Maoni

Maslahi ya wanasiasa yanachelewesha kuundwa upya kwa tume ya IEBC

Na BENSON MATHEKA December 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MJADALA kuhusu kuchelewa kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) umebadilika kuwa lawama.

Ishara zote zinaonyesha kuwa wanasiasa wakuu na washirika wao wana maslahi tofauti na matarajio ya wapigakura.Huku wapigakura wakilenga kuwa na tume ya kusimamia masuala ya uchaguzi na mipaka ikiwemo kujaza viti vya uwakilishi vilivyo wazi ili wapate haki ya uwakilishi, wanasiasa wana malengo tofauti ambayo hawawezi kutamka.

Ni maslahi ya wanasiasa hao yaliyosambaratisha tume iliyosimamia uchaguzi mkuu wa 2022.Kama haingesambaratishwa kwa kushinikiza makamishna watatu waliotofautiana na matokeo ya urais ya uchaguzi huo kujiuzulu na mmoja kutimuliwa kupitia mchakato uliokuwa na ushawishi wa kisiasa, IEBC ingekuwa na makamishna wanne kwa wakati huu na mjadala wa sasa haungekuwa.

Wapigakura wa maeneo 11 hawangekuwa wamenyimwa haki yao ya uwakilishi. Inashangaza licha kelele za wanasiasa kuhusu hali ya IEBC, hakuna anayeona dharura iliyopo ya kuwapa haki wakazi wa maeneo yasiyo na mwakilishi katika bunge la kitaifa na mabunge kadhaa ya kaunti.

Kwa wanasiasa wakuu wanaoweza kufanikisha kuundwa kwa tume hiyo, muhimu kwao ni uchaguzi mkuu wa 2027 ambao kiti cha urais kitakuwa kikigombewa.

Hii inadhihirishwa na kauli za wanasiasa hao na washirika wao kwamba serikali ya sasa itashinda muhula wa pili huku wapinzani wao wakisema itaenda nyumbani.

Ni hali hii inayosababisha mvutano kuhusu uanachama wa jopo la kuteua makamishna wa IEBC ambayo inapaswa kuwa huru.

Hivyo basi, ni wazi kuwa ikiwa pande zote hazitakubaliana katika mfumo huru wa kuunda tume hiyo, lawama zitaendelea hata ikiundwa hadi uchaguzi mkuu wa 2027 jinsi ilivyokuwa katika uchaguzi wa 2022.