Maoni

MAONI: Utamu wa pesa unajulikana Mlimani

Na DOUGLAS MUTUA April 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

PESA ni tamu. Tena tamu sana! Ndio maana pale kwetu Mlimani hatuzitukani wala kuzikalia vikao vya kuzidhalilisha.

Na hatujui kuna pesa chafu. Eti tuseme pesa ni mbaya? Tangu lini? Unawezaje kuzichafulia jina?

Si hata wahenga wenyewe walisema pesa ni mvunja mlima, nao wajuaji wa mitaa hii wakaongeza kuwa ni sabuni ya roho?

Mwenzako nitaongeza kuwa pesa ni kiburudisho cha kweli. Ukiziona, hata kama si zako, unatabasamu kwa kuzitamani. Unasema ‘laiti zingalikuwa zangu…’

Umewahi kusikia kauli kwamba pesa zikizoea kupitia mikononi mwako – hata kama si zako; pengine umeajiriwa benki tu – uso wako unaanza kung’aa, nao mwili kunawiri? Labda ni kweli… nadhani.

Ni kutokana na ukweli huu mwingi tu ambapo nashangaa kwa nini marafiki wa mwenyeji wa Ikulu wanaotokea Mlimani hawamwambii kweupe: huwezi kuchafua pesa katika eneo hilo.

Wala asikwambie mtu unaweza kuzitumia kuuvunja Mlima kikweli, eti uwe tambarare. La hasha! Mambo mengine hata hayafikiriki.

Kuvunjika kwa mlima katika muktadha huu ni kule kuyeyuka kwa nyoyo zetu kwa kiasi fulani, tukakubali kujitokeza kukusikiza, mradi unalipa.

Na ni kulipa vizuri, si Sh200. Hizo hata hatumpi mtoto kununulia peremende siku hizi. Zikishaingia mkononi, basi! Usijali nanunulia bangi, pombe, unga au sukari.

Zimekuwa zangu sasa; zako tele ulizobakisha sikuulizi unanuia kuzifanyia nini.

Na mwaka 2027 ukifika tutaongea kana kwamba hatukuwahi kukutana hata mara moja.

Hiyo itakuwa biashara mpya, haitawezeshwa kwa muamala mzee wa mwaka 2025.

Sisi wenyeji wa Mlimani tunaweza kushangazwa na madai mengineyo ambayo ‘Kaongo’ ametoa dhidi ya mwanetu wa Wamunyoro, lakini hilo la Sh10 bilioni halitushangazi kamwe.

Hiyo ni biashara nzuri. Mwanetu alikuwa anatafuta mali, kitu ambacho kinafurahiwa sana kwetu, kwa hivyo tunaelewa alikuwa katika harakati za kuukimbia umaskini, auache kwa kona saba!

Tumevunjika nyoyo kiasi tu kwa kuwa shinikizo hilo la Sh10 bilioni halikuzaa matunda. Angalizipata zingalikuwa zimewaajiri watu wengi sana wa eneo letu kwa kuwa hangezificha chini ya godoro.

Amini usiamini, hata leo hii ‘Kaongo’ akimpa mwenzetu mwingine fursa ya kutagusana naye katika ngazi hiyo, kisha waachane bila angaa jaribio la mwenzetu kuondoka na mafedha, mwenzetu atakuwa ametuangusha sana.

Wewe endelea kutucheka tu, lakini ukweli wa mambo ni kwamba hatukatai pesa.

Na usithubutu kusema eti tunapenda pesa sana. Hata wewe unapoamka asubuhi na mapema huendi kuokota kuni za kupikia uji.

Umuhimu wa hela ni siri tuliyogundua kitambo sana. Ukiwa nazo unaweza kuwalipa watu wakutukanie mtu, kisha ukae kitako na kutazama wakizichapa kishenzi!

Unaweza pia kuwalipa watu wakushangilie hata kama unayosema ni upuuzi mtupu.

Na kwetu sisi hakuna lolote baya hapo kwa sababu aliyelipa na anayelipwa wanafurahia. Mlalamishi ni nani? Ni heri kutumia akili kuliko kuchosha akili.

[email protected]