Maoni

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Ya Rabi tujaalie amani duniani, maafa yamezidi

Na ALI HASSAN February 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KWA jina la Mwenyezi Mungu mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na neema ndogo ndogo. Tumejaaliwa leo hii siku hii bora na tukufu kukumbushana na kuambizana mawili matatu kuihusu dini yetu tukufu ya Kiislamu.

Ilivyo hasa ni kuwa kitabu chetu kitukufu cha Kurani kimetuhimiza kukumbushana. Na pia mafunzo ya dini yetu hii tukufu yanahimiza kuisaka elimu ya dini popote pale ilipo.

Awali ya yote tuchukue uzito wa nafasi hii murua kumhimidi, kumshukuru, kumtukuza na kumuenzi Muumba wetu Mwenye-Enzi, aliyeumba ardhi na mbingu na vyote vilivyomo, Allah (SWT).

Ama katika usanjari uo huo, twamtakia kila la kheri na kumtilia dua Mtume wetu (SAW). Leo hii ndugu yangu, na kama ambavyo tumekuwa tukifanya siku hadi siku, tunazidi kuiombea dunia – na hasa bara la Afrika – kuwa na amani.

Maisha hayana thamani wala utu ikiwa kila kona ni mitutu ya bunduki, risasi, mabomu na vilipuzi vya kila aina. Ndiyo maana, kwa uwezo wake Mola wetu Mtukufu, tutazidi kuhubiri amani na kutakiana heri.

Vipo vita vya aina aina. Hata tu ugomvi wa nyumbani ni vita. Hivyo basi tunaomba suluhu kwa kila aina ya suitafahamu yoyote ile.

Baadhi ya maeneo yamekuwa kwenye vita tangu hapo. Hadi leo. Ya Rabi. Ni muda sasa tangu Urusi kuanza mashambulizi yake ya zana kali kali dhidi ya Ukraine. Hadi nukta hii makabiliano hayo yangali kuendelea.

Athari zake ni mauaji, uharibifu wa makazi na kuvuruga kabisa uchumi kote duniani.

Vita vya Gaza vimekuwepo kwa muda sasa. Sawa na mashambulizi ya Israel katika eneo la Lebanon, sikwambii Iran na kwingineko.

Nafuu ilikuwa imeanza kupatikana kwenye ukanda wa Gaza.

Tukasema Alhamdulillahi. Hii ikitokana na mwafaka wa kusitishwa kwa vita vilivyokuwepo ambapo Wapalestina wengi wamehama makwao. Uharibifu wa makao. Mauaji na majeraha kusambaa kote.

Lakini tena ni kama kidonda kinatoja damu. Hadi tunapoyaandaa makala haya, hali ilikuwa inatokota! Gaza ikisema kuwa Israel imekiuka makubaliano ya kusitisha tandabelua hilo.

Nayo Israel, ambayo imepata nguvu mpya na kiburi kutoka kwa rais wa Marekani Donald Trump, ikisema kuwa kama Gaza haitowaachilia mateka wake (Waisrael) kufikia Jumamosi, basi jeshi lake limesimama wima wima kuendeleza mashambulizi dhidi ya Palestina.

Subhannalla!

Ongezea hilo kwa machafuko ambayo yanashuhudiwa nchini Sudan, Sudan Kusini, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo na unaona umuhimu wa kuzidisha dua na maombi ili suluhu ya amani ipatikane duniani.

Ijumaa Mubarak