Maoni

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Tukithirishe kuwakumbuka waliotangulia mbele ya haki

Na HAWA ALI July 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SIFA zote njema anastahiki Mwenyezi Mungu Azzan wajalla, swala na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad Swallallahu Alayhi Wasallam.

Hakika mauti ni jambo la hakika lisiloepukika. Mwenyezi Mungu Azzan wajalla amesema katika Kitabu chake kitukufu: Kila nafsi itaonja mauti.”(Surat Aali Imran: 185).

Hili ni onyo na ukumbusho kwa kila mwanadamu kwamba dunia si maskani ya milele, bali ni sehemu ya mapito, na kila mmoja wetu atarudi kwa Mola wake ili ahesabiwe kwa aliyo yafanya.

Katika masiku haya ya huzuni, tumehuzunishwa sana na taarifa ya kifo cha Kadhi Mkuu wa Kenya, Sheikh Abdulhalim Hussein, ambaye amezikwa jana.

Inna Lillahi wa Inna Ilayhi Raji’un. Kifo chake ni pigo kubwa si tu kwa familia na jamaa zake, bali kwa Umma mzima wa Kiislamu nchini Kenya na nje ya mipaka yake.

Alikuwa kiongozi mwenye hekima, mcha Mungu, na mwenye kujitolea katika kuhudumia Uislamu na jamii.

Mwenyezi Mungu ampe malipo mema kwa kila lililo jema alilotenda katika uhai wake, amsamehe makosa yake, na amuingize katika rehma Zake zisizo na mipaka.

Mtume wetu Muhammad Swallallahu Alayhi Wasallam alituusia tukithirishe kumkumbuka mauti, kwani mauti ndiyo mkatishaji wa ladha na starehe zote.

Hakuna mwenye mamlaka ya kuichelewesha au kuharakisha; inapowadia haina muda wa kuongezewa wala kupunguzwa.

Ni wajibu wetu, kama Waislamu, kutafakari juu ya maisha yetu kila siku na kurejea kwa Mola wetu kwa toba ya kweli kabla haijachelewa.

Kwa hivyo, tunapomkumbuka Kadhi Mkuu Abdulhalim Hussein, tujikumbushe nasi kuwa tupo katika foleni hiyo hiyo ya mauti.

Tusitawishe nyoyo zetu kwa malengo ya dunia pekee, bali tujiandae kwa safari ya Akhera kwa matendo mema, uchamungu, na unyenyekevu kwa Mola wetu.

Tumuombe Mwenyezi Mungu Azzan wajalla amsamehe Kadhi wetu, ampe makazi bora kabisa katika Jannatul Firdaus, awatie subira wafiwa na jamii ya Kiislamu kwa ujumla.

Tumuombe pia atuwezeshe sisi tuliobaki kuishi maisha ya uongofu na kumaliza maisha yetu kwa laa ilaha illaLlah Muhammadur Rasulullah.