 1991. Tangu wakati huo, Kenya imepiga hatua kubwa sana kidemokrasia.
Vyama vingi vimewawezesha wananchi kuwa na uhuru wa kushiriki katika siasa kwa kujiunga na vyama hivyo, kupiga kura na kushiriki katika mazungumzo ya kitaifa kuhusu masuala mbalimbali hasa ya kisiasa na kiuchumi.
Fauka ya hayo, Kenya imekuwa na vyama vingi vinavyoshiriki katika siasa na uchaguzi mkuu.
Hata hivyo, mfumo huu wa vyama vingi vya kisiasa ndio umekuwa donda sugu katika kuimarika kwa maisha ya mwananchi kiuchumi kwani umechangia baadhi ya viongozi kukosa kuwajibika na badala ya kubadili tabia zao wakakimbilia kuanzisha vyama vipya kwa kizingizio ya kuleta mabadiliko mapya.
Kila wakati wa uchaguzi unapowadia, vyama vya kisiasa vya awali hutelekezwa na wanasiasa kubuni vyama vipya.
La kustaajabisha ni kuwa, katika vyama hivyo vipya, tabia zao huwa ni zilezile. Changamoto huanza punde tu uteuzi wa wawaniaji katika vyama hivyo unapokosa uwazi.
Baadhi ya wawaniaji huamua kuomba kura kama wagombea huru kwa madai kuwa vyama hivyo vimekosa uwazi.
Hili ni thibitisho kuwa si kila wakati chama humchagua mgombeaji ambaye ni chaguo la wananchi.
Kwa sababu hii, Kenya inahitaji viongozi wenye maadili kuliko kuwa na vyama vipya vya kisiasa.
Viongozi wenye maadili watahakikisha kuwa haki za kimsingi za kikatiba zimeheshimiwa, kuna uwazi katika kutoa nafasi za ajira na matumizi mema ya mgao wa fedha katika kaunti na maeneo bunge.
Viongozi wema watarejesha matumaini ya wananchi kuwa viongozi wanajali mahitaji yao.
Wananchi wanapowaamini viongozi wao wataonyesha uzalendo na kuwajibika zaidi katika kulipa ushuru na kuitumikia nchi yao.
Viongozi wenye maadili watasababisha wananchi kuwa na uhuru wa kutoa mapendekezo badala ya kuikosoa serikali mara kwa mara na kuandaa maandamano yanayoishia katika vurugu kwani watakuwa na hakikisho kuwa mapendekezo yao yatatiliwa maanani.
Viongozi wenye maadili watapitisha sheria wakiongozwa na hitaji la mwananchi.
Watakuwa na sera zinazopanua soko la bidhaa za kilimo nchini na kupunguza bidhaa za kigeni ili kuimarisha uchumi nchini.
Nafasi za ajira zitapatikana Wakenya wanapojihuzisha katika shughuli za kuzalisha mali nchini kuliko wanapotegemea kukua kwa uchumi katika mataifa mengine ili wapate kazi huko.
Msimu wa wanasiasa kujipanga katika vyama vipya umewadia. Ni vyema wananchi wawapige msasa wanasiasa kwa kuzingatia maadili yao kuliko vyama vyao vipya.
Kuwepo kwa jina jipya la chama kusisababishe wananchi kusahau tabia ya mwanasiasa yeyote.
Tuwe tayari kuchuja waliozembea na kubaki na wenye bidii na maadili ya kuhakikisha uchumi wa nchi yetu umeimarika zaidi ili kupunguza changamoto zinazotukumba.
Tegemeo la uchumi bora ni viongozi wenye utu si vyama maarufu.