Maoni

MAONI: Viongozi wa kidini wanaambia serikali ambacho raia wanahofia kusema

Na BENSON MATHEKA November 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KWA muda wa zaidi ya miaka miwili iliyopita, Kenya imekumbwa na hali isiyoeleweka huku kila kitu kikionekana kwenda yombo.

Raia wamekuwa wakilia kwamba wanalemewa na hali ngumu ya maisha chini ya utawala wa sasa lakini hakuna aliyekuwa akisikia kilio chao huku wawakilishi waliowachagua katika mabunge ya kaunti na ya kitaifa wakiunga sera za serikali.

Usalama ulibaki kwa wanaounga serikali huku wanaokosoa serikali wakitekwa nyara na maafisa wa usalama wanaokanusha kufanya hivyo na kukosa kuchukua hatua za kuwasaka.

Mawakili waliojaribu kutetea waathiriwa wa ukiukaji wa haki waliweza tu kupata maagizo ya mahakama ambayo hayakuheshimiwa na walio mamlakani huku watu wakiendelea kuuawa kiholela.

Ni baada ya kuona hali na mwelekeo mbaya wa nchi huku raia wakikosa wa kuwasaidia ambapo viongozi wa kidini waliamua kuchukua hatua na kukosoa serikali, wa hivi punde wakiwa Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini ambao hawakusaza serikali ambayo imekuwa ikitumia kila aina ya mbinu kuzima sauti zinazoikosoa ili ionekane haina makosa na kwamba ni serikali pekee inayoweza kusema ukweli hata pale inapoua demokrasia inayotoa haki kwa kila raia.

Hata kabla ya kuchanganua taarifa ya maaskofu kuweza kubainisha masuala waliyoibua, viongozi na maafisa wa serikali walikurupuka na kuanza kuwakosoa.

Kwa kufanya hivi, waliendeleza kile ambacho maaskofu hao na viongozi wengine wa kidini wamekuwa wakilaumu serikali kwa kufanya. Iwapo serikali haitabadilisha mbinu zake za kushughulikia malalamishi ya umma, hali itazidi kuwa mbaya.

Kwa hakika, viongozi wa kidini wanasema kile ambacho raia wanaogopa kusema wasiandamwe na serikali. Iwapo watanyamaza au kunyamazishwa, Kenya itakuwa katika giza kuu.