MAONI: Wanasiasa waige Rose Muhando wajitolee kwa yote wayafanyayo
NYIMBO ni kati ya vipera muhimu vya fasihi simulizi. Moja ya sifa kuu ya nyimbo ni kuwa chombo cha burudani.
Mmoja wa wasanii wa ngoma za injili Rose Muhando kutoka Tanzania ni mbobezi wa nyimbo ambazo zimeacha kumbukumbu kubwa hususan Kenya aliko na lukuki ya mashabiki.
Mimi nilianza kumsikiza mapema miaka ya 2000. Si kwamba nilikuwa mlokole mno la, pia sikuwa mpagani.
Nilikuwa mtu ninayejielewa. Tunachojifunza kwa Rose Muhando ni kuwa, ukipewa jukumu fanya kwa dhati ya moyo wako vizazi vitakukumbuka.
Kenya, jamii ya wanasiasa inaaminiwa sana pengine baada ya Mungu. Kwa umaarufu hao ni wa pili.
Baadhi ni “miungu” kwa wafuasi wao.
Je wanayofanya sasa hivi mbali na hadithi za barabara, mitego, mundu khu mundu na vitendawili nini kingine kinaweza kumbukwa na umma 2050?
Mfano wa Rose Muhando na nyimbo zake unatakiwa kutuonesha umuhimu wa uthubutu katika maisha.
Wakati huu watu wameibuka na kufanya sarakasi kuhusu miziki ya Rose Muhando kama Mteule na ile ambayo Watanzania husema “imevunja kabati” ama vijana wa Gen – Z kuita “kufinish Kumalo” ni wimbo wa Amina.
Unaigizwa na vizazi tofauti na ni midundo iliyoshamiri katika miaka ya 2000.
Hata mimi nimejaribu hiyo “challenge” lakini pale pa kuanguka chini huwa najiepusha nisije nikavuruga mipango ya mishipa yangu.
Ni gumzo tu.
Wanasiasa wa wakati huu wanatakiwa kuwa na utambulisho wao katika ngoma zao za siasa.
Katika miaka ya nyuma, kulikuwa na kina Rose Muhando wa siasa.
Mathalan kundi la ‘Seven bearded Sisters’ lilikuwa kundi pinzani ndani ya chama kimoja cha KANU kutoka 1979 hadi 1983 hivi.
Walijumuisha James Orengo, Koigi wa Wamwere, Mashengu wa Mwachofi, Dkt Chibule Wa Tsuma, Chelagat Mutai, Abuya Abuya na Lawrence Sifuna.
Wanakumbukwa hadi leo kwa juhudi zao za kulikomboa bunge kiasi cha kumkera aliyekuwa waziri wa sheria na Mwanasheria Mkuu wa kwanza wa Kenya huru Charles Mugane Njonjo.
Baadhi yao wana ile misimamo bado kama James Orengo ambaye hanyamazi haki za watu zinapohujumiwa.
Kenneth Matiba na Charles Rubia walifungwa kwa kupinga matokeo ya kura za mlolongo wakati Rais Moi hakuwa mtu wa kujibiwa akishika lake.
Martin Shikuku anakumbukwa kuwa muumini mkubwa wa majimbo tangu siku za KANU na KADU.
Jaramogi Oginga Odinga anatambuliwa kuwa baba wa upinzani wa kweli. Hao ndio akina Rose Muhando wa siasa za Kenya. Watu wanaonukuliwa na kuigwa na jamii pana ya Wakenya.
Kama Rose Muhando anavyosema “nipishe nipite” wao hupita vizuizi vya siasa bila kujali.